Home Habari za michezo KOCHA WA SIMBA AFURAHI KUPATA SAINI YA ONANA, AFUNGUKA MPANGO WAKE

KOCHA WA SIMBA AFURAHI KUPATA SAINI YA ONANA, AFUNGUKA MPANGO WAKE

Tetesi za usajili Simba

Wakati kocha wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ akifurahia ujio wa mshambuliaji Leandre Onana kutoka Rayon Sports, nyota huyo anakutana na wakati mgumu katika kuingia kikosini moja kwa moja.

Simba ilikamilisha usajili wa Onana wiki hii na kupewa mkataba wa miaka miwili kukipiga Msimbazi, huku Robertinho akifurahia usajili wake.

Robertinho amesema Onana ni kijana mdogo mwenye uwezo mkubwa, hivyo kupata saini yake ni jambo bora, huku akiamini kuwa nyota huyo ataongeza ufanisi kwenye eneo la ushambuliaji.

“Kama nilivyosema tangu msimu uliomalizika, nataka kuona kila eneo nina wachezaji ambao wanaweza kucheza nafasi zaidi ya mbili uwanjani, hii itasaidia kuleta mapinduzi makubwa kwetu,” amesema.

Lakini Simba ambayo imemaliza katika nafasi ya pili pili kwa mara ya pili mfululizo kwenye Ligi Kuu, ndiyo iliyokuwa kinara wa ufungaji msimu uliopita, kwa kufunga mara 75, ikiwa pia imerruhusu machache (17), dhidi ya mabingwa, Yanga.

Kazi hiyo kubwa imefanywa na mfungaji bora, Saido Ntibazonkiza, aliyekuwa na mabao 17 na asisti 12, wakati Chama akifunga manne na asisti 17. John Bocco na Moses Phiri walifunga mara 10 kila mmoja.

Pape Sakho alikuwa na mabao tisa, wakati mpinzani mkubwa wa Onana katika kikosi cha kwanza, Jean Baleke akifunga mara nane na ‘hat trick’ mbili, Habib Kyombo na Kibu Denis wote wakiwa na mabao mawili.

Wadau wa soka wamebariki usajili wa Onana kwenye kikosi cha Simba wakisema licha ya timu hiyo kuwa kinara wa mabao ya kufunga msimu uliopita, bado walikuwa na shida wanapowakosa nyota kadhaa.

Mshambuliaji wa zamani Simba, Bakari Kigodeko alisema Simba haikuwa na mshambuliaji mwenye kipaji cha kufunga (Goal Gater), bali ilikuwa na wanaotumia nguvu kwenye kufunga, hivyo usajili wa Onana ni mzuri.

“Licha ya kwamba Baleke alikuja kuwa msaada kwenye kufunga, bado anatumia nguvu nyingi, Onana ni mchezaji mzuri na atakuja kuisaidia Simba.

“Simba msimu uliopita ilikuwa ikishinda mechi moja mabao mengi, lakini katika mechi nyingine wanapata tabu kupata mabao, nadhani ujio wa Onana utaongeza kitu, sioni kama kuna shida sana maeneo ya kiungo na beki,” alisema.

Mshambuliaji wa zamani, Emmanuel Gabriel alisema licha ya kutomfahamu Onana kwa upande wake, lakini rekodi aliyonayo mchezaji huyo inaonyesha ni mzuri.

“Kuna utofauti kati ya ligi yetu na Rwanda, kwahiyo anachotakiwa kuja kukifanya Onana ni kuonyesha uwanjani kwamba anaweza kufunga na si jambo lolote,” alisema.

Wakati huo huo, Kocha wa Fountain Gate, Novatus Fulgence alisema Simba kumsajili Onana wanaongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji, kwani kuna muda waliwahi kupitia nyakati ngumu.

“Si makosa kwao kuongeza mshambuliaji kwa sababu kuna wakati Phiri aliumia walipata tabu hadi Baleke (Jean) alipokuja kuwa sawa na kuanza kufunga,” alisema Fulgence.

SOMA NA HII  ISHU YA SINGIDA KUSHIRIKIANA NA YANGA KUIMALIZA SIMBA IKO HIVI