Home Habari za michezo ILE ISHU YA CLEOPHACE KUTUA SIMBA YAINGIA ‘KIRUSI’….MABOSI ZAKE WAIBUKA NA KUMVUTA...

ILE ISHU YA CLEOPHACE KUTUA SIMBA YAINGIA ‘KIRUSI’….MABOSI ZAKE WAIBUKA NA KUMVUTA JUU KWA JUU…


UONGOZI wa Dodoma Jiji FC umesema umefikia katika hatua nzuri ya mazungumzo ya kumbakisha klabuni hapo kiungo wake, Cleophace Mkandala ambaye anawaniwa na Simba na Yanga zote za jijini Dar es Salaam.

Mkandala ameonyesha kiwango kizuri msimu huu na kuanza kuhusishwa na mipango ya kuondoka Dodoma Jiji FC.

Katibu Mkuu wa Dodoma jiji FC, Fortunatus Johnson alisema nyota huyo bado ana mkataba na timu hiyo ambayo unaisha Julai 30, mwaka huu na mazungumzo ya kumwongezea mkataba mpya yamefika hatua chanya.

Johnson alisema taarifa za nyota huyo kutakiwa katika klabu hizo anaziona katika mitandao, jambo ambalo wamelazimika kukutana na kiungo huyo kwa ajili ya kuwekana wazi na hatimaye kusaini mkataba mpya.

“Hatuna mpango wa kumwacha Mkandala, licha ya muda wa mkataba wake uliobakia unaruhusu kuzungumza na timu nyingine, hatuna hofu juu ya hilo kwa sababu tuko na mazungumzo mazuri na nyota huyo ya kuongeza mkataba mpya kusalia ndani ya Dodoma Jiji FC,” alisema kiongozi huyo.

Aliongeza klabu hiyo ina matumaini makubwa ya kumbakiza nyota huyo kwa sababu wana nafasi ya kuendelea katika mikiki mikiki ya ligi hiyo kwa msimu ujao.

“Mipango yetu kwa sasa ni kuhakikisha tunashinda michezo sita iliyosalia ili kujiweka katika katika nzuri ya kuendelea kubakia katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, tunaamini nafasi na uwezo wa kupambana tunao,” Johnson alisema.

Naye Mkandala alilsema kuwa kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu anapigania timu yake kupata matokeo mazuri katika michezo iliyobakia ya msimu huu.

Mkandala alisema yeye bado ni mchezaji wa Dodoma Jiji na sasa nguvu na akili zake ziko katika kuhakikisha anasaidia timu yake hiyo kufikia malengo na kupata matokeo mazuri.

“Unajua sitaweza kusema lolote kwa sasa kuhusu mkataba wangu lakini nikuambie nguvu zangu ni kuhakikisha Dodoma Jiji inaendelea kubaki katika Ligi Kuu, baada ya hapo ndio nitaweka wazi juu ya hatima yangu kuendelea kutumikia Dodoma au kwenda kujaribu changamoto kwa timu ambayo itanihitaji,” alisema Mkandala.

SOMA NA HII  KUHUSU TAARIFA ZA YANGA KUWAPULIZIA DAWA WAARBU JUZI...TFF NAO WATIA NENO...MSIMAMO WAO HUU HAPA...