Home Habari za michezo YANGA MPYA INGETAKIWA IWE HIVI

YANGA MPYA INGETAKIWA IWE HIVI

KOCHA YANGA AMPIGIA SALUTI DIARRA...AONGOZA KWA UOKOAJI SHIRIKISHO

YANGA ndio timu Bora Tanzania kwa sasa. Kama unapenda sawa. Kama hupendi, sawa pia. Hawakuchukua ubingwa wa ligi yetu kwa bahati mbaya. Hawakuchukuwa Kombe la FA kwa bahati mbaya. Ni ubora juu ya ubora.

Hawakuwafunga TP Mazembe nje ndani kwa bahati mbaya. Hawakufika Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa bahati mbaya. Ni ubora juu ya ubora. Asikwambie mtu, kocha bora anahitaji wachezaji bora. Hata Pep Guardiola, anahitaji kuwa na wachezaji bora kwenye kikosi kishinda mataji. Anahitaji Kelvin De Bruyne. Anamhitaji Earling Haaland. Ungependa Yanga mpya iweje kuelekea msimu ujao?

Naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Natamani Yanga wampate mtu kama Bruno Gomes wa Singida Fountain Gate. Yule Mbrazili ni fundi kweli kweli wa soka.

Anaweza kufanya vitu vingi sana uwanjani. Yanga hawana mchezaji mbunifu kama Bruno. Anajua kufunga. Ana kasi na pasi zake ni uhakika.

Yanga mpya inahitaji kuwa na kiungo mbunifu ambaye anaweza kuiunganisha vema safu ya ulinzi na safu ya ushambuliaji. Ni muda muafaka kabisa wa kupiga hodi pale Singida na kumchukua Bruno. Alikuwa mhimili mkubwa sana wa Singida msimu uliopita.

Amechangia mno Singida kumaliza nafasi ya nne. Kama Yanga wanataka kweli kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya 30, Bruno ni moja ya watu wanaohitajika kikosi. Ni aina ya mchezaji ambaye akija Jangwani, anaingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza.

Moja kati ya maeneo ambayo Yanga wanapoteza asili, ni upande wa mawinga. Baada ya Simon Msuva na Mrisho Ngassa kuondoka, Yanga haijawahi kupata winga wa maana. Imepata wasanii tu. Imepata wanariadha tu. Ni muda wa kuleta winga wa ukweli kama Kipre JR wa Azam FC. Yule ni aina ya mawinga wanaohitajika ndani ya Yanga.

Sio tu kwamba ana kasi, yule mtu fundi. Mabeki wengi watapasua viatu msimu ujao. Fundi sana mguuni. Ukitazama pale Yanga, Farid Mussa hajatumika sawasawa. Ukitazama Jesus Moloko, umaliziaji wake bado sio wa kiwango cha juu.

Kama Yanga wangekuwa wanaweza kusajili wachezaji waliocheza ligi yetu msimu uliopita, ningeshauri waende Azam FC na kumchukua Kipre JR. Hawa ni aina ya wachezaji wa kigeni tunaowahitaji nchini.

Mchezaji wa kigeni ni lazima aonyeshe tofauti kubwa uwanjani. Kama Yanga wanataka kucheza tena Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, unahitaji kuwa na mawinga kama Kipre JR. Mchezaji ambaye ana uwezo wa kupunguza mabeki hata wawili na kutengeneza nafasi.

Mchezaji ambaye anaweza kuuficha mpira. Winga wa aina hii hayupo pale Jangwani. Mchezaji mwenye ubora huu, haonekani pale Yanga. Kitendo cha Yanga kufika fainali msimu uliopita, ni kama kutangaza vita msimu huu.

Yanga sio “Underdog” tena. Yanga sio wadogo tena. Wanahesabika kama timu kubwa sasa Afrika. Unataka Yanga mpya iweje? Naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Kwa gharama yoyote, Fiston Mayele na Djigui Diarra ni lazima wabakie kikosini. Kumpoteza hata mmoja, gharama yake ni kubwa sana. Kwangu mimi, hawa ndio wachezaji ambao pengo lao ni kazi sana kuliziba wakiondoka.

Ukitazama pale katikati, Yannick Bangala hakuwa na msimu mzuri. Alikuwa chini sana msimu uliopita. Khalid Aucho ni mchezaji mzuri, lakini umri nao unamkimbiza. Yanga wanahitaji kupata kiungo mmoja wa chini wa maana.

Wanahitaji mtu aina ya James Akaminko au Mzamiru Yassini. Wanahitaji mtu flani hivi katili pale katikati kukichafua. Yanga haiko salama sana kwenye kiungo.

Wanahitaji mabadiliko makubwa. Mtu katili mmoja anahitajika. Kama Yanga wanataka kutetea ubingwa wao wa ligi, wanahitaji mtu aina ya Akaminko. Kama wanahitaji kwenda Fainali ya Afrika, wanahitaji mtu kama Mzamiru Yassini.

Umeitazama Yanga vizuri kwenye eneo la kiungo? Naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Ujio wa Mudathir Yahya ulikuwa na tija kubwa sana, ingawa ametumika zaidi kama kiungo mshambuliaji.

Salum Abubakar ‘Sure Boy’ ni mtu na nusu, lakini bado nawaona wanakosa mtu wa kazi wakutuliza dimba. Mchezaji aina ya Akaminko ni muhimu sana.

Moja kati ya vitu nilivyoshangaa msimu uliopita, ni kuona Djuma Shaban na Joyce Lomalisa wanawekwa benchi na Kibwana Shomari na Dickson Job.

Haya yalikuwa ni matusi makubwa sana kwa Wakongomani hao. Kibwana sio beki asili wa kushoto, kumpeleka benchi Lomalisa ni kumkosea heshima. Job sio beki wa pembeni wa asili, kumweka benchi Djuma ni dharau kubwa.

Nadhani ni muda wa kuwarudisha Djuma na Lomalisa kwenye kikosi cha kwanza. Yanga wanatakiwa kuleta beki wa kati wa miraba minne pale kwenye ukuta wao.

Kipande cha mtu kama Pascal Wawa wa zama zile . Mtu ambaye atakuwa juu ya Bakari Mwamnyeto na Dickson Job.

Hapo ukuta itakuwa tayari kwa mapambano. Hapo tayari safari ya kutwaa ubingwa wa 30 wa Ligi Kuu itakuwa imeanza. Kennedy Musonda na Mayele wanatosha kabisa kukimbiza kule juu. Hii ndio Yanga ninayoiona mimi.

Najua umewafuatilia sana Wananchi. Naomba maoni yako kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba yangu ya simu hapo juu. Kama watapata mawinga wawili aina ya Kipre JR, moto utawaka sana msimu ujao. Kama watapata mtu kazi kama Akaminko pale kati, watu maji wataita mma!

Kama watapata mtu mwenye udambwidambwi kama Bruno Gomes wa Singida, watu watalala na viatu. Kama watapata beki kisiki mmoja kama Henock Inonga. Ukuta utakuwa salama kabisa kwa msimu ujao. Tukutane Jumatano kwenye safu yangu ya Mzee wa Kaliua. Nina jiwe moja zuri sana hutakiwi kulikosa Mwanaspssoti Jumatano.

SOMA NA HII  YANGA HII SASA TOO MUCH