Home Habari za michezo STAA WA YANGA ANAYEUZA MISHIKAKI….AFUNGUKA A-Z JINSI MO DEWJI ALIVYOMTIMUA BILA HURUMA…

STAA WA YANGA ANAYEUZA MISHIKAKI….AFUNGUKA A-Z JINSI MO DEWJI ALIVYOMTIMUA BILA HURUMA…

KIPANYA MALAPA | SIO MISHIKAKI TU HADI UKONDA | MIKASA YAKE NDANI YA MIAKA 17

“Nilipostaafu soka nilifanya kazi tofauti, nimekuwa kondakta wa daladala, kisha nikafanya mambo ya mtaani na sasa nauza mishikaki na kacholi,” ndivyo anaanza kusimulia Kipanya Malapa, miongoni mwa nyota walioipandisha Singida United kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mshambuliaji huyo nyota anasema pamoja na kwamba soka halikumlipa kama ambavyo biashara ya mishikaki na kacholi inavyomlipa kwa sasa, lakini limempata umaarufu.

“Watu wakiniona nauza mishikaki, baadhi yao wanafikiri maisha yamenipiga, la hasha, pesa ninayoipata hapa kwa siku ni zaidi ya mara mbili ya mshahara niliokuwa nikilipwa Singida United,” anasema.

Malapa aliyewahi pia kuitumikia Yanga 2003 anasema, mshahara mkubwa aliolipwa kwenye maisha yake ya soka ni Sh 50,000, akiwa Yanga ambayo sasa anaingiza pesa hiyo kwa siku kwenye kijiwe chake cha mishikaki kilichopo Buguruni Malapa, eneo lililotokana na jina la baba yake, ambaye ana nyumba tatu hapo.

“Mzee na mama walituachia urithi wa nyumba, nne ziko Buguruni, tatu ziko Tabata Chang’ombe, tuko sita kwenye familia yetu, tukigawana kodi sikosi laki tano kwa mwezi, lakini kwanini nikae na kutegemea kodi? Hivyo najishughulisha,” anasema.

Baada ya soka ilikuwa hivi

Kipanya alistaafu 2006, anasema tangu wakati huo amekuwa akifanya kazi mbalimbali, ikiwamo za mihangaiko ambayo haikumpa amani ya moyo.

“Niliifanya kutokana na ushawishi wa marafiki, sikuipenda kabisa, niliwaza kwanini nifanye kazi ambayo ukimuona mbele yako mtu kavaa suti una hofu.

“Niliifanya muda mfupi sana na kuiacha, ilikuwa ni kazi ya wasiwasi, niliichoka na nikaiacha, japo sikuwahi kuingia kwenye matatizo, lakini niliziona kwa wenzangu.

“Nilihitaji kufanya kazi isiyo na presha, nikapata wazo la kuuza mishikaki na kacholi, kilipo kijiwe changu ni kwenye eneo la nyumba yetu nyingine, mke wangu mrembo, Zawadi amekuwa na mchango mkubwa kwenye kazi yangu,” anasema.

Akisimulia namna alivyokutana na Zawadi, Kipanya anasema ilikuwa ni Buguruni yeye akiwa na biashara ya duka la vifaa vya shule na ofisini (Stationary).

“Zawadi alinipenda, akaogopa kuniambia, alikuwa karibu na mimi akisubiri nimuanze, Mungu aliniongoza nikamwambia, hakunisumbua kwa kuwa tulipendana,” anasema Kipanya.

Anasema wakati wanaanza uhusiano, tayari alishastaafu soka, ingawa mkewe alikuwa akimuita staa, jina analomuita hadi sasa.

Akiwa maeneo ya nyumbani kwake, Buguruni Rozana, Kipanya ni maarufu kwa jina la straika, ni mtu wa watu huku akitaniwa mara kadhaa na majirani zake ambao ni wanazi wa Simba, kutokana na mchezaji huyo kuwahi kucheza Yanga na ni timu ambayo anakiri kuwa na mapenzi nayo, lakini Singida ndipo ilipo roho yake.

Malapa alisajiliwa Yanga 2003 baada ya kuifunga timu hiyo na watani zao, Simba kwenye Ligi Kuu kwa nyakati tofauti.

“Mzee Mzimba ndiye alinifuata, kwa kuwa ni timu niliyoipenda hata sikujiuliza, japo nilikuwa na hofu ya namba kwa kuwa niliokuta ina watu, akina Sakilojo Chambua, Said Maulid, Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, Kibavu, Waziri Mahadhi ‘Mandieta’ na Edibily Lunyamila, kwangu ilikuwa nikicheza sawa nisipocheza sawa, kwani wale walikuwa na uwezo kuliko mimi.

“Nilicheza kwa muda mfupi kama miezi tisa, nikaomba nirudi Singida ambako nilikuwa nyota ili nipate nafasi ya kucheza, waliniruhusu ingawa baadaye nilijiunga na timu nyingine hadi 2006 nilipostaafu nikiwa na timu ya Mundu ya Zanzibar,” anasema.

4-0 za Simba

Katika maisha yake ya soka Yanga, Malapa anasema moja ya vitu vilimuondoa kwenye timu hiyo ni kipigo cha mabao 4-0 kwenye mechi ya watani dhidi ya Simba katika Kombe la Tusker.

“Niliiona ile mechi ndiyo ya kumaliza shida zangu zote, tuliahidiwa bonasi nono tukiifunga Simba, akili yetu ikawa haiwazi tena mpira tunawaza tu bonasi, muda mwingi tulizungumzia pesa tulizoahidiwa, kibao kikageuka, siku hiyo nilisahau hata njia ya nyumbani, badala ya kwenda Buguruni nikaenda Mbagara,” anasema.

Kisa Yanga, Mo Dewji amtimua

Kipanya anakumbuka namna bosi wake, Mohammed Dewji (Mo) alivyomtimua baada ya kusajiliwa Yanga.

“Kassim Dewji ndiye alinirejesha Singida nilipotoka Yanga, Mo Dewji hakutaka hata kunisikia,” anasema Kipanya ambaye anamtaja mzee Zagalo kuwa mtu aliyemtoa kisoka.

“Kabla ya kusajiliwa Singida nilikuwa nacheza timu za mchangani za hapa Dar es Salaam, kule ni vita, mashabiki watemi, wachezaji wababe.

“Usipokaa vizuri mashabiki wa timu yako wanaweza kukupiga, mimi nakumbuka niliwahi kung’olewa meno uwanjani na beki, aliruka akanipiga kiwiko nikicheza Maji Kipawa ya Mwananyama dhidi ya Brake Pool ya Vingunguti.

“Mashabiki waliniambia hakuna kutoka, nilisukutua na kuendelea na mechi, mchangani kulinikomaza hadi nakwenda kucheza Mtwara alikonipeleka mzee Zagalo, kipindi hicho Bandari Mtwara ilikuwa ni moto, kwenye uwanja wao hutoki.

“Niliifunga Bandari Mtwara, tukarudi Dar ili kucheza na Pan, wakati huo sikuwa nimesajiliwa japo kwenye mechi na Bandari nilicheza kinyemela, Pan wakaniwekea ngumu, sikucheza, Kassim Dewji akapambana mechi ziluzofuata nikacheza hadi tunaipandisha daraja Singida United.

Kipanya anayejiita ‘King of Singida United’ asiyeamini ushirikina kwenye soka zaidi ya mazoezi anasimulia maisha ndani ya klabu hiyo.

“Nakumbuka kuna siku tulikuwa kambini, tukaomba tuletewe matunda wachezaji, viongozi wakakubali, siku iliyofuata tukaletewa mapera.

“Kingine ni maisha ya timu, tulikuwa tunalazimika kusafiri usiku ili tusiingie gharama ya vyumba tukienda kucheza nje ya mkoa, tulikuwa tukilipwa posho 2,500 hivyo pesa ya vyumba tunagawana kuongezea kwenye posho.

“Hatukuwa na dereva, nahodha wa timu Issa Kasanga ndiye alikuwa dereva wetu tukienda mkoani na tulikuwa tunamwambia asimame tupakie abiria ili kuongezea ongezea posho zetu, kipindi hicho nalipwa mshahara Sh20,000.

“Chakula kambini ilikuwa ni cha mzunguko tulikuwa na mama mmoja anatupikia, tofauti na Yanga ilikuwa kishua, tuliishi kishua hakukuwa na njaa za kubania posho.

Anasema Singida United iliposhuka daraja alisajiliwa Reli Morogoro, ambako alilipwa fedha nusu, baadaye walitakiwa kwenda kucheza mechi Kigoma, timu ikakosa nauli.

“Wakati huo nipo Morogoro mji mpya, sina fedha nikaambiwa timu ilishavunjwa, nilikuwa na mipira sita ya timu, nikaiuza 60,000 ili nipate nauli ya kurudi Dar es Salaam, ila baadaye uongozi ulituita tuliokuwa tunaida timu, pesa yangu ilikuwa laki nne, wakakumbushia mipira yao wakanikata 150,000.

Kipanya aliyesajiliwa Yanga kwa Sh600, 000 na Singida Sh45,000 anasema maisha ya soka yana presha.

“Unaweza kuwa unapata hela lakini unakonda kila siku, kuna presha kubwa kwenye soka, ya mashabiki, viongozi, watu wa mtaani na wewe mwenyewe kuwa na presha ya kucheza, usikosee, ukizomewa inakuharibu kisaikolojia,” anasema.

Maisha ya ukondakta

Kipanya anasema baada ya kutoka kucheza soka la ushindani, alipata kibarua kwenye daladala yenye njia ya Gongolamboto-Uhuru (sasa Gerezani).

“Bosi wangu alikuwa na timu, akaniambia nikacheze huko, hivyo asubuhi nikawa naingia kibaruani, jioni namuachia deiwaka nakwenda kufanya mazoezi.

“Kwenye mechi, nilikuwa nakula posho mara mbili, daladala lile ndilo litapeleka wachezaji nikiwa kondakta, tukifika nashuka naingia uwanjani, baada ya mechi narudi kwenye ukonda,” anasema.

Kipanya anasema kwenye kazi hiyo alikuwa anaamsha gari saa 10 alfajiri anarudi nyumbani saa 6 usiku.

“Lazima kila siku mpate hesabu ya tajiri na hela ya mafuta, inayobaki ndiyo ujira wetu, biashara ikiwa nzuri konda anaondoka na Sh 35,000, dereva 50,000 kwa siku.

“Hamna hamna, konda ataondoka na Sh 10,000 na dereva 15,000, ila asikwambie mtu makonda wengi wanaiba, haondoki na ile tu wanayogawana na dereva.

“Mimi nilikuwa na uhakika wa kuiba 15000 hadi 35000 kutegemea na biashara, usiku nikijumlisha na tulizogawana nakuwa na pesa nzuri.

“Vichimbo vya makonda wengi ni vingi, anaweza kushonea kwenye jeans au kumpigia mtu akija anampa wanakutana usiku, hivyo hata akichukua posho 10,000 kwa konda ni sawa tu, ingawa ni kazi inayotaka ujitoe hasa,” anaongeza.

Kijiwe cha mishikaki

Akiwa na mkewe mrembo Zawadi, Kipanya anasema ana mchango mkubwa kwenye biashara yake inayomuingizia hadi Sh50,000 kwa siku.

“Mke wangu yupo sokoni, lakini ndiye mpishi wa kacholi ninazouza pia.

“Alfajiri saa 9 nakata nyama hadi saa 11 asubuhi, nikishazitunga hadi saa 12, mimi nalala yeye anakwenda sokoni, akirudi saa 3 mimi naamka kuandaa vitu vya jioni kijiweni, yeye analala, saa 10 ndipo nakuwa kwenye kijiwe changu hadi saa 3 usiku,” anasema.

Kipanya, ambaye mmoja wa watoto wake, Gadaf anacheza timu ya vijana ya Azam FC, anasema umaarufu wake kwenye soka kunamlazimu kuweka mishikaki ya bure ya marafiki.

“Nikitengeneza ya Sh20,000 basi nitaongeza ya Sh4000 ya marafiki, atakuja tu mtu utamsikia ‘ahh! streka au ohh mwanangu, amechukua wa bure’.

“Nawapa ila na mimi nafahamu ni wapi nazirejesha, anaweza kuja shabiki akatoa elfu 10, akala mishikaki miwili 400, chenji ananiachia najazilizia kule, kijiwe kinanilipa, naingiza pesa nzuri ya kuhudumia familia.

“Siku ikitokea Yanga amefungwa, kuna wengine wanakuja kununua mishikaki kwa kukebehi tu wakijua mimi Yanga,” anasema mfungaji huyo nyota wa zamani ambaye alianza na mtaji wa Sh20,000 miaka mitano iliyopita.

SOMA NA HII  WAWA AMSALITI BOCCO KISA MAYELE...MASTAA WASHANGAZWA ISHU NZIMA IKO HIVI