Home Habari za michezo NABI AFUNGUKA KILICHOMPONZA KAIZER CHIEFS BAADA YA KUONDOKA YANGA

NABI AFUNGUKA KILICHOMPONZA KAIZER CHIEFS BAADA YA KUONDOKA YANGA

Habari za Michezo

WAKATI mashabiki wa Kaizer Chiefs ya Sauzi wakiujia juu uongozi wa klabu hiyo kwa kumteua kocha mzawa,Molefi Ntseki, aliyekuwa kocha wa Yanga Nasreddine Nabi amefunguka kilichomzuia asitue kwenye timu hiyo aliyokuwa kwenye mazungumzo nao tangu aage Jangwani.

Nabi ameliambia Mwanaspoti, alikuwa kwenye hatua za mwisho kukubaliana na Kaizer lakini alishindwa kukubaliana na masharti ya viongozi waliomzuia kwenda na wasaidizi anaowataka hivyo akaona isiwe tabu.

Kocha huyo aliyeiongoza Yanga kwa miaka miwili na nusu na kubeba nao mataji saba tofauti yakiwamo mawili ya Ligi Kuu na ASFC pamoja na Ngao ya Jamii, alisema mipango yake ilikuwa kwenda Chiefs na wasaidizi wake angalau wawili muhimu.

“Niliwaambia siwezi kukubaliana na maamuzi yao, kwani nilitaka wanipe nafasi ya kwenda angalau na wasaidizi wangu wawili muhimu ambao naamini watanisaidia ninavyotaka mimi,” alisema Nabi na kuongeza;

“Niliona kuna ugumu kwao hasa waliponiambia wapo watu pale wenye mikataba nao na kuivunja ni gharama kubwa, nikaona hawataweza kunisaidia vile ambavyo nataka kuibadilisha timu yao na kuachana nao.”

Wiki iliyopita, Kaizer ilimtangaza Molefi Ntseki aliyekuwa timu ya vijana kuwa kocha mkuu kuchukua nafasi ya mzawa mwenzake Arthur Zwane anayekuwa kocha msaidizi kwa sasa na Nabi aliishukuru timu hiyo kwa kuonyesha imani naye japo mambo yalikwama na kukanusha ishu ya dau.

“Sikuwa na tatizo kuhusu malipo kila kitu kilikuwa sawa, ila walipaswa kujifunza kwa Pitso (Mosimane) kila anapoenda anaenda na wasaidizi, ishu eti niliikata Yanga ili niende Kaizer ni watu kusema wasichokijua, kwa sasa ni wakati mzuri kukaa karibu na familia hili ni muhimu,”alisema na kusisitiza kwamba kwa sasa ana mipango mipya itajulikana punde.

SOMA NA HII  DIARRA YANGA MAMBO YAZIDI KUNOGA, ALAMBA DILI HILI LA KIBABE