Home Habari za michezo WAFAHAMU USM ALGER WAPINZANI WA YANGA CAF…MAJAA KUMBE NI ‘MCHELE MCHELE TU’…HAWANA...

WAFAHAMU USM ALGER WAPINZANI WA YANGA CAF…MAJAA KUMBE NI ‘MCHELE MCHELE TU’…HAWANA MAAJABU..

Habari za Yanga

Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, wanakwenda kukutana na timu ya USM Alger ya Algeria kwenye mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Jumapili ijayo na marudiano yatakuwa nchini Algeria kwenye Uwanja wa Juillet wa Tano, Juni 3.

Watanzania wengi hawaifahamu vizuri timu hii, japo imeshawahi kucheza mechi mbalimbali za kimataifa. Je, wawakilishi wa Tanzania Yanga wanakutana na timu ya gani? Mwandishi wa makala haya anakuletea historia, rekodi na takwimu kadhaa kuhusu klabu hiyo.

Imetwaa ubingwa wa ligi mara nane

Jina kamili la klabu hiyo ni Union Sportive de la Medina d’Alger, kwa kifupi ndiyo inatamkwa USM Alger, klabu hii imeanzishwa mwaka 1937, miaka miwili tu baada ya kuanzishwa kwa Yanga. Ipo kwenye Ligi Kuu ya Algeria na Uwanja wake wa nyumbani ni Omari Hamadi wenye uwezo wa kuingiza watazamani 17,500.

Imeshatwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini mwao mara nane mpaka sasa ikiwa ni misimu ya 1962/63, 1995/96, 2001/02, 2002/03, 2004/05, 2013/14, 2015/16, na 2018/19.

Imeshika nafasi ya pili kwyenye Ligi Kuu mara nne, mwaka 1997/98, 2000/01, 2003/04, na 2005/06.

Ilifika fainali Ligi ya Mabingwa 2015

Mwaka 2015 ilifanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini kwa bahati mbaya ikafungwa jumla ya mabao 4-1 na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Ilichapwa mabao 2-1 nyumbani na ilipokwenda Lubumbashi iliambulia kipigo kingine cha mabao 2-0 na kulikosa kombe hilo. Na hayo ndiyo mafanikio makubwa zaidi ya klabu hiyo.

Iliteswa na Samatta

Kwenye mechi hizo mbili za fainali USM Alger hawatoweza kumsahau straika wa Kitanzania ambae ni nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta ambaye aliwafunga mabao mawili, kila mechi akishindilia bao moja.

Fainali ya kwanza ilichezwa Oktoba 31, 2015 kwenye Uwanja wa Omari Hamadi nchini Algeria, ilihushuhudiwa na watazamani 15,000, USM Alger ikilala mabao 2-1, yaliyofungwa na Ranford Kalaba dakika ya 28 na Samatta kwa mkwaju wa penalti dakika ya 79, huku bao lao la kufutia machozi likiwekwa ndani ya nyavu na Mohamed Seguer dakika moja kabla ya mechi kumalizika.

Fainali ya mkondo wa pili ilichezwa kwenye Uwanja wa TP Mazembe, Lubumbashi DRC, Novemba 8, 2015 ikishuhudia USM Alger akitandikwa mabao 2-0, Samatta akifunga tena bao kwa mkwaju wa penalti dakika ya 74 na Roger Assale dakika tatu za nyongeza kabla pambano kumalizika, hivyo kufungwa jumla ya mabao 4-1.

Imeshakutana na Yanga Shirikisho

Fainali hiyo inakwenda kuzikutanisha timu ambazo zimeshawahi kukutana mwaka 2018 kwenye kombe hilo hilo la Shirikisho barani Afrika, zikiwa Kundi D.

Mara ya kwanza ilikuwa Mei 6, 2018, USM Alger ikiikaribisha Yanga, kwenye mechi hiyo, wenyeji walishinda mabao 4-0, yaliyofungwa na Oussama Darfalou, Farouk Chafai, Abderrahmane Meziane na Mohamed Zemmamouche.

Zilikutana tena kwenye mzunguko wa pili Agosti 19, Yanga ikishinda mabao 2-1, mabao ya washindi yakifungwa na Deus Kaseke dakika ya 44 na Heritier Makambo dakika ya 47.

Nafasi ya nane Ligi Kuu

USM Alger inakamata nafasi ya nane kwenye Ligi Kuu nchini Algeria, ikiwa imecheza mechi 20, ikishinda tisa, sare tano na kupoteza jumla ya mechi sita. Imejikusanyia pointi 32 kwenye ligi hiyo yenye timu 16, inayoongozwa na kinara CR Belouizdad yenye pointi 50.

SOMA NA HII  KUELEKEA UCHAGUZI MKUU SIMBA...KABURU NJIA NYEUPEEE...KAZI ILIYOBAKI NI HII...