Home Habari za michezo BINGWA MSIMU HUU KUPATIKANA MEI 24 AU JUNI 16…YANGA AKITELEZA TENA KIDOGO...

BINGWA MSIMU HUU KUPATIKANA MEI 24 AU JUNI 16…YANGA AKITELEZA TENA KIDOGO TU..SIMBA HUYOOO…


Kama sio Mei 24, basi kabla ya Juni 16, bingwa wa Ligi Kuu Bara atakuwa ameshafahamika kutokana na ramani ya ubingwa wa ligi hiyo ilivyo kwa sasa baada ya vigogo, Simba na Yanga kulazimishwa sare na Namungo na Ruvu Shooting.

Simba ambao ni watetezi walilazimisha sare ya 2-2 ugenini dhidi ya Namungo, wakati watani wao wanaoongoza msimamo kwa sasa, Yanga ilitoka suluhu na Ruvu mjini Kigoma juzi na kujiweka katika nafasi nzuri ya kulibeba taji hilo kama itakomaa mechi zijazo.

Matokeo ya timu hizo yaliifanya Yanga izidi kujikita kileleni na alama zao 56 baada ya mechi 22, huku Smba ikifikisha pointi 43 katika mechi zao 21 na hesabu sasa zinaonyesha Yanga inahitaji alama 15 tu ili ifikishe pointi ambazo hazitafikiwa na yoyote.

Kama Yanga itashinda mechi tano tu kati ya nane ilizonazo mkononi itafikisha pointi 71, ambazo hazitaweza kufikiwa na Simba ambayo hata kama itashinda michezo yao tisa itaishia kufikisha alama 70.

Ramani ya ubingwa kwa Yanga inaweza kurahisishwa iwapo Simba itachemsha kwenye baadhi ya mechi zao tisa zilizosalia kukamilisha msimu na kufanya mechi za mwisho za vinara hao kuwa kama za kukamilisha ratiba tu kwa msimu huu.

Ratiba inayonyesha Yanga katika mechi tano zijazo ambazo kama itashinda mfululizo basi itautangaza ubingwa kabla ya Juni 16 na iwapo Simba itateleza katika mechi zao badi hata Mei 24 haifiki itakuwa tayari imebeba taji lao la 28 la Ligi ya Bara tangu 1965.

Yanga itaanza kuvaana na Tanzania Prisons Jumatatu ijayo jijini Dar es Salaam kabla ya kuifuata Dodoma Jiji mjini Dodoma watakaovaana nao Mei 15 halafu itarudi Dar kuialika Mbeya Kwanza katika mechi itakayopigwa Mei 21 kabla ya kusafiri hadi Mwanza kucheza na Biashara United katika mchezo utakaofanyika Mei 24.

Mechi yao ya tano itawakutanisha na Wagosi wa Kaya, Coastal Union itakayopigwa Juni 15 kwenye uwanja wa Benjamini Mkapa na kama mambo yatawaendea vyema basi ponti 15 itakazovuna zitatosha kuwapa taji la 28 la Ligi Kuu Bara wakipora taji kwa Simba.

Hata hivyo, Yanga inapaswa kuwa makini kwa mechi hizo tano kutokana na rekodi za wapinzani wao kwa mechi za duru la kwanza na hata kwa msimu uliopita.

Kuvaana na Prisons na Mbeya Kwanza zinazopambana kushuka daraja inaweza kuwapa ugumu katika mbio hizo za ubingwa.

Mbeya Kwanza inaburuza mkia kwa sasa, ikiwa na pointi 18, wakati Coastal ipo juu yao na alama 21 ikifuatiwa na Prisons iliyokuwa uwanjani jana huku ikiwa na pointi 22.

Timu hizo tano zote zinapambana kujinasua na janga la kushuka daraja hivyo zitaipa Yanga wakati mgumu japo wanajangwani wanajivunia ubora wa kikosi chao na rekodi za mechi za duru la kwanza dhidi ya timu hizo tano za kuwapa ubingwa, kwani iliichapa Prisons 2-1, ikailaza Dodoma 4-0, ikaitandika Mbeya 2-0 huku Biashara ikipigwa 2-1 na ikainyoa Coastal 2-0.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA ALHAMISI

Mambo yakiwa hivyo kwa Yanga, upande wa Simba ambao imekubali yaishe katikam kutetea ubingwa wao inaoushikilia kwa misimu minne mfululizo nazo ina mechi tisa za kibabe ambazo ni lazima ishinde zote, huku ikiiombea Yanga ipoteze baadhi ya mechi na kutetea taji kimiujiza.

Simba baada ya sare na Namungo itarudi uwanjani Jumapili kuvaana na Ruvu Shooting ambao imekuwa na desturi ya kuisumbua, japo katika duru la kwanza ilibamizwa mabao 3-1.

Baada ya hapo itacheza dhidi ya Kagera Sugar, Azam, Geita Gold na KMC na kwenye mechi za awali ni Kagera ndio imekuwa ikiisumbua Simba timu hizo zinapokutana na hata kwenye duru la kwanza Wekundu walilala kwa bao 1-0 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

WASIKIE WADAU

Msemaji wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema bado wana mechi nane na bado wapo katika malengo ya ubingwa, hivyo wana mechi tano za kuhakikisha wanakamilisha lengo lao.

“Licha ya kwamba tumepata sare, hatujatetereka katika kutimiza malengo yetu ya ubingwa. Bado tuna mechi nane na tunataka tutimize lengo letu katika mechi nne zijazo,” alisema Bumbuli, huku Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema sare dhidi ya Namungu imezidi kuwaweka katika nafasi finyu ya kutwaa ubingwa msimu huu.

“Ngoma ni ngumu kweli kweli kutwaa ubingwa msimu huu, kila shabiki wa Simba ajue tu. Kwa sasa tunacheza kuhakikisha mashabiki wetu wanafurahi, hata kama hatutatwaa ubingwa lakini tukishinda kwenye mchezo wowote kwa sasa mashabiki wa Simba watafurahi

“Isifike mahali ukakosa ubingwa vile vile ukaumiza mioyo ya watu, mashabiki wanatakiwa wakikaa waseme, ndio msimu huu tumepambana lakini tumezidiwa,” alisema Ally.

Naye Beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, George Masatu alisema kimahesabu Simba ina nafasi ndogo ya kuchukua ubingwa msimu huu, ila kwenye soka lolote linaweza kutokea .

“Timu itakayojipanga vizuri katika mechi ziliobaki ndio itakuwa bingwa kwa sababu mechi bado nyingi na wengi tunaona Simba hana nafasi tena ya ubingwa msimu huu lakini soka lina maajabu yake hivyo tusubiri tuone hadi mwisho timu itakayopata pointi ambazo haziwezi kufikiwa na mwenzake ndio itajulikana bingwa nani,” alisema Masatu na kuongeza;

“Nani alitegemea Simba itatoka sare na Namungo au Yanga itatoka suluhu na Ruvu? Hapo ndio utajua kuwa soka lina maajabu yake na soka dakika 90 sio kubashiri.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here