Home Habari za michezo SIMBA WAPATA NGEKEWA NYINGINE CAF….WAPEWA MWAMUZI MWENYE BAHATI YA USHINDI….

SIMBA WAPATA NGEKEWA NYINGINE CAF….WAPEWA MWAMUZI MWENYE BAHATI YA USHINDI….

Mwamuzi wa Simba leo

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika limefanya uamuzi ambao unaonekana kama neema kwa wawakilishi wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba katika mchezo dhidi ya Raja Casablanca, leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku.

Uamuzi huo ni wa kumteua mwamuzi mwenye nyota ya bahati kwa timu zinazocheza nyumbani pindi anaposhika filimbi katika mashindano ya klabu Afrika, Blaise Ngwa (41) kutoka Cameroon.

Kumbukumbu ya mechi za nyuma za mashindano ya klabu Afrika ambazo zilichezeshwa na refa huyo inaonyesha mara nyingi timu mwenyeji imekuwa ikifanya vizuri kwa kupata ushindi huku ikiwa ngumu kwa wageni.

Katika mechi 11 za mashindano ya klabu Afrika ambazo Ngwa amechezesha, timu zilizokuwa nyumbani zilipata ushindi mara nane, sare mbili na mara moja timu ngeni ilipata ushindi.

Hata hivyo, Simba inapaswa kuwa makini upande wa nidhamu kwani amekuwa na tabia ya kupenda kumwaga kadi ambapo katika mechi hizo 11 alizochezesha, alitoa kadi 49 za njano ikiwa ni wastani wa kadi 4.5 kwa mechi.

Mwamuzi huyo atasaidiwa na wenzake watatu kutoka Cameroon ambao ni Elvis Nguegoue, Carine Artezambong na Jeannot Bito.

Wakati Simba wakipewa mwamuzi huyo, watani wao Yanga wamekutanishwa na mwenye nuksi na timu za nyumbani, AbdelAziz Bouh kutoka Mauritania kuchezesha mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe, kesho Jumapili kuanzia saa 1:00 usiku uwanja huohuo.

Kumbukumbu zinaonyesha Bouh (30) katika mechi sita za mashindano ya klabu Afrika alizochezesha, timu zilizokuwa nyumbani zilipata ushindi mara mbili, sare mbili na kupoteza mbili.

Katika mechi hizo ambazo mwamuzi huyo kutoka Mauritania alichezesha, alitoa kadi 20 zote zikiwa za njano ambazo ni wastani wa kadi tatu kwa mchezo. Bouh atasaidiwa na wenzake wa Mauritania, Hamadine Diba, Brahim H’Made na Moussa Diou.

Beki wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Nadir Haroub ‘Canavaro’ alisema wawakilishi wote wa Tanzania wasiingie na mawazo ya marefa vichwani kwenye mechi zao mwishoni mwa wiki hii.

“Wajiandae kwenda ndani ya uwanja kupambana na wasiwafikirie marefa. Wakitimiza wajibu wao, watafanya vizuri pasipo kujali marefa wanapendelea upande wa pili au wanachezesha kwa kufuata sheria za soka.

“Naamini Simba na Yanga wote wana timu nzuri na watatumia vyema uwanja wa nyumbani kupata ushindi,” alisema Cannavaro.

Katika hatua nyingine, mabosi wa Simba wamewapokea maofisa kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF) waliokuja nchini kwa ajili ya ukaguzi wa maandalizi ya Super League itakayoshirikisha klabu nane na itakayoanza Agosti.

Simba ni kati ya vigogo nane vilivyoripotiwa vitashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo, sambamba na Al Ahly, Esperance, Wydad Casablanca, TP Mazembe, Mamelodi Sundowns, Horoya na Petro de Luanda.

SOMA NA HII  MANARA :- TFF IMFUKUZE KAZI AMROUCHE....ANAIHUJUMU YANGA MCHANA KWEUPEEE...