Wakati Simba ikirudi Dar kutokea Morocco ilipokwenda kucheza mechi ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi C dhidi ya Raja Casablanca, inaelezwa kwamba, tayari mabosi wa klabu hiyo wamekamilisha mazungumzo na uongozi wa Al Hilal ya Sudan kwa ajili ya kumpata mshambuliaji msumbufu raia wa DR Congo, Makabi Lilepo.
Simba imefanikiwa kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo baada ya kufikisha alama 9, nyuma ya Raja Casablanca ya Morocco yenye 16.
Baada ya kufuzu, Simba imepania kufanya kweli zaidi kuanzia msimu huu na ujao katika michuano yote watakayoshiriki, hivyo kwa sasa wameanza mapema mikakati ya kuimarisha kikosi chao.
Chanzo chetu kutoka Simba, kimesema kuwa, muda wowote kuanzia sasa uongozi huo utaenda kumalizana na Lilepo huko Sudan.
“Tuliingia ushirikiano na Al Hilal wa kubadilishana wachezaji jambo ambalo sasa tunaenda kulifanya kuona tunapata mbadala wa Augustine Okrah, hatutaki kufanya tena makosa katika eneo la usajili,” kilisema chanzo hicho.
Kwa upande wa Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Mpango wetu msimu ujao ni kuhakikisha tunasajili watu sahihi, hivyo kwa sasa tunafanya kila namna kuangalia wachezaji bora na wenye uwezo katika klabu zote zilizoshiriki michuano ya kimataifa.
“Japo kusema hivi hakumaanishi tayari tumeshaanza usajili, tunasubiri ripoti ya kocha, hivyo kwa sasa sina tarifa ya mchezaji gani atakuwa nasi msimu ujao, zaidi tumepeana majukumu ya kuhakikisha kila mchezaji mzuri Afrika tutakayemtaka basi tutahakikisha tunamsajili.”