Home Habari za michezo VYUMA VIPYA SIMBA KUANZA KUANIKWA JUMATATU…WATAANZA NA HUYU…

VYUMA VIPYA SIMBA KUANZA KUANIKWA JUMATATU…WATAANZA NA HUYU…

Habari za Simba leo

Uongozi wa Simba SC umesema sasa wapo tayari kuanza kuwatambulisha wachezaji wake wapya waliowasajili kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na mashindano ya Kimataifa.

Simba SC itaanza kuwatangaza wachezaji hao Jumatatu ya Juma lijalo lakini imekiri kufanya mazungumzo na winga Mcameroon, Leandre Willy Onana Essomba anayetegemewa kujiunga na timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao.

Akizungumza jijini Dar es salaam Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema kuwa juma hili wanataka kumalizana na wachezaji wote ambao wataondoka, pia kupisha sikukuu ya Idd el Haji, kabla ya kuanza kuanika majembe yao kuanzia Jumatatu.

“Kuanzia Jumatatu tunaanza kuangusha mmoja mmoja kama mkwezi anavyoangusha nazi akiwa juu ya mnazi, huwa anaangusha moja baada ya nyingine, kwa hiyo tusubiri, tuwe na subira, tule kwanza Idd, tuchinje, Jumatatu tukiamka, tutaanza kuwatangaza wachezaji wetu wapya, kazi imeanza kuelekea msimu ujao,” amesema Ahmed.

Aidha, alisema kuhusu Onana ni kweli mchezaji huyo alikuja hapa nchini hivi karibuni na ameshaondoka.

“Onana ni mchezaji mzuri na ameshakuja Tanzania, tusubiri tuone kuanzia Jumatatu nani na nani watatangazwa kujiunga na Simba SC, sasa tuangalie kama atakuja Simba SC au hatokuja, wanachama na mashabiki wa Simba SC wavute subira, muda wetu ni ule ule saa saba mchana, jua kali dunia nzima inaona,” amesema Ahmed.

Hata hivyo, licha ya Ahmed kutoweka wazi, taarifa zinasema tayari Simba SC imeshamalizana na winga huyo wa kushoto akitokea klabu ya Rayon Sport ya Rwanda.

Msimu huu, Onana alishika nafasi ya pili kwenye orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Rwanda, akipachika jumla ya mabao 10, akitanguliwa na wachezaji wawili, Robert Mukongotya wa Mukura Victory na Shaban Hussein Shabalala wa AS Kigali, wote wakiwa na mabao 12, Kuhusu itakapoweka kambi msimu huu.

Ahmed amekiri kuwa wanataka kuweka nje ya nchi, lakini itategemea na watatangaza pale Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), litakapotoa ratiba yake ya msimu.

“Huwezi kuweka kambi kabla TFF kutangaza msimu mpya wa mashindano, ila tutakwenda nje,” amesema

SOMA NA HII  UKWELI LAZIMA USEMWE...GOLI LA ORLANDO HALIKUWA HALALI...JE..VAR HAINA MSAADA KWA WAAMUZI..?