Home Habari za michezo MASTAA SIMBA WASHIKWA NA NJAA KALI KAMBINI…WAENDELEA KUTEMBEZA KICHAPO

MASTAA SIMBA WASHIKWA NA NJAA KALI KAMBINI…WAENDELEA KUTEMBEZA KICHAPO

MASTAA SIMBA WASHIKWA NA NJAA KALI...WAENDELEA KUTEMBEZA KICHAPO

KIKOSI cha Simba kimerejea kambini kujiandaa na mechi zijazo baada ya wachezaji wasioitwa timu za taifa kumaliza mapumziko ya siku tano, huku Kocha Mkuu Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akisema sasa ni mwendo wa dozi ili mambo yawe sawa

Simba inakabiliwa na mechi nne za kibabe ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco, robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Ihefu na Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu na Yanga kati ya Aprili 1-16.

Robertinho aliwapumzisha wachezaji ambao hawajaitwa timu za taifa na jana walirudi kuanza kujifua ili kuwaweka fiti kabla ya kuungana na wenzao saba walio na majukumu ya kitaifa kwa nchi zao wakiwamo Aishi Manula, Beno Kakolanya na Mzamiru Yasin waliopo Taifa Stars, Clatous Chama (Zambia), Peter Banda (Malawi), Pape Sakho (Senegal) na Henock Inonga (DR Congo).

Simba iliyotoka kuinyoosha mabao 7-0 Horoya ya Guinea na kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa itaifuata Raja kukamilisha ratiba Aprili 1 kabla ya kurudi kuivaa Ihefu kwenye ASFC Aprili 7 na siku tatu kucheza tena na Ihefu katika Ligi Kuu, ilhali Aprili 16 itakuwa na kibarua na Yanga.

Kwa kutambua mechi zilivyo karibu na ugumu wake Robertinho alisema anataka wachezaji waliosalia nchini kuungana kambini kwa vile hataki kupunguza kasi waliyonayo.

Mbrazili huyo alisema jukumu lake ni kuimarisha viwango ili kupata kilicho bora ndio maana wamewaita haraka kambini kuwapa dozi na hata watakapokutana na wenzao kusiwe na tofauti kubwa kikosini.

“Kipindi hiki tunaweza kufanya kazi karibu zaidi na kujaribu kuimarisha viwango vya mchezaji mmojammoja kwenye timu. Ni muhimu kufanya kazi na kuwaweka sawa ili wenzao wakirejea wawe tayari kwa ushindani, “ alisema kocha huyo aliyewahi kuinoa Rayon Sports ya Rwanda na Vipers ya Uganda.

“Nataka kila mchezaji kuwa sawa na tayari muda wowote kutumika. Hatua tunayokwenda inahitaji kuwa na kikosi kipana ambacho kitamudu ushindani kwenye mashindano yote kikiwa na nguvu ileile ya ushindani. Tuna mechi ngumu mbele yetu kuliko tulizocheza na hatutaki kupoteza.”

Simba ipo nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu ikiwa na pointi 57, nyuma ya Yanga yenye 65 kila mmoja ikicheza mechi 24 na kuteleza kwa Wekundu mechi hizo mbili zijazo ikiwamo ya Ihefu na Kariakoo Derby, itaipa nafasi kutangaza ubingwa mapema ikishinda dhidi ya Kagera Sugar.

Pamoja na kiwango bora ilicho nacho kwa sasa, Robertinho alisema anatamani kuona zaidi kuona mastaa wakiongeza njaa ya mafanikio.

SOMA NA HII  WAKATI SIMBA WAKIUGULIA KIPIGO CHA JUZI...AHMED ALLY AIBUKA NA HILI LINGINE..ATUPA JIWE YANGA...