Home Azam FC AZAM FC WAANZA FUJO ZA USAJILI BONGO….WABEBA KIFAA HIKI CHA AL HILAL...

AZAM FC WAANZA FUJO ZA USAJILI BONGO….WABEBA KIFAA HIKI CHA AL HILAL YA SUDAN KIBABE…

Tetesi za Usajili Bongo

KLABU ya Azam Fc katika kuhakikisha inakuwa bora kwa msimu ujao, imebisha hodi Al Hilal ya Sudan ikitaka kumsajili kwa mkopo mshambuliaji wa timu hiyo, Lamine Jarjou.

Azam awali ilikuwa na hesabu za kuchukua wachezaji wawili kwa mkopo katika timu hiyo, Jarjou na Makabi Lilepo, lakini dili la Lilepo linaonekana kuwa gumu na hivyo mabosi wa timu hiyo wameamua kumkomalia straika huyo mwenye miaka 21 raia wa Gambia ili aje kuliamsha Chamazi.

Habari zinasema kuwa  upande wa Lulepo kuna mvutano mkubwa kwani sehemu ya pesa ya kumfanya Al Hilal kumuachia kiraka huyo mwenye uwezo wa kucheza kama winga zote na mshambuliaji wa kati ni takribani dola 250,000 ambazo ni sawa na Tsh 591 milioni kwa mkopo wa mwaka mmoja.

Kwa sasa Azam imegeukia upande wa Jarjou na uwezekano wa kukamilika dili hilo ni mapema kwa sababu mchezaji na yeye yupo tayari kutoka kwa mkopo ili apate nafasi ya kucheza kwenye timu inayocheza mashindano ya Caf.

Sababu kubwa ya mchezaji huyo kukubali kutoka pia ni nchi ya Sudan kuwa na vita huku ikiwa haijulikani ni lini itamalizika wakati huo huo sehemu zingine Ligi zikiendelea.

Inafahamika kuwa mabosi wa Azam tayari wameshaanza kufanya mazungumzo na Jarjou huku wakimtumia na kocha wao mkuu, Youssouph Dabo.

Dabo ni raia wa Senegali taifa lenye asili ya Jarjou, japo ana uraia wa Gambia, hivyo wanazungumza lugha moja na inaelezwa kuna ushawishi mkubwa wa mchezaji huyo kutua nchini.

Chanzo kimoja kutoka ndani ya Azam Fc, kilidokeza  kwamba wanataka kufanya usajili wa maana kama ilivyokuwa msimu huu na lengo ni kuongeza ushindani.

“Usajili wetu kwa kiasi kikubwa msimu huu wote wameona kwamba hatujafanya makosa makubwa kwa sababu wanacheza na wanashindana vya kutosha;

“Jarjou ni uhakika atakuja hapa labda tu mambo yabadilike lakini upande wa Lilepo na yeye kama mambo yatabadilika kwenye upande wa pesa yake basi atakuja, wote hawa ni kwa mkopo.”
Alipotafutwa msemaji wa Azam, Hasheem Ibwe alisema kwa kifupi;

“Kutakuwa na maingizo mapya kwenye timu na lengo ni kuhakikisha tunakuwa kikosi bora kama ilivyo sasa.”

SOMA NA HII  MECHI HII YA YANGA YAPELEKWA MBELE...HUYO NABI SASA!!