Home Uncategorized SIMBA, NAMUNGO WATOENI KIMASOMASO MASHABIKI NA TAIFA KIUJUMLA

SIMBA, NAMUNGO WATOENI KIMASOMASO MASHABIKI NA TAIFA KIUJUMLA

 


MICHUANO ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kwa msimu wa 2020/21, inatarajiwa kuanza mwishoni mwa wiki ijayo ambapo kwa Tanzania Bara, Simba na Namungo ndiyo wawakilishi.

 

Simba ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu Bara kwa msimu uliopita, watashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na Namungo watacheza Kombe la Shirikisho Afrika.

 

Plateau ya Nigeria ndiyo wapinzani wa Simba katika hatua hii ya awali ambapo mechi ya kwanza itachezewa Nigeria kati ya Novemba 27 hadi 29, huku marudiano ni hapa Dar kati ya Desemba 4 hadi 6, mwaka huu.

 

Tarehe kama hizo pia tutashuhudia Namungo wakipambana na Al Rabita ya Sudan Kusini. Mechi ya kwanza ni hapa Dar na marudiano ni ugenini.

 

Tunaamini kuwa maandalizi mazuri ndiyo njia ya kupata mafanikio. Hivyo Simba na Namungo wanatakiwa kuwa makini na kwa kufanya maandalizi ya nguvu

 

Simba ina historia katika michuano hiyo na wengi wanatamani kuona timu hiyo inafanya vizuri na kuweka rekodi zaidi ya ile ya awali ambayo waliweka katika msimu wa 2017/18 kwa kufika robo fainali.

 

Lakini hili linawezekana endapo tu watafanya maandalizi bora na ya kutosha na kuwasoma vyema wapinzani wao jambo ambalo litakuwa msaada kwa wao kupata matokeo mazuri.

 

Michuano hii toka mwanzo ilifahamika kuwa ni lazima iwepo, hivyo timu zinatakiwa kujipanga kweli na kusiwe na visingizio vingi sijui mara ratiba siyo rafiki, kiukweli hilo lisipewa nafasi hata kidogo.


Kama Simba na Namungo walijipanga toka mwanzo walipopata nafasi hizo za kuiwakilisha Tanzania kimataifa jambo ambalo ni kubwa watafanya vizuri kwenye mechi za awali ambazo siku zote huwa ni sawa na fainali.

 


Tunaamini kila kitu kitakwenda sawa katika michuano hiyo ambayo ni muhimu kwa klabu zetu kuipa heshima Tanzania ambapo baadaye hutoa nafasi ya kuwa na timu nyingi katika michuano hiyo ya kimataifa.

 

Watanzania wengi ndoto yao ni kuona klabu hizo zinafanya vizuri kimataifa kwa msimu huu kwa kufika mbali na sio kuishia hatua za mwanzo kama ilivyokuwa msimu uliopita.

SOMA NA HII  DUH!KUMBE ISHU YA KICHUYA NA SIMBA KUNA FILAMU ILIKUWA INACHEZWA

 

Kwa upande wa wachezaji, mnapaswa kujituma kwa bidii kwani ni fursa kwenu kujitangaza kwenye soko la kimataifa.

 

Ni wazi kuwa ndoto ya kila mchezaji ni kucheza soka la kulipwa nje ya Tanzania lakini kikubwa mchezaji anapaswa kuwa na nidhamu pamoja na kujituma kwa bidii ili kuhakikisha mnatimiza malengo yenu.

 

Tunaamini kuwa timu zimejipanga kutokana na muda mwingi wa maandalizi kabla ya kuanza kwa michuano hii.

 

Usajili mlioufanya tuna imani ulikuwa unalenga zaidi michuano hiyo ya kimataifa hivyo tunategemea mtaipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

 

Mashabiki mnapaswa kuziunga mkono klabu hizo shiriki kwenye michuano hiyo ya kimataifa katika kuhakikisha malengo ya klabu yanatimia ili waweze kutotoa kimasomaso.