Mfungaji wa Bao la ushindi la Young Africans kwenye mchezo wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara dhidi ya Simba SC Feisal Salum ‘Fei Toto’, amefunguka namna alivyochukua maamuzi ya haraka ambayo yaliiwezesha timu yake kutinga Fainali ya michuano hiyo.
Feisal amezungumza na kueleza udhaifu wa wapinzani wao ambao ulipelekea kupiga shuti langoni mwa Simba na kufunga bao la ushindi katika dakika ya 25 ya mchezo huo, uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba Jumamosi (Mei 28).
“Nilikuwa nawaangalia viungo wa Simba wanavyocheza, uzuri wao na udhaifu wao, kuna baadhi ya wachezaji wanaocheza eneo la kiungo hawana kasi, ni wachezaji wazuri, lakini wana udhaifu huo, hivyo nikatafuta ni jinsi gani ya kuutumia udhaifu huo. Siyo kila mchezaji amekamilika, hata mimi nina madhaifu yangu,” amesema Fei Toto ambaye pia huichezea Taifa Stars na timu ya Taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes.
Amesema siri ya kupiga mashuti ni mazoezi binafsi ambayo anayafanya, lakini pia uthubutu kwani siyo kila shambulizi ni lazima wachezaji wafike hadi kwa golikipa.
“Nimefunga mabao haya msimu huu kama matatu hivi, unajua kuna maeneo ukisogea unaona umjaribu kipa, golikipa naye ni binadamu, zingine zinakataa, zingine huwa zinakubali. Nilisogea nikaona sikabwi, na kuna nafasi ya kupiga, nikapiga mwanangu kambani, mnyama kafa.” Amesema huku akiangua kicheko.
Mchezaji huyo alijiunga na Young Africans mwaka 2018 kwa namna ya kushangaza, kwani asubuhi alitambulishwa kama mchezaji wa Singida United, lakini jioni akatangazwa kuwa mchezaji wa ‘Wananchi’. Kabla ya ‘sinema’ hiyo, mchezaji huyo alikuwa akiichezea JKU ya Zanzibar.