Home Habari za michezo SIMBA YA ROBO NI TISHIO…VINARA LIGI YA MABINGWA AFRIKA WABAKI MIDOMO WAZI

SIMBA YA ROBO NI TISHIO…VINARA LIGI YA MABINGWA AFRIKA WABAKI MIDOMO WAZI

BEKI WA SIMBA SHOMARI KAPOMBE

MBRAZIL wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ wala hana presha na timu ambayo anaweza kupangwa nayo kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na badala yake yupo bize juu ya namna ya kufanyia kazi makosa yaliyojitokeza hatua hiyo ili kukiweka tayari kikosi chake.

Droo ya Robo Fainali ya mashindano ya CAF 2022/23, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika inatarajiwa kufanyika leo Jumatano, Aprili 5, 2023 mjini Cairo, Misri kuanzia saa 02:30 usiku kwa saa za huko (18h30 GMT na 03:30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki). Droo hiyo itaonyeshwa moja kwa moja kwenye majukwaa ya kidijitali ya CAF na TV washirika.

Wakati wadau wa soka nchini wakisubiri kwa hamu droo hiyo ili kujua wapinzani wa Simba na Yanga, Robertinho ambaye anatarajia kuanza programu zake za mazoezi leo, Jumanne yupo bize na mafaili ya kile ambacho kilitokea hatua ya makundi ambayo walimaliza nafasi ya pili (C), nyuma ya Raja Casablanca ya Morocco.

Kocha huyo alisema; “Hatuwezi kuchagua mpinzani wa kukutana naye, yeyote ambaye tutapangwa naye tutakabiliana naye, tunaweza kufanya maajabu na kushangaza Afrika, tutafanya maandalizi hatua kwa hatua, yapo ambayo tuliyaona kwenye makundi tutadili nayo ili kuweka sawa mambo kabla ya hatua ya robo fainali,”

“Siku zote nimekuwa na mtazamo chanya hivyo matarajio yangu ni makubwa, yaliyopita yamepita na kazi kubwa ni kuona vile ambavyo tunaweza kuwa bora maradufu hatua inayofuata, tupo pazuri nafikiri mashabiki wasubiri timu bora zaidi robo fainali.

“Tumeshafanya kazi ya kurekebisha makosa na muda tulionao tutamalizia, naamini kwenye ubora wa timu na hilo litatimia,” alisema kocha huyo aliyezaliwa miaka 62 iliyopita.

Katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ambao Simba ilikuwa Morocco kucheza dhidi ya Raja Casablanca, Robertinho alionekana kukerwa na makosa binafsi ambayo yaliwagharimu na kuwafanya kupoteza mchezo huo (3-1) ambao aliutazama kama kipimo cha robo fainali.

Mara baada ya mchezo huo, Robertinho alinukuliwa akisema; “Ni mpira wa miguu, ni wakati wa kuelewa kama hakukuwa na makosa leo labda mechi ingekuwa ya sare kwa sababu Raja alifunga kisha tukasawazisha na kisha kuna kitu kilifanyika ambacho sipendi kuzungumzia. Ni aibu, ni mpira wa miguu.”

Katika droo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, vinara wa makundi (4) ambao ni Wydad Casablanca, Raja Casablanca (Morocco), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Esperance de Tunis (Tunisia), watatenganishwa na wale ambao walimaliza nafasi za pili, Al Ahly (Misri), JS Kabylie, CR Belouizdad (Algeria) na Simba (Tanzania).

Kisha itachezeshwa droo kati ya timu ambazo zipo chungu cha kwanza (vinara) na wale ambao walishika nafasi za pili, timu ambazo zilitoka kundi moja mfano Simba na Raja Casablanca hawatakutana hatua hiyo na hata zile ambazo zinatoka nchi moja.

Katika droo ya nusu fainali, ambayo nayo itachezeshwa usiku huo, timu kutoka kundi moja au zile za taifa moja zinaweza kukutana dhidi ya nyingine.

Mechi za kwanza zitachezwa Aprili 15 na 16, na za marudiano zitachezwa Aprili 22 na 23, mwaka huu, Simba na timu nyingine ambazo zilishika nafasi ya pili kwenye makundi yao zitaanzia nyumbani na kumalizia ugenini ili kupata mshindi wa jumla.

SOMA NA HII  MAJERAHA YAMTESA PHIRI SIMBA...BALEKE AMKOSESHA RAHA...AMEFUNGUKA HAYA