Home Habari za michezo BAADA YA YANGA KUMCHUKUA MKUDE, SIMBA YAMLETA MBADALA WAKE

BAADA YA YANGA KUMCHUKUA MKUDE, SIMBA YAMLETA MBADALA WAKE

Baada ya kuachana na kiungo, Jonas Mkude aliyeitumikia Simba SC kwa miaka 13, Wanamsimbazi wamemalizana na kiungo Mtanzania, Hamis Abdallah anayekipiga nchini Kenya.

Simba SC ambayo nafasi ya kiungo wana wazawa wawili, Mzamiru Yassin, Nassoro Kapama na kwa upande wa wageni ni Sadio Kanoute na Willy Onana.

Ujio wa Hamis utaongeza chachu ya ushindani kwenye eneo hilo, huku kiungo huyo akiwa na kazi kubwa ya kufanya kuhakisha anapata namba mbele ya Mzamiru, ambaye amejitengenezea namba kikosi cha kwanza.

“Usajili wa kiungo huyo ni mapendekezo ya kocha ambaye aliomba kila nafasi kuwa na wachezaji wawili, ili kuwa na kikosi cha ushindani.

“Tayari Hamis amekamilisha usajili na atakuwa miongoni mwa wachezaji watakaoitumikia Simba SC msimu ujao, tunaamini ongezeko lake litakuwa na chachu ya ushindani,” kilisema chanzo hicho ambacho hakikutaka jina lake litangazwe hadharani.

Imefahamika kuwa usajili kwa upande wa wazawa umekamilika kwa mujibu wa ripoti ya kocha, ambayo ilikuwa inahitaji wachezaji watatu na hadi sasa wamekamilika.

Wachezaji wazawa waliosajiliwa dirisha hili la usajili ni Shaban Chilunda (mshambuliaji), Hussein Bakari, ambaye ni beki wa kati na Hamis katika kiungo.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ kwenye mazungumzo yake ya hivi karibuni, alisema bado wanaendelea kufanya usajili mzuri na kuna vifaa vingine vitatambulishwa

hivi karibuni. “Wachezaji wapya wanaendelea kuwasili kambini, nawakumbusha tu kusajili, hatujamaliza furaha zaidi itakuja hivi karibuni,” alinukuliwa Try Again juma lililopita.

Hadi sasa, Simba SC imesajili wachezaji saba, wakiwamo wanne wa Kigeni na watatu wazawa.

Wa kigeni ni Willy Onana, Aubin Kramo, Fabrice Ngoma na Che Malone Fondoh, wazawa wakiwa David Kameta, Hussein Bakari na Chilunda, huku Hamis akitarajiwa kuwa mzawa wa nne.

SOMA NA HII  WAWAKILISHI WA KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA, SIMBA, YANGA, AZAM, SINGIDA FG, RATIBA KAMILI IKO HIVI