WAKATI homa ya pambano la watani wa jadi ikianza kupanda kabla ya timu hizo kuvaana Jumapili ya wiki hii, SOKA LA BONGO limenasa faili ya waamuzi watakaopewa pambano hilo la 110 katika Ligi ya Bara tangu ilipoasisiwa mwaka 1965.
Simba na Yanga zitavaana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, huku Mnyama akiwa mwenyeji, akiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya 1-1 katika pambano la duru la kwanza lililopigwa Oktoba 23 mwaka jana.
Imezoeleka mara nyingi majina ya waamuzi wanaopewa pambano hilo hufichwa na kuja kutajwa siku moja kabla hazijashuka uwanjani, lakini safari hii SOKA LA BONGO limeweza kuyanyaka mapema majina ya waamuzi wanne watakaochezesha dabi hiyo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Nassor Hamduni aliliambia SOKA LA BONGO kuwa tayari majina manne kwa ajili ya pambano hilo yameorodheshwa, ila yatatangazwa muda muafaka ukishafika.
Mwamuzi huyo wa zamani wa kimataifa, alisema wameteua waamuzi wanne pekee na sio sita kama ambavyo huko nyuma ilivyokuwa ikifanyika katika dabi zilizokuwa na presha kubwa.
“Tumechagua majina manne ya waamuzi wenye uwezo mkubwa ambao wote wana kitambaa cha Fifa kutokana na kuwepo kwa mwenendo mzuri waliokuwa nao hivi karibuni kwenye ligi.
“Kwa sasa tunangoja kuyaidhinisha na Jumatano yatawekwa wazi ili kila mmoja ajue na tumefanya hivyo kutokana nani viwango vya waamuzi kuongezeka kwa sasa,” alisema Hamduni.
Kutokana na kauli ya bosi huyo huku ikifahamika Tanzania ina waamuzi wenye kitambaa cha Fifa kuwa ni 14 na mmoja wapo (Salum Siyah) anachezesha Ligi Kuu ya Zanzibar. Waamuzi 13 waliosalia wapo Ligi Kuu Bara ambapo watano wanachezesha katikati ambao ni Ahmed Arajiga, Ramadhan Kayoko, Tatu Malogona, Jonesia Rukyaa na Hery Sasii.