Home Habari za michezo YANGA SC WAITUPIA LAWAMA TFF ISHU YA PELE….WALIA KUFANYIWA HUJUMA…

YANGA SC WAITUPIA LAWAMA TFF ISHU YA PELE….WALIA KUFANYIWA HUJUMA…

Pele kutua Yanga SC

MARA kadhaa kumekuwa na mivutano baina ya TFF na klabu ya Yanga SC na kusababisha mambo mengi kwenda mrama.

Hili siyo jambo la kujadili sana kwa sababu kila mmoja ni shuhuda namna taasisi hizi mbili zinavyopimana ubavu huku Yanga SC ikisema TFF ni Simba.

Lakini mgogoro baina ya taasisi hizi ni wa muda mrefu kidogo na asili yake ni gwiji wa soka, Edson Arantes dos Nascimento, ‘Pele’ ambaye amefariki Desemba 29, 2022.

Mwaka 1973, Yanga SC ilifanya jitihada za kumleta Pele na klabu yake ya Santos hapa nchini kwa ajili ya mechi ya kirafiki.

Alitakiwa aje Desemba mwaka huo, lakini ikashindikana. Februari 1974 Yanga SC ilienda kuweka kambi Brazil kujiandaa na ligi ya taifa, sasa Ligi Kuu.

Wakiwa huko ikajaribu tena kufanya ushawishi kwa Pele na Santos kuja Tanzania na kupewa matumaini. Yanga ikarejea nchini Februari 28, 1974 na matarajio yalikuwa Pele na Santos waje Aprili.

Lakini Aprili ilipofika Pele na Santos hawakuja. Katibu Mwenezi wa Yanga SC (sasa ndiyo Afisa Habari), Mshindo Mkeyenge, akatangaza kuahirishwa kwa safari hiyo.

Mkeyenge akasema mratibu wa ziara hiyo, Mbrazili, Elias Zaccur alikuwa anaenda Misri kwenye Afcon akiambatana na Rais wa Shirikisho la Soka la Brazil, Joe Havellange na huko wangeitaarifu Yanga SC mipango zaidi ya safari hiyo.

Lakini AFCON ikaisha na hakukuwa na taarifa mpya, matumaini yalizidi kufifia na Yanga ikakaribia kukata tamaa.

Ndipo Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wakati FAT, ambayo sasa ni TFF, Said El Maamry (RIP) alipoingilia kati mchakato huo akisema Yanga SC hiawezi kufanikiwa bila mkono wa FAT.

Kuanzia hapo, yeye ndiye akawa anasimamia mchakato kwa niaba ya Yanga SC.

El Maamry alikuwa amerejea nchini akitokea Cairo, Misri alikohudhuria mkutano wa shirikisho la vyama vya soka Afrika (AFC sasa CAF) na akiwa huko alikutana na Joao Havelange aliyemhakikishia Santos na Pele watakuja Tanzania.

El Maamry alisema Havelange amemwahidi kutumia uwezo wake wote kuhakikisha Santos inakuja nchini.

Mwenyekiti huyo alisema mbali na Santos kuwa kwenye Ligi ya Brazil, Havelange aliahidi watairuhusu timu hiyo ije Dar kwa wiki mbili.

El Maamry alisema Santos itakapokuwa nchini mbali na kucheza na wenyeji wao Yanga SC, pia FAT imepewa mchezo mmoja ambao itaamua timu hiyo itacheza na timu gani.

Alipoulizwa Santos itacheza na timu gani katika mchezo huo, El Maamry alisema shauri hilo litaamuliwa na Kamati ya Utendaji ya FAT.

Mungu si Athuman, El Maamry alipata mwaliko wa kwenda Brazil, Aprili 1974 kutoka chama cha soka cha nchi hiyo.

Kiongozi huyo wa soka alisema akiwa nchini humo atazungumzia ziara ya Santos kuja Tanzania.

Hii ilikiuwa ziara ya kwanza ya kiongozi wa soka nchini kupata mwaliko kutoka chama cha soka cha Brazil.

Mwezi huohuo Aprili, zikatoka taarifa mpya kwamba kuna timu kadhaa za soka za Brazil zimepangwa kutua Tanzania na kucheza michezo kadhaa ya kirafiki, kati ya timu hizo Santos ikiwa na Pele wake.

Mpango huo umeandaliwa na FAT na mratibu wa timu za Brazil barani Afrika, Elius Zaccur.

Katibu Mkuu wa FAT, Martin Mgude alisema mipango inakwenda vizuri na timu ya kwanza kutua itakuwa ni Galicia ambayo ingeanza michezo yake Aprili 6.

Pia, timu hiyo ilipangiwa kwenda Tanga kucheza mchezo mmoja wa kirafiki.

Hata hivyo, alisema FAT haikuwa imepanga timu hiyo itacheza na timu gani.

Mgude alisema timu ya pili kutua nchini kutoka Brazil ingekuwa ni Colorado FC ambayo mchezo wake wa kwanza ungekuwa Mwanza, Aprili 24.

Pia, timu hiyo ingerudi Dar es Salaam na kucheza michezo miwili Aprili 27 na 28.

Katibu huyo alisema timu ya mwisho kutua nchini ni Santos ambayo ingetua Mei na kucheza michezo miwili.

Timu hiyo ingeambatana na staa wake Pele ingecheza michezo miwili Mei 8 na 10.

Baadaye ziara hiyo ikarushwa tena hadi Septemba mwaka huo.

Baada ya danadana kuwa nyingi, El Maamry akapasua jipu kwa kusema hakuna tena uwezekano wa Pele na Santos kutua nchini.

El Maamry alisema uwezekano wa Pele kutua nchini umetoweka baada ya mchezaji huyo kutangaza kustaafu kucheza soka mwezi Oktoba mwaka huo.

El Maamry alisema chama chake kwa kushirikiana na Yanga walifanya mipango ya kumleta Pele na klabu yake ya Santos Tanzania Septemba 1974 kucheza michezo kadhaa ya kirafiki.

Kiongozi huyo alisema FAT ilipeleka barua kwa viongozi wa michezo wa Brazil, lakini hawakupewa jibu lolote.

Hapo ndipo mgogoro wa Yanga na FAT ambao sasa umerithiwa na TFF, ulipoanza. Klabu ya Yanga ikaibuka na kusema imepata hasara kubwa kutokana na ziara ya Pele na Santos kushindwa kufanyika.

Mwenyekiti wa Yanga, Mangara Tabu Mangara (RIP) alisema hasara imetokana na gharama ya kuwasafirisha wajumbe wawili kwenda Brazil kukutana na Pele mapema 1974. Hasara nyingine ni matayarisho madogo madogo ambayo mwenyekiti huyo hakutaka kuyataja. Hata hivyo, inaeleweka kwamba Yanga ilijiandaa kwa mapokezi makubwa ikiwemo kutengeneza khanga maalumu zilizoandikwa ‘Pele na Santos wageni wa Yanga SC’.

Mangara alimlaumu moja kwa moja El Maamry kwa kuihujumu ziara hiyo. Akasema kwa muda wa miezi mitatu au minne alikuwa akishughulikia ziara hiyo kwa niaba ya Yanga SC, lakini kumbe alikuwa anawapotezea muda.

Mangara alisema alishtushwa sana na tamko la kiongozi huyo wa FAT aliposema Pele na Santos hawawezi kuja Tanzania kama ilivyopangwa.

Mangara alisema kama sio ziara hiyo kushughulikiwa na El Maamry klabu yake kwa njia yoyote ile ingeweza kumleta Pele na klabu yake ya Santos.

El Maamry alitakiwa awe anatoa taarifa ya maendeleo ya ziara hiyo kwa viongozi wa Yanga SC.

Mangara alilalamika kwa muda wote huyo hawakupata taarifa yoyote kutoka kwa El Maamry hadi pale walipokuja kusikia Pele na Santos hawawezi kuja Tanzania.

Kiongozi huyo aliwaomba radhi wananchi wote ambao kwa muda mrefu walikuwa na matarajio ya kumuona Pele akiitumikia timu yake ya Santos.

Alisema pamoja na timu yake kushindwa kumleta Pele lakini jitihada zinafanywa kuwaridhisha wananchi kwa njia yoyote ile.

El Maamry alikanusha kusababisha kufa kwa ziara ya Pele na klabu yake ya Santos. Alisema lawama zilizotolewa na Yanga hazina msingi wowote bali kujenga uhasama baina ya klabu hiyo na FAT hasa kama wanachama na wapenzi wa klabu hiyo wataziamini.

El Maamry alisema katika ziara yake ya Brazil alifika hadi Santos na kuzungumza na viongozi wa Santos na Pele juu ya ziara yao ya Tanzania kama alivyotumwa na Yanga SC.

Kiongozi huyo alisema walikubaliana Pele na Santos wangekuja nchini Septemba 1974 baada ya ziara ya klabu hiyo iliyofanyika Hispania.

Hata hivyo, El Maamry alisema ziara ya klabu hiyo na Pele kulitegemea ruhusa ya viongozi wa Chama cha Soka cha Brazil.

Kiongozi huyo wa FAT alisema katika mkutano wa Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Soka (FIFA) uliofanyika Munich, Ujerumani (Magharibi), viongozi wa soka wa Brazil waliuahidi ujumbe wa Tanzania, Pele na Santos wangetua nchini baada ya fainali za Kombe la Dunia.

El Maamry alisema licha ya ahadi hiyo, FAT ilipiga simu mara kwa mara Chama cha Soka cha Brazil, lakini hakuna jibu la maana tulilopewa.

“Sasa iwapo Pele ameacha kucheza soka mimi nahusikaje na kutokuja kwake,” alihoji.

Viongozi wa Yanga SC wakainunia FAT…chuki ikarithiwa na TFF hadi sasa taasisi hizi zinaishi kwa visasi. Lakini chanzo ni Pele na Santos 1974.

Makala hii imenakiliwa  kutoka gazeti la Mwanaspoti kwenye kolamu ya Mzee wa Upupu.

SOMA NA HII  AZIZ KI ATWISHWA ZIGO LA MAGOLI YA GUEDE YANGA....ISHU NZIMA IKO HIVI...