Home Habari za michezo YANGA YAIFANYIA UMAFIA SIMBA KWENYE USAJILI

YANGA YAIFANYIA UMAFIA SIMBA KWENYE USAJILI

Tetesi za usajili Yanga

KAMA Kocha Miguel Gamondi ataridhia wiki hii mazoezini kwamba Djuma Shabaan apigwe chini, viongozi watashusha chuma kingine fasta ambacho inadaiwa hata Simba walikitamani.

Mwanaspoti limejiridhisha kwamba, Yanga imefanya mazungumzo na beki wa kulia pale Asec Mimosas ya Ivory Coast, Kouassi Yao tayari ameshakaa mguu sawa kuja kuchukua jezi ya Mkongomani huyo.

Yao ambaye pia anacheza kama winga mabosi wa Yanga wanapiga hesabu kwamba ni mtu muafaka wa kuja kuongeza kasi upande wa kulia kwani hata kwenye ripoti ya Kocha Nabi Mohamed alishawaambia kwamba wamchomoe Djuma walete mtu wa kazi.

Kwa mujibu wa rekodi zake, beki huyo mpya anajua kupiga krosi za maana Gamondi hatakuwa na shida katika kumuingiza kwenye mifumo yake kutokana na pia anahitaji beki mwenye ubora wa kujua kupandisha mashambulizi na kuzalisha krosi nyingi haswa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa inayoanza Agosti 20.

Mwanaspoti linajua Yao aliwahi kuzungumza na Simba wamsajili msimu huu lakini wekundu hao wakakumbana na ugumu wa nafasi za wachezaji wa kigeni na kuamua kuachana naye wakamchukua mzawa David Kameta Duchu waliyemrudisha juzi usiku kwa mkataba wa miaka mitatu.

Simba iliwahi kumsajili Duchu akitokea Lipuli ya Iringa lakini hakuweza kufanya makubwa wakamtoa kwa mkopo na sasa wamemrudisha kundini.

Yao uzoefu wake wa miaka mitatu katika mashindano ya Afrika utambeba ndani ya Yanga ambayo msimu ujao itakuwa na kibarua cha kuendeleza makali yao kufuatia kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliokwisha.

Faili la Djuma pale Yanga halisomeki vizuri wakipiga hesabu za kumng’oa kwa kuangalia takwimu zake za uchezaji msimu uliopita lakini pia nafasi yake ya mchezaji wa kigeni, mabosi wa klabu hiyo wanaona hajafanya maajabu makubwa katika miaka yake miwili.

Ukiacha ubora wake kutokuwa mkubwa Djuma pia anatajwa kwamba nidhamu yake haiwaridhishi mabosi wake lakini uamuzi wa mwisho ameachiwa kocha wao Miguel Gamondi ambaye rasmi leo ataanza nae mazoezi ya uwanjani.

Djuma bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Yanga ambapo tayari beki huyo ameshatua nchini kuja kuanza msimu mpya chini ya Gamondi, baada ya ushawishi wake wa kutaka kusitisha mkataba kukwama, huku Yanga wakimuangalia kimachale.

Inaelezwa kwamba Djuma ana hesabu za kuelekea TP Mazembe ya DR Congo ingawa miamba hiyo tayari imeshamchukua beki mpya wa kulia kutoka Mauritania Ibrahima Keita ambaye kama aliyekuwa kocha wa Yanga Nasreddine Nabi angebaki alitaka asajiliwe Yanga.

Gamondi amesisitiza kwamba anataka timu inayoupiga mwingi na ndio maana ametaka Kambi ianze mapema.

SOMA NA HII  WAKATI YANGA WAKIMNGOJA KWA HAMU MANZOKI....BUMBULI ATUPIWA VIRAGO KIMYA KIMYA...MRITHI WAKE NI HUYU HAPA....