Mashabiki wa Simba kutoka Tanzania leo wameuteka mtaa wa Divo uliopo jijini hapa nchini Malawi huku wakisisitiza kuwa lazima leo Nyasa Big Bullet alale 3-0.
Simba inatarajia kushuka uwanjani saa 9:00 alasiri kwa saa za Malawi kupepetana na wapinzani wake ambao ni wenyeji kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi itakayopigwa uwanja wa Taifa Bingu.
Leo mashabiki wa Wekundu hao wametua kwa mzuka mwingi na kupokelewa na wenyeji wao na kufanya mtaa huo kuzizima kwa muda kutokana na ‘vibe’ walilokuwa nalo.
Mashabiki hao wamesema wameamua kuifuata timu yao kuhakikisha wanaipa sapoti na kuondoka na ushindi mnono licha ya kuwa ugenini.
Amiri Mrisho mmoja wa mashabiki amesema leo wanaamini Chama lao litaibuka na ushindi wa mabao matatu kutokana na uwezo wa kikosi na mchezaji mmoja mmoja.
Naye Rehema Peter amesema hawana wasiwasi na Mnyama na lazima wapinzani wale nyingi kutokana na nguvu waliyonayo.
“Tumekuja kuwaua, yeyote atafunga hata Banda (Peter) anaweza kumaliza mchezo leo tunachotaka ni ushindi, tumejipanga.”