Home Habari za michezo MAYELE AFUNGUKA MAZITO BAADA YA KUONDOKA YANGA

MAYELE AFUNGUKA MAZITO BAADA YA KUONDOKA YANGA

Aliyekuwa Mshambuliaji kinara wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Fiston Kalala Mayele amesema anaamini siku moja atarudi tena kuitumikia timu hiyo kutokana na sapoti na mafanikio makubwa aliyoyapata akiwa na miamba hiyo katika kipindi cha misimu miwili mfululizo.

Mshambuliaji huyo juzi Jumapili (Julai 30) alitambulishwa rasmi kwenye timu yake mpya ya Pyramids FC ambayo amejiunga nayo kwa mkataba wa miaka mitatu, huku Young Africans ikinufaika kwa kubeba kitita cha Sh bilioni 2.8 kutokana na mauzo yake.

Akizungumza akiwa nchini Misri Mshambuliaji huyo alieleza kuwa ameondoka Young Africans kwa nia njema na lengo lake ni kwenye kusaka changamoto mpya kwa ajili ya maisha yake na familia yake.

“Haya ni maamuzi magumu kwangu, uongozi ulipambana kuhakikisha nabaki, tulifanya vikao vingi lakini maamuzi yangu niliamua kuondoka ingawa siyo kwa ubaya nashukuru viongozi wamenielewa na kunikubalia ombi langu naamini ipo siku nitarudi tena Young Africans,” amesema Mayele.

Mshambuliaji huyo amesema ingawa anahisi machungu makali kuondoka Young Africans, lakini mafanikio aliyoiachia timu hiyo katika misimu miwili aliyoitumikia yanamfanya ajione shujaa na kumwondolea unyonge huku akiwataka wachezaji wapya na wale wa zamani kuendelea kuipigania timu hiyo ili kufanya vizuri msimu ujao.

Amesema akiwa Young Africans, aliishi kama yupo kwao Lubumbashi hiyo ni kutokana na mapenzi makubwa kutoka kwa viongozi na mashabiki wa timu hiyo na hivyo vikamwezesha kufanya kazi yake kwa mafanikio makubwa na kubeba mataji sita akishikiriana na wachezaji wenzake.

Amesema pamoja na kuondoka kwake anaamini Young Africans itaendelea kufanya vizuri msimu ujao na hiyo ni kutokana na usajili mzuri ilioufanya msimu huu ameuona kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi anaamini wanao uwezo wa kutetea mataji yote matatu.

Aidha, Mayele amemshukuru Rais wa timu hiyo, Hersi Said kwa sapoti na ushirikiano na ukaribu kwa timu na wachezaji wake ambao umechangia kuwatia moyo na kufikia malengo yao msimu uliopita.

“Rais Hersi amekuwa msaada mkubwa sana kwetu, amekuwa na ukaribu wa hali ya juu kwa timu yake mara kadhaa tumekuwa tukisafiri naye iwe ndani au nje ya nchi, hii imechangia wachezaji kupata hamasa ya kupambana,” amesema Mayele.

Mshambuliaji huyo alijiunga na Young Africans misimu miwili iliyopita na katika kipindi chote ameisaidia timu hiyo kubeba mataji sita, mawili ya Ligi Kuu, Ngao za Jamii mara mbili na makombe ya Shirikisho ‘ASFC’ mara mbili na kucheza Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Pia alibeba tuzo sita ikiwemo Mfungaji Bora wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika na Mfungaji Bora Tanzania Bara pamoja na Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara (MVP).

SOMA NA HII  EHEE...PABLO AVUNJA UKIMYA ISHU YA KUTAKIWA NA ORLANDO PIRATES YA SAUZI...AITAJA SIMBA....

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here