Home Habari za michezo SABABU ZA SIMBA KUACHANA NA KIPA WAO MBRAZILI ZAWEKWA WAZI

SABABU ZA SIMBA KUACHANA NA KIPA WAO MBRAZILI ZAWEKWA WAZI

kipa wa simba

BENCHI la ufundi la Simba lilitarajiwa kukutana usiku wa jana mara baada ya mechi ya mwisho iliyopigwa jioni dhidi ya Batman Petrolspor A.S ili kuanza mchakato mpya wa kusaka kipa mpya, baada ya Mbrazili, Jefferson Luis aliyesajili hivi karibuni kupigwa chini.

Inaelezwa kipa huyo aliyesajiliwa kutoka Resende iliyopo Daraja la Tatu huko Brazili amepata majeraha makubwa na hivyo kupendekeza kusitishiwa mkataba kwani atakuwa nje kwa muda mrefu, hata hivyo maamuzi ya mbadala wake ilitegemea kutolewa baada ya mechi na Batman.

Taarifa kutoka ndani ya kambi ya timu hiyo iliyopo Uturuki ni kwamba kipa huyo alisajiliwa huku akiwa na tatizo la misuli nyuma ya paja jambo lililogundulika kwa muda aliokuwa huko.

“Ni kweli amegundulika na tatizo hilo na anaweza kukaa nje kwa muda mrefu ila bado siwezi kusema moja kwa moja kama mkataba wake utavunjwa au lah! Maana maamuzi hayajafikiwa,” kilisema chanzo hicho, lakini taarifa nyingine zinasema tayari kipa huyo ndio basi tena Msimbazi.

Jefferson aliyetambulishwa Jumapili ya Julai 23 na kupewa mkataba wa miaka miwili alisajiliwa na timu hiyo huku akitajwa ndiye mbadala sahihi wa kipa namba moja wa kikosi hicho, Aishi Manula.

Manula aliumia tangu Aprili mwaka huu kwenye ushindi wa mabao 5-0 katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Ihefu huku akitarajiwa kurejea uwanjani kuanzia Oktoba.

Kipa huyu mwenye umri wa miaka 29, tangu aliposajiliwa na Resende mwaka 2017 muda mwingi alikuwa akitolewa kwa mkopo kwenda timu mbalimbali hadi kufikia hatua ya mwisho alipotua nchini kujiunga na Simba.

Luis ametolewa kwa mkopo kwenye jumla ya timu tano tofauti ambazo alikuwa kwa nusu msimu ama msimu mmoja pekee.

Timu hizo tano ambazo fundi huyu alipelekwa kucheza kwa mkopo ni pamoja na Athletic, Itabaiana, Volta Redonda, SC Aymores na Itabirito FC-MG.

Kwa msimu uliopita akiwa na Resende, kipa huyu amecheza jumla ya mechi 21 katika michuano yote ambapo aliruhusu mabao 35 na akamaliza mechi tatu tu kati ya hizo bila ya nyavu zake kutikisika.

Kuumia kwa kipa huyo kunatoa nafasi nyingine kwa viongozi wa Simba kuingia sokoni ili kusajili mpya kutokana na kutokuwa na imani na Ally Salim aliyekuwa langoni michezo yote ya mwishoni wa msimu.

SOMA NA HII  MANULA ATAKA NAFASI YAKE SIMBA, ISHU IKO HIVI