Home Habari za michezo KUELEKEA USAJILI MPYA SIMBA….HAWA HAPA MASTAA 10 WANAOTAKIWA KUPIGWA CHINI HARAKA…

KUELEKEA USAJILI MPYA SIMBA….HAWA HAPA MASTAA 10 WANAOTAKIWA KUPIGWA CHINI HARAKA…

Habari za Simba SC

Baada ya klabu ya Simba kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya robo fainali kwa mara ya nne kwenye misimu mitano, wanachama na mashabiki wa timu hiyo sasa wamekuja juu wakitaka mabadiliko makubwa kwenye kikosi.

Aprili 28, ikiwa nchini Morocco, Simba iliondolewa kwa mikwaju 4-3 ya penalti, baada ya kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Mabingwa Watetezi, Wydad Athletic Club ya Casablanca, baada ya matokeo ya jumla kusomeka bao 1-1 na kulazimika kupigiana matuta.

Hii ni baada ya Simba nayo kutanguliwa kushinda bao 1-0, Aprili 22 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Imekuwa ikiishia hatua hiyo tangu 2019, ilipotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa kwa mabao 4-1 dhidi ya TP Mazembe jijini Lubumbashi, baada ya mechi ya kwanza kutoka suluhu, 2021 iliondolewa kwenye hatua hiyo kwa mabao 4-3 dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, ikifungwa mabao 4-0 ugenini na kushinda mabao 3-0 nyumbani.

Mwaka jana iliondolewa kwenye hatua ya robo fainali kwa penalti 4-3 dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika ya Kusini, kila timu ikishinda bao 1-0 nyumbani.

“Viongozi wetu wameliona na kulijua hilo na kwenye dirisha hili la usajili ndicho tunachoenda kufanya.

Tutafanya kila linalowezekana ili kutoka hapa tunapoishia kwa miaka mitano sasa. Tunafanya usajili uliokuwa bora, tutatafuta wachezaji watakaoweza kutusaidia kutoka hapa kwenda kwenye hatua inayofuata, wachezaji tuliokuwa nao hivi sasa pasina shaka yoyote wanaweza kutufikisha robo fainali, hata Ligi ya Mabingwa ikianza hii leo, tuna uwezo wa kucheza robo fainali, sasa nini kinatakiwa?

Ni kusajili na kupata nyota wengine wapya kwenye viwango bora na vya juu, kuja kuungana na hawa wana wa robo fainali kuja kutupeleka nusu fainali na hata faimali,” alisema Meneja Habari na Mawasiliano Ahmed Ally hivi karibuni.

Wakati ikitaka kufanya usajili huo, wapo wachezaji ambao wataachwa mwishoni mwa msimu na taarifa zinasema itaacha wachezaji wengi, kwani ina kikosi kizima ambacho hakiwezi kusaidia kikosi cha kwanza.

Mwandishi wa Makala haya, ameorodhesha wachezaji 10 ambao wanatakiwa kuondoka na kupisha usajili wa wataokuja kuitoa hapa ilipo kwenda mbele.

1. Habib Kyombo

Alisajiliwa na kuanza kuitumika timu mwanzoni mwa msimu akitokea Mbeya Kwanza wakati huo ikiwa Ligi Kuu Tanzania Bara. Straika huyo alitegemewa kuchukua taratibu nafasi ya John Bocco ambaye umri imeanza kumtupa mkono, lakini hata akiingia haonyeshi chochote tofauti.

Ni mmoja wa wachezaji wanaotarajiwa kuonyeswa mlango la kutokea Msimbazi

2. Mohamed Outtarra

Beki huyu raia wa Burkina Faso kuelekea msimu huu akitokea Al Hilal ya Sudan akiwa tegemeo. Alitarajiwa kuziba vema pengo la Paschal Wawa aliyetimkia Singida Big Stars, lakini amekuwa akikaa benchi si kwenye michuano ya kimataifa tu, au ya Ligi Kuu, bali hata Kombe la FA. Huyu pia ni wa kuwapisha wachezaji wapya wataosajiliwa.

3. Gadiel Michael

Alijiunga na Simba mwaka 2019 akiwa kama mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Yanga. Tangu ajiunge hadi leo hajawahi kumtia wasiwasi Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kwenye namba yake ya beki wa kushoto.

Kwa muda wote huo amekuwa mchezaji anayekuwapo uwanjani kama mwenzake ni majeruhi, au amepumzishwa kwa ajili ya mechi muhimu. Kama Simba inayokuja inataka wachezaji wawili wanaopigania namba eneo hilo, anapaswa aondoke. Amekuwa hachezeshwi hata kwenye michuano kama ya FA.

4. Jonas Mkude

Ndiye mchezaji pekee aliyehudumu muda mrefu kwenye kikosi cha Simba. Alikitumikia kikosi cha vijana chini ya miaka 20 hadi mwaka 2015 alipopandishwa kwenye kikosi cha kwanza na kuhudumu kwa misimu minane sasa.

Hata tangu msimu uliopita, kiungo huyo mkabaji hayupo kwenye kiwango chake cha kawaida. Anatajwa kuwa huu ni msimu wake ya mwisho, na anatakiwa awapishe wengine.

5. Nassor Kapama

Kapama ambaye ni anacheza nafasi nyingi uwanjani, tangu asajiliwe hajaonyesha cha ziada ambacho wanachama na mashabiki wa Simba wanakifikiria.

Alisajiliwa msimu huu kutoka Kagera Sugar na ingawa hucheza mara chache sana, lakini kiwango anachoonyesha ni cha timu za kawaida na si timu yenye mahitaji makubwa kama Simba.

6. Augustine Okra

Kuna wakati anakupa ambacho wanachama na mashabiki wa Simba wanakitaka, halafu kuna wakati hakupi. Hivi karibuni alitoka kwenye majeruhi. Na angalau alionyesha mchezo mzuri kwenye mechi dhidi ya Namungo Jumatano iliyopita.

Hata hivyo inadaiwa ana mambo mengi nje ya uwanja na ndiyo inasababisha kutokuwa na mwendelezo mzuri. Kama Simba wanataka kufika nusu fainali msimu ujao, huyu pia anatakiwa aondoke.

7. Erasto Nyoni

Simba kama inataka kweli kuwafanya vema na kupita kwenye hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa haipaswi tena kuwa na mchezaji kama Erasto Nyoni. Siyo kama si mchezaji mzuri, lakini umri umemtupa mkono.

Mwaka 2007 alikuwa anaichezea timu ya taifa, Taifa Stars akiwa anaichezea Vital’O ya Burundi. Ni miaka 16 sasa imepita, akiwa amepitia timu za Azam na Simba. Sidhani kama anweza kuendana na kasi ya wachezaji vijana kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Anafaa awapishe sasa vijana.

8. John Bocco

Itakuwa si vema kama Bocco hatotendewa haki kwa kuachwa kwa heshima mwishoni mwa msimu huu. Nahodha huyo ameifanyia vitu vingi vizuri Simba ikiwamo kuipa ubingwa misimu minne mfululizo.

Kitendo cha viongozi kung’ang’ania aendelee si tu kama kinasababisha kuziba nafasi za kusajili vijana, lakini pia vijana wa sasa kumvunjia heshima yake anapokosea kwa sababu wao wanataka ushindi sio historia.

Inafaa naye aondoke au apewe kazi yoyote ile, ili nafasi yake ipate mtu mwingine damu changa ambaye anaweza kuitoa Simba hapo ilipo.

9. Ismael Sawadogo

Ni moja kati ya sajili mbovu zilizowahi kufanyika kwenye klabu hiyo. Na wala hakuna maneno mengi zaidi ya kusema tu awapishe wengine.

10. Peter Banda

Simba haijawahi kumfaidi mchezaji huyo, na wale yeye hajawahi kuipa chochote zaidi ya kuvumiliana tu. Ni mchezaji kijana ambaye amekuwa akiandamwa na majeruhi, kila anapocheza mechi moja tu, iwe timu ya taifa yake ya Malawi au klabu yake.

Tangu asajiliwe msimu wa pili huu unaelekea ametumia muda mrefu kujiuguza kuliko uwanjani.

Kwa sababu wachezaji wa kigeni wanatakiwa 12 tu na nafasi hizo ndizo zinatakiwa kusaka wachezaji bora watakaikwamua Simba, anatakiwa atolewe hata kwa mkopo kwenda kwenye timu nyingine kuliko kukaa na mchezaji ambaye klabu inatumia muda mwingi kumuuguza kuliko yeye kuitumikia timu uwanjani.

SOMA NA HII  MWENYEKITI WA SIMBA SC AFARIKI DUNIA