Home Habari za michezo WAKATI MGUNDA AKITAMBA KUFANYA MAAJABU LEO…COASTA UNION WAENDELEA KUMKAZIA ROHO…WADAI HAWAJUI KITU…

WAKATI MGUNDA AKITAMBA KUFANYA MAAJABU LEO…COASTA UNION WAENDELEA KUMKAZIA ROHO…WADAI HAWAJUI KITU…


Subirini muone. Uzoefu alionao kocha wa muda wa Simba, Juma Mgunda akiwa ngazi tofauti ya timu za taifa umetajwa unaweza kuwa msaada kwenye kikosi hicho kwenye mchezo wa kesho wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi.

Awali Simba ilikuwa kwenye presha ya nani atakaa katika benchi la ufundi la mchezo huo wa CAF baada ya kuachana na Zoran Maki aliyejiunga Al Ittihad ya Misri, huku kocha msaidizi aliyekuwa akikaimu ukocha mkuu, Seleman Matola akikosa vigezo vya kukidhi kulingana na CAF.

Akiongelea uteuzi uliofanywa na Simba, Mkurugenzi wa Ufundi wa zamani nchini, Ammy Ninje alisema; ”Mgunda ni kocha mzuri aliyewahi kuhudumu kwenye nafasi tofauti ngazi ya juu taifa, anaweza kutumia uzoefu huo kuisaidia Simba, ni mtu anayejua vizuri soka la Afrika.”

Msimu uliopita Mgunda aliyewahi kuwa sehemu ya benchi la ufundi la Taifa Stars chini Etienne Ndayiragije, aliiongoza Coastal Union ya Tanga kufika fainali ya ASFC na kupoteza kwa mikwaju ya penalti 4-1 baada ya sare ya 3-3, kikosi kilichokuwa na nyota kama, Abdul Suleiman aliyekuwa mchezaji bora na Victor Akpan walioondoka na kutua Azam na Simba kwa sasa.

Mkongwe Abdallah Kibadeni aliyewahi kuinoa Simba, Kagera Sugar, Majimaji na Stars, alisema makocha wenye Leseni A za CAF ni wachache, jambo ambalo halileti afya kwa maendeleo ya mchezo huo.

“Soka linaajiri sehemu kubwa ya watu, linaiingizia serikali mapato, kutokana na umuhimu huo, kupitia sensa iliyofanya mwaka huu, serikali itabaini mapungufu ya uwepo wa makocha wachache wenye Leseni A,” alisema Kibadeni na kuongeza;

“Simba kumchukua Mgunda sijaona ubaya kwani ni kocha wenye Leseni A na amekuwa na mchango mkubwa kwa soka la Tanzania.”

Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Salum Madadi, aliye na Leseni A pia, alisema ni wakati wa makocha wazawa kuamka na kuanza kujiongeza kwa kusoma ukocha kupitia online kuliko kusubiri zile fursa za TFF, CAF na Fifa pekee.

“Kusoma ni mtu binafsi mwenyewe huwezi kumlazimisha, ila wanatakiwa kuonyesha ushindani dhidi ya makocha wageni wajao nchini, niliwahi kufundisha timu moja pamoja na kocha mgeni, nilionyesha uwezo uliowashawishi mabosi kutaka nibakie na mgeni akaondolewa na nilipewa heshima ya juu,” alisema Madadi aliywahi kuinoa Simba na kuongeza;

SOMA NA HII  LANGONI KWA RIVERS KUNAWAKA MOTO...YANGA KUWENI MAKINI MTAUMIA

“Sina maana kwamba waliopo ni wabaya, wanatakiwa kupewa heshima kubwa, pia nao wasome.”

Beki wa zamani wa Simba, Kasongo Athuman alisema kwa sasa timu hiyo inahitaji utulivu akimtaka kocha msaidizi Seleman Matola kuvaa ujasiri wa kukabiliana na hasira za mashabiki, lakini jambo la msingi ampe ushirikiano wa kutosha Mgunda.

“Kwa kile kinachoendelea kiwafunze mabosi wa Simba, kwani kuondoka kwa kocha Zoran haikuwa sapraizi, ila kwa sasa sio wakati wa kunyosheana vidole, wachezaji wapambane watoboe warudishe morali ya mashabiki kwenda uwanjani,” alisema Kasongo.

UONGOZI COASTAL

Katibu wa Coastal, Omari Ayoub alisema hawakufanya mawasiliano yoyote na Mgunda zaidi ya kuona taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa anakwenda kuwa kocha wa muda wa Simba.

“Hatujafanya mawasiliano yoyote na Mgunda, tumeona taarifa kama ilivyonekana kwenye mtandao, sina chochote ninachokujua zaidi ya kwamba kocha huyo alimaliza mkataba nasi.

“Mgunda alimaliza mkataba wake wa kimaandishi na klabu yetu Septemba Mosi, lakini tulikuwa tumezungumza naye ili aendelea kuifundisha Coastal, hivyo alishakubali hivyo tulikuwa katika kutimiza taratibu za kisheria ili kumalizana naye kumpa mkataba mpya ili aendelee kukaa kwenye benchi la ufundi , “alisema Ayoub na kuongeza.

“Tulitegemea wiki hii tungesaini nae mkataba mpya, kabla ya kuona hizo taarifa ya kutua Simba. Hatuhusiki chochote kjiunga na Simba na timu yetu itakuwa chini ya Kocha msaidizi Joseph Lazaro,” alisema Ayoub na kufafanua, Mgunda hana kosa lolote kwa alichokifanya kwa sababu ni hiari yake, kwani hayo ni mambo ya kazi na inawezekana ameangalia penye manufaa zaidi.

Hata hivyo habari za kuaminika kutoka kwa baadhi ya viongozi wa timu hiyo ya Tanga ni kwamba dili la Mgunda kwenda Simba klabu hiyo ilihusika baada ya mabosi wa Simba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuzungumza naye baada ya Msimbazi kurudi shirikisho kuomba msaada wa kupata kocha na kulituma jina CAF, huku wakiendelea kumtafuta kocha mkuu mpya.