Home Habari za michezo MSUVA AFUNGUKA MASHARTI YAKE HAYA KAMA SIMBA, YANGA ZINAMTAKA

MSUVA AFUNGUKA MASHARTI YAKE HAYA KAMA SIMBA, YANGA ZINAMTAKA

SIMON MSUVA AMUHAKIKISHIA MAMA SAMIA...AFCON 2023 TUNAKWENDA

WAKATI mastaa wenzake wa daraja lake wakila bata kwenye fukwe mbalimbali za starehe kipindi hiki cha mapumziko mambo ni tofauti kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Simon Msuva amekuwa akitumia zaidi ya saa mbili kwa siku kuvuja jasho ili kuwa tayari kwa kazi muda wowote.

Kwa sasa Msuva yupo nchini kwa zaidi ya wiki tatu kwa mapumziko kufuatia msimu wa Ligi Daraja la Kwanza Saudia Arabia kumalizika, pia anasikilizia dili mpya na nono ambazo zitatokea kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho na watu wake siku chache zijazo katika kipindi hiki cha usajili.
Mkataba wa Msuva na Al-Qadsiah FC aliyeichezea kwa mwaka mmoja ulimalizika Juni 30, 2023 na kwa mujibu wa taarifa kutoka Saudia inaelezwa mabosi wa timu hiyo wameandaa ofa mpya kwa nyota huyo ambaye alipachika mabao manane na kuwa mfungaji wao bora.
Lakini pia Mwanaspoti linafahamu kuwa Al Duhail ambayo anicheza Mkenya Michael Olunga huko Qatar ni miongoni mwa timu ambazo zinasaka saini yake.

Ukweli wa hayo na mengine mengi huyu hapa Msuva ambaye tumefanya naye mahojiano ya kina kwenye fukwe ya Escepa One ambako alikuwa akivuja jasho na wachezaji wengine wa Ligi Kuu Bara ambao amekuwa na ukaribu nao na kufichua kwanini anajifua kama amepewa adhabu.
“Kazi yetu inahitaji uwe tayari muda wowote, unaweza kuona kuwa huu ni muda wa mapumziko lakini ukijiachia sana unaweza kurudi kuanza maandalizi ya msimu ukajikuta uko nyumam, tofauti na wenzako, ni vizuri kuwa tayari, ujue sisi muda mwingine ni kama askari vile,” anasema Msuva.

DILI ANAZOTAKA
Nyota huyo wa zamani wa Moro United na Yanga aliyeanza soka lake katika klabu ya Azam kisha kwenda Morocco kukipiga Difaa El Jadida na Wydad Casablanca, anasema vipaumbele vyake kwa sasa ni kwa dili za timu za Falme za Kiarabu (UAE) wenye watu wenye fedha zao.

“Nahitaji kutengeneza pesa na sio kitu kingine, niwe muwazi kwa sasa sifikirii kabisa kurudi nyumbani, hata kama itatokea timu ambayo itanipa ofa ambayo itaendana na huku ambayo nitapata, zipo sababu za msingi,” anasema Msuva na kuongeza;

“Uwezekano wa kutengeneza pesa Uarabuni ni mkubwa kwa sababu mbali na pesa ya usajili wamekuwa wakilipa mishahara mizuri ambayo huwezi kulinganisha na nyumbani japo naona siku hizi mambo sio mabaya wapo wachezaji ambao nimekuwa nikiona wanalipwa vizuri ila sio kama kule (Saudia).”
Kuhusu ofa zilizopo hadia sasa, nyota huyo anayeshika nafasi ya tatu kwa kufunga mabao mengi kwenye kikosi ca Taifa Stars nyuma ya Mrisho Ngassa na Mbwana Samatta anasema; “Sio sawa kuziweka sawa wakati bado hatujamalizana, naweza leo kusema hivi halafu kesho mambo yakabdilika ni vizuri kuwa na subira na kuona nini kitatokea kwa sababu bado dirisha la usajili lipo wazi hadi mwezi wa nane, ila zipo timu za Saudia, China na Qatar. Naweza kucheza kwenye moja ya mataifa hayo.”

ALIVYOTUA SAUDIA
Msuva anasimulia alivyotua Saudi Arabia haikuwa kinyonge na alikuwa tayari kucheza Ligi Daraja la Kwanza kutokana na maslahi mazuri ambayo alipewa na Al-Qadsiah FC ambayo ilikuwa na mpango wa kupanda ligi kuu nchini humo.

“Nilipokewa vizuri na kupewa heshima kubwa kwa sababu walijua mimi ni mchezaji wa timu ya taifa, walinipa nyumba nzuri na gari la kifahari, sikuwa na maisha ya kinyonge kwakweli nilipata kila ambacho nilikuwa nikihitaji,”

“Walijitahidi viongozi na wachezaji ambao tuliwakuta ili kuhakikisha ninazoea maisha ya pale (Saudia), walihisi naweza kupata tabu kwa sababu sijawahi kuishi humo lakini niliwaeleza kuwa nilicheza mpira Morocco kwa miaka mingi hivyo wasiwe na wasiwasi na mimi,” anasema Msuva na kuongeza;.

“Kiukweli hakuna changamoto yoyote ya maisha ambayo nilikumbana nayo kwa sababu tamaduni za Waarabu ni kama zinaendana hivyo hapakuwa na jipya kwangu zaidi ya kuwafanyia kazi yao kama ambavyo walikuwa wakitegemea.”

UPWEKE ALISHAZOEA
Wapo wachezaji ambao wamekuwa wakishindwa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kutokana na upweke, Msuva kwake ni tofauti kutokana na umuhimu wa ndoto zake kuwa mkubwa kuliko kuwa karibu na ndugu na majamaa huku mambo yakiwa hayaendi.

“Kukaa karibu na washikaji halafu mambo yakiwa hayaendi kuna faida gani, nimeamua kukubali upweke ili nitengeneze wepesi wa maisha yangu hata baada ya kuachana na mpira pamoja na ndugu na jamaa ambao wamekuwa wakiniangalia, nikiwakumbuka sana nitawapigia simu,” anasema.

HII KALI
Wanaume pekee ndio wana haki isiyo na masharti ya kuanzisha talaka.
Hiki ni kati ya mambo ambayo aliyasikia; “Yapo mambo mengi ambayo kimsingi ni tofauti kabisa na kwetu Tanzania, wanawake wamekuwa wakijitunza sana kwa wenzetu na ni ngumu kumuona akizurura hovyo mtaani.”

Kwa mujibu wa Sheria kwenye ishu ya talaka inatamka tu kwamba mwanamke anapaswa “kujulishwa” kuhusu talaka na ana haki ya kulipwa fidia ya kifedha ikiwa hajafahamishwa. Kinyume chake, wanawake hawana haki ya kukomesha ndoa kwa upande mmoja.

ISHU YA PITSO
Kama sio changamoto ambazo kocha Muafrika Kusini, Pitso Mosimane alikumbana nazo Al Ahli Saudi FC basi huenda msimu ujao wawili hao wangefanya kazi pamoja kwani alishapendekeza jina la mshambuliaji huyo kwenye kikosi chake.
“Tuliongea na kwa bahati nzuri ananifahamu kabla ya hata kwenda Saudi Arabia na hata tulipoonana kwenye mechi ambayo niliifunga timu yake alisema kuwa mimi ni Mtanzania na tulibadilisha namba kwa sababu anapenda kazi yangu na alitamani tufanye naye kazi msimu uliofuata,”

“Bahati mbaya imembidi aondoke baada ya kuipandisha timu daraja kutokana na changamoto ambazo zilikuwa zimetokea, ujue Waarabu wapo na jeuri ya pesa, wanaweza kufanya chochote wanachojisikia, lakini nilimtakia kila la kheri huko ambako amepata kazi mpya,” anasema.

Baada ya kuachana na Al Ahli Saudi FC, Pitso alikuwa miongoni mwa makocha ambao walikuwa wakihusishwa kuchukua mikoba ya Nasriddine Nabi aliyeomba kuondoka Yanga baada ya kumalizika kwa msimu uliopita wa 2022/23.

FOWLER KUTUA AL QADSIAH
Siku chache zilizopita nyota wa zamani wa Liverpool, Manchester City na timu ya taifa la England, Robbie Fowler alitangazwa kuwa kocha mpya wa chama ambalo Msuva amemaliza mkataba wake, anaongeleaje uteuzi huo.

Al-Qadsiah aliandika kwenye mitandao yao ya kijamii: “Robbie Fowler. Mmoja wa wachezaji maarufu katika Liverpool na Ligi Kuu ya Uingereza. Ni Kocha wa Qadisiyah.”
“Naamini anaweza kuisaidia timu kutoka sehemu moja na kwenda nyingine kutokana na uzoefu alionao kwenye soka. Bado hajanitafuta na pengine kwa sababu kila kitu changu kipo kwa watu ambao wananisimamia, naamini kabla ya kufanya maamuzi ya mwisho tutawasikiliza,” anasema.

Fowler ambaye enzi zake alikuwa mshambuliaji, anakibarua cha kuzungumza na baadhi ya nyota wa timu hiyo akiwemo Msuva kuhakisha wanaongeza mkataba wa kuendelea kuipigania timu hiyo kupanda daraja.

SIMBA, YANGA NI TISHIO
Viwango vya miamba ya soka la Tanzania, Simba na Yanga vimemkuna Msuva kwa kusema kwa sasa ni tishio kwenye soka la Afrika na kama wataendelea na kasi waliyonayo wanaweza siku moja kutwaa ubingwa wa Afrika.
“Nimecheza soka nyumbani kabla ya kwenda nje, naweza kusema soka la kipindi kile ni tofauti kabisa na sasa, kuanzia kwenye maslahi ya wachezaji hadi upande wa ushindani kwa sababu nimeona ongezeko la wadhamini linazifanya timu kuwa na nguvu kubwa ya ushindani,”

“Wapo marafiki zangu ambao wamekuwa wakiniuliza kuhusu klabu hizo kutokana na ofa ambazo wamekuwa wakipewa na nimekuwa nikiwaeleza uzuri wake na changamoto ambazo wanapaswa kujiandaa kukabiliana nazo maana ni timu kubwa ambazo zinapresha kubwa. Binafsi natamani siku moja kusikia timu ya Tanzania ikichukua ubingwa wa Afrika itakuwa heshima,” anasema.

Ndani ya miaka ya hivi karibuni, Simba imefika mara tatu katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mara moja upande wa shirikisho ambao Yanga msimu uliopita alitinga fainali ambayo alipoteza kwa kanuni ya bao la ugenini, mchezo wa kwanza alipoteza kwa mabao 2-1, ushindi wa bao 1-0 akiwa ugenini dhidi ya USM Alger haukutosha kutwaa ubingwa huo.

YEYE NA WYDAD FRESHI
Miezi 12 iliyopita Shirikisho la Kimataifa ‘FIFA’ liliagiza Mabingwa wa Soka Barani Afrika kwa wakati huo Klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, kumlipa Msuva zaidi ya dola laki saba (Sh 1.6Bilion).
FIFA ilitoa agizo hilo kwa Wydad Casablanca, baada ya kukamilisha kesi iliyokuwa inaunguruma baina ya pande hizo mbili kwa zaidi ya miezi sita.

Hata hivyo Wydad Casablanca ndio ilikua ya kwanza kufungua kesi dhidi ya Msuva, ikiamini Mchezaji huyo alikua na jambo la kujibu kwa madai alivunja mkataba bila sababu, lakini mambo yaliwageukia na hapa Msuva anasema alishawasamehe kwa yote na hana tatizo nao.
“Siwezi kuficha kuwa nilipitia kipindi kigumu sana kwenye maisha yangu ya soka lakini nashukuru Mungu nilivuka, wapo ambao walisimama na mimi na kunitia moyo ila ndio mpira lazima muda mwingine tukutane na changamoto ili zituimarishe,”

“Baada ya kunilipa changu nilifungua moyo na kuangalia upande mwingine wa maisha, nilicheza kwa moyo wangu wote Wydad kwa sababu ni moja ya klabu kubwa Afrika na ni kweli iliongeza thamani yangu kama mchezaji,” anasema.
Msuva aliifungulia Mashtaka Wydad Casablanca, kwa kushinikiza kulipwa stahiki zake, ambazo hakuzipata kwa muda mrefu kutoka kwa miamba hiyo ya Afrika.

“Ule msimu ambao walitwaa ubingwa wa Afrika nilikuwa sehemu ya kikosi chao ambacho kiliuanza msimu na nilifanya vizuri mechi za awali. Sikupata medali na wala sikuona sababu ya kufuatilia kwa sababu tuliachana kwa misuguano,” anasema Msuva.

Msuva alisaini mkataba wa miaka minne na Klabu hiyo ya Casablanca, alilazimika kuusitisha mkataba huo mwezi Disemba mwaka 2021, kutokana na malimbikizo ya mishahara pamoja na sehemu ya pesa yake ya usajili (signing fee).

ALIPOTEA CASABLANCA
Casablanca ni mji wa bandari na kitovu cha kibiashara magharibi mwa Morocco, mbele ya Bahari ya Atlantiki. Msuva aliwahi kupotea hapa anasimulia namna ilivyokuwa wakati akicheza soka la kulipwa nchini humo.

“Nilikuwa nikitoka sehemu moja na kwenda nyingine, aiseeh Casablanca imejengeka sana na kwa mgeni kidogo inahitaji uwe makini mno vinginevyo unaweza kukutana na kama kilichonikuta, nilipotea ikabidi nianze kuuliza lakini nashukuru Mungu wenyeji walinisaidia,” anasema.

REKODI YA STARS
Msuva ambaye amekuwa kwenye kiwango bora kwa muda mrefu, anafukuzia rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote kwenye kikosi cha timu ya taifa, ameachwa mabao manne na Mrisho Ngassa anayeshikilia rekodi hiyo akiwa na mabao 25.
Msuva anajisikia raha na fahari kuwa mmoja wa wachezaji ambao wapo kwenye orodha hiyo.

“Natamani ukifikiwa wakati wa kustaafu kwangu kuwe na mengi mazuri ambayo nilifanya kwenye taifa langu, kila siku nimekuwa nikijituma na kujitoa kwa ajili ya kufanikisha yale ambayo watanzania wamekuwa wakitamani kuona yakifanywa na timu yao,” anasema.
Msuva anashika nafasi ya tatu kwenye orodha hiyo nyuma ya nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta mwenye mabao 22. Ngassa ambaye ameachana na soka la ushindani aliweka rekodi hiyo kuanzia 2006–2015.

VIATU VYAKE USIPIME
Ukiipenda kazi yako haiwezi kuwa ishu kujigharamikia ndivyo ilivyo kwa Msuva ambaye amekuwa akitoa dolla 400 (Sh. 969,822) kwa ajili ya kununua viatu vyake vya kuchezea soka aina ya Nike ambavyo amekuwa akivipenda kwa miaka mingi.
‘Nimekuwa nikipenda kuvaa viatu vya Nike miaka mingi sasa kwa sababu hunisaidia kufanya yale ambayo nahitaji uwanjani kwa urahisi,” anasema.

WASHIKAJI ZAKE
Kila ambapo amekuwa akirejea Tanzania, Msuva anasema amekuwa akiwakumbuka washikaji zake wa kitaa ambao asilimia kubwa ni wachezaji ambao bado hawajatoboa kwa kuwaletea vifaa ili kuchochea ndoto zao.

“Timu yangu ya mtaani ni Baruti na nimekuwa nikifanya nayo mazoezi siku moja moja, nimekuwa nikiongea na wachezaji wadogo kuwaeleza vile ambavyo wanaweza kutoboa, siwezi kusaidia kila mmoja ila ambacho najaaliwa nimekuwa nikiwashika mkono,” anasema mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga.

Wasifu:
Jina: Simon Happygod Msuva
Kuzaliwa: Oktoba 2, 1993
Mahali; Dar es Salaam
Uraia: Tanzania
Urefu; 1.75 m (5 ft 9 in)
Nafasi: Winga/Straika
Klabu: Al-Qadsiah FC
Alikopita: Azam, Moro United, Yanga, El Jadida na Wyda

SOMA NA HII  GOMES: TUNA SAFU BORA YA ULINZI