Home Habari za michezo SIMBA SC:- TUMELINASA FAILI LA HOROYA…TUNALIFANYIA KAZI…TUNAWAANGALIA KWA JICHO LA TATU

SIMBA SC:- TUMELINASA FAILI LA HOROYA…TUNALIFANYIA KAZI…TUNAWAANGALIA KWA JICHO LA TATU

Habari za Simba SC

BENCHI la Ufundi la Simba, linatambua kwa sasa timu hiyo ina dakika 90 za kibabe ili kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Horoya Jumamosi na katika kuweka mambo sawa wamelinasa faili la Waguinea na kulifanya kazi chapu.

Mgunda alisema ugumu na umuhimu wa mchezo huo umeanza kwa benchi la ufundi, wachezaji hadi viongozi na katika kuondoa presha kwa mastaa wao wamewatengenezea mazingira kwa kuwapa mbinu mpya za kupata pointi tatu nyumbani.

Mgunda alisema Horoya ilikusanya pointi tatu ikiwa kwao; “Horoya ni wazuri vile vile ukianzia mchezaji mmoja mmoja na namna wachezaji walivyo kwenye morali nzuri ya kupambana na kuna vitu vipya tumewapa ili kuidhibiti,” alisema Mgunda na kuongeza;

“Lengo letu ni moja kuanzia benchi la ufundi, wachezaji na viongozi ambao wamekuwa karibu na timu kuhakikisha inakuwa kwenye hali ya utulivu hili tunaamini litasaidia kufikia malengo yetu ya kukusanya pointi tatu na kutinga robo fainali.”

Kwa upande wa Kocha Mkuu, Roberto OliveiraRobertinho’ alisema; “tuko kwenye nafasi nzuri ya kuendelea kuandika rekodi nyingine katika ardhi yetu ya nyumbani, tunatambua ugumu uliopo na umuhimu wa mchezo huu kuanzia kwetu benchi la ufundi, viongozi na mashabiki wetu ambao wamekuwa nasi bega kwa bega hivyo hatupo tayari kuwaangusha,” alisema.

Kocha huyo aliongeza wachezaji wanahitaji sana mchezo huo kwa ajili ya kuweka rekodi nyingine lakini pia kulipa kisasi baada ya mechi ya kwanza kupoteza bao 1-0 Februari 11 nchini Guinea.

“Mbinu muhimu ambayo nimewapa wachezaji wangu na tutakayoitumia kwa ajili ya kupata matokeo mazuri na kutimiza malengo yetu ni kuhakikisha tunapambana mwanzo wa mchezo hadi mwisho tukiamini hii itakuwa njia salama kwetu ya kutompa mpinzani nafasi ya kutushambulia kirahisi,”

“Kwa muda mchache pia tumetumia kwa kuwafuatilia katika michezo yao ya hivi karibuni na tumegundua wameimarika kwa kiasi kikubwa tofauti na awali tulivyokutana nao hivyo ni mechi ya maamuzi kwa sababu kila timu ina nafasi ingawa kwetu tunaiangalia kwa jicho la tatu na la kipekee sana.”

SOMA NA HII  BAADA YA KUMUACHA CHAMA..SIMBA YAJIBU MAPIGO KWA MCHEZAJI WA YANGA.