Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI NA AZAM…NABI KAAMUA KULA SAHANI MOJA NA BANGALA…MOLOKO APEWA MBINU...

KUELEKEA MECHI NA AZAM…NABI KAAMUA KULA SAHANI MOJA NA BANGALA…MOLOKO APEWA MBINU MBADALA…


Kocha wa Yanga, Nassredine Nabi amesema ili kufanya vizuri kama ilivyokuwa msimu uliopita anataka wachezaji kupambana na kushinda dhidi ya timu kubwa kama ilivyo michezo inayofuata na fasta akawapa kazi maalumu nyota wake akiwamo Yanick Bangala na Jesus Moloko.

Nabi alisema amewaeleza wachezaji kulingana na ushindani mashindano ya ndani ili kufanya vizuri wanatakiwa kupambana kupata matokeo mazuri kwenye michezo dhidi ya Azam, Simba na timu nyingine ambazo wanachuana nazo kwenye mbio za ubingwa msimu huu.

Kocha huyo aliyeiongoza Yanga kucheza mechi 39 bila kupoteza tangu ilipofungwa na Azam Aprili 25, mwaka jana, alisema ushindani wa Simba na Azam ni mkali na Yanga katika kila mashindano na mara nyingi moja kati ya watatu hao huchukua ubingwa mashindano ya ndani.

“Tunahitaji kucheza kwa umakini mkubwa, mbinu nyingi kulingana na vile ambavyo nawaelekeza katika mazoezi na wapinzani vile ambavyo wanakuja na kujitoa kila mchezaji kutimiza majukumu yake pamoja na nidhamu naamini mwisho wa mchezo tutashinda,” alisema Nabi.

“Mara nyingi mechi kubwa dhidi ya Simba na Azam zinakuwa na mbinu nyingi kuliko matumizi ya nguvu. Naamini hata hii inayofuata itakuwa hivyo kulingana na wapinzani wetu walivyoimarika msimu huu ndio maana nimekaa na kuzungumza na wachezaji wajipange.

“Kuna programu maalumu wakati huu katika mazoezi tunafanya kiufundi pamoja na yale ya nguvu kwani kuna vitu niliviona kutoka kwa wapinzani ndio maana tunafanya aina hizo mbili za mazoezi ili kwenda kuwakabili.

“Kupambana zaidi dhidi ya mechi kubwa kama hii ya Azam sio kama tumezidharau timu nyingine, hapana, bali tunawaheshimu kwani bila kupata ushindi dhidi yao pia ni ngumu kufikia mafanikio ya kufanya vizuri na kushinda mataji kama malengo yalivyo.”

Kocha huyo alisema kuna baadhi ya wachezaji wamebaki kutokana na wengine kuitwa timu ya taifa, ila hilo sio tatizo kwani kila mmoja atapokea alichomwandalia.

Nabi alisema wachezaji waliobaki kama Jesus Moloko, Stephane Ki, Fiston Mayele, Yanick Bangala na wengine kila mmoja anatakiwa kulinda kiwango chake ili wakiungana na walio katika timu ya taifa wawe sawa katika utimamu wa miili. “Tunahitaji kurudi na nguvu zaidi kwenye mechi ya Azam ili kupata ushindi kwani ukiangalia msimu huu tulitumia nguvu kubwa kutokana na kuanza msimu kwa kucheza michezo miwili ugenini,” alisema Nabi aliyekuwa Zanzibar kuipiga chabo Azam ilipokuwa ikicheza na Taifa Jang’ombe visiwani humo.

SOMA NA HII  TIMU ZA SAUZI ZAENDELEA KUIBOMOA YANGA....KOCHA MWINGINE HUYU HAPA NAYE ANASEPA...

Yanga na Azam zinatarajiwa kuvaana wiki ijayo wakati Ligi Kuu itakaporejea kutoka kwenye mapumziko ya wiki mbili, mechi itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku kila timu ikiwa na matokeo tofauti katika michezo miwili ya awali ya ligi hiyo. Yanga ni ya pili, huku Azam ni ya tano.