Kinara wa mabao Ligi Kuu Bara, Fiston Mayele amefichua mastaa wa timu hiyo wamekubaliana kugawana fedha zilizoahidiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kununua kila bao katika mechi za CAF kwa Sh5 milioni.
Yanga inashuka uwanjani leo hii kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, siku chache baada ya Rais Samia kusema atanunua kila bao kwa Sh5 milioni na mastaa wa Yanga wamejiongeza mapema.
Yanga itashuka uwanjani leo Jumapili kuikabili TP Mazembe ya DR Congo kwenye mchezo wa Kundi D wa Kombe la Shirikisho.
Akizungumza Mayele alisema wachezaji wa Yanga wamekaa kikao na kukubaliana kila mmoja atekeleze majukumu yake kuhakikisha timu inatoka uwanjani na ushindi kwa kufunga mabao ya kutosha na kitakachopatikana kitagawanywa sawa kwa kila mmoja.
Mayele alisema wamesikia ahadi iliyotolewa na mkuu wa nchi na kama wachezaji wanazitolea macho fedha hizo, ila wamekubaliana kwa pamoja kila mmoja afanye majukumu yake uwanjani kiasi kitakachopatikana watagawana.
“Kila mchezaji anaitolea macho fedha hiyo na kila mmoja anatamani kuipata na tumekubaliana kwa pamoja kila mtu kutimiza majukumu kwa usahihi ili kuhakikisha timu inashinda mbele ya TP Mazembe kwa kutambua tukizungua tutaikosa fedha hiyo,” alisema Mayele na kuongeza;
“Tumekubaliana kama timu, atakayepata nafasi ya kufunga, afunge bila kujali kwani pesa itakayopatikana tutagawana kwani nia yao ni moja kupata matokeo mazuri yatakayotuvusha tulipo sasa.”
Mayele alisema wamefanya hivyo ili kuhakikisha wanatengenezeana nafasi zitakazowafanya wafunge na sio kila mchezaji kuingia ndani ya 18 kwenda kufunga mwenyewe kwani wanaweza kujitibulia na kusababisha timu ikose ushindi nyumbani.
Akizungumzia mchezo huo kwa ujumla alisema wanatarajia mchezo mzuri na wa ushindani huku akiwaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kuwapa ushirikiano wao kama wachezaji wamejiandaa kufanya kilicho bora.
Nahodha msaidizi wa Yanga, Dickson Job alisema wanatambua zawadi kubwa wanayoitaka wanayanga ni matokeo mazuri kwenye mchezo wa Jumapili wao kama wachezaji pia wamejiandaa kushindana na kutumia kila nafasi watakazotengeneza.
“Ni mchezo ambao tunauchukulia kama fainali hii ni kutokana na matokeo mabaya tuliyoyapata ugenini tunahitaji matokeo mazuri ili kurudi kwenye mstari na kuendelea na ushindani hatimaye kutinga hatua inayofuata,” alisema Job na kuongeza;
“Tunawaheshimu wapinzani wetu ni wazuri na watashuka dimbani wakiwa na marali nzuri kutokana na matokeo mazuri waliyoyapata hilo halitutoi mchezoni sisi pia tunahitaji matokeo kwenye uwanja wetu wa nyumbani ili kujiwekea mazingira mazuri ya ushindani.” alisema.
Job alisema wanakutana na timu bora iliyotwaa mataji zaidi ya 10 ya michuano ya CAF, hivyo wataingia uwanjani wakiiheshimu lakini kupambana ili kupata pointi tatu nyumbani baada ya awali kupoteza mechi ya ugenini kwa kufungwa na US Monastir kwa mabao 2-0, nchini Tunisia.