Home Habari za michezo “KIBURI NA JEURI VIMEMFIKISHA NAVATUS ULAYA….WACHEZAJI WA KIBONGO WAVIVU…”

“KIBURI NA JEURI VIMEMFIKISHA NAVATUS ULAYA….WACHEZAJI WA KIBONGO WAVIVU…”

Habari za Michezo Bongo

EDO KUMWEMBE:


Nilikuwa nasoma mitandaoni. Kama ilivyokuwa wakati ule Mbwana Samatta akienda kutesa sehemu mbalimbali kuanzia TP Mazembe na kwingineko mashabiki walikuwa wanashangaa. Walishangaa sana ni namna gani Mtanzania anaweza kufanya mambo makubwa katika soka.

Na sasa mashabiki wanamshangaa Novatus Dismas. Juzi alitangazwa kuwa mchezaji mpya wa Shakhtar Donetsk ya Ukraine. Atacheza katika Ligi Kuu ya Ukraine, lakini zaidi atacheza katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Shakhtar wamepangwa kundi moja na Barcelona, Porto na Roya Antwerp ya Ubelgiji.

Kwetu ni habari kubwa. Katika mitandao yetu ni habari kubwa. Kwa nchi nyingi za Afrika, hasa zile za Afrika Magharibi hii ni habari ya kawaida tu. Sio tu kwamba ni habari ya kawaida, lakini rafiki zangu Wanigeria au Waghana wasingejua kwamba kuna mchezaji wao amehamia Shakhtar Donetsk akitokea Ubelgiji.

Kwanini? Wana maelfu ya wachezaji Ulaya ambao kila siku wanahama kutoka klabu moja kwenda nyingine. Wana maelfu ya wachezaji wanaotoka mabara mengine kwenda Ulaya kila uchao. Kuna sababu nyingi nyuma yake. Moja inahusu nafasi yao ya Kijiografia na kihistoria.

Sababu nyingine? Ni uthubutu wa wachezaji wao. Nitakukumbusha kitu. Miaka miwili iliyopita nilikwenda katika nchi ya Mauritania katika michuano ya Mataifa ya Afrika chini ya umri wa miaka 20. Hapa ndipo nilipokiona vema kipaji cha Novatus Dismas. Baada ya kumalizika pambano moja dhidi ya Ghana niliona naona wachezaji wa Ghana walivyomzunguka Nova na kukihusudu kipaji chake.

Wengi walimuuliza alikuwa anacheza wapi. Wakati ule alikuwa anacheza Israel. Wao walikuwa wanacheza katika timu mbalimbali za Ulaya. Wengi walikuwa wanashangaa kwanini Nova alikuwa anacheza katika Ligi Kuu ya Israel badala ya kucheza katika Ligi zao kama vile Ufaransa, Ubelgiji, Ujerumani, Italia na kwingineko.

Ilinikumbusha namna ambavyo mwaka 2012 niliongea na Yaya Toure pale Abidjan katika pambano fulani kati ya Ivory Coast dhidi ya Taifa Stars. Aliniuliza Samatta alikuwa anacheza wapi baada ya kukoshwa na kipaji chake. Nilipomwambia kwamba anacheza DR Congo katika klabu ya TP Mazembe aliniambia kwa Kiingereza kilichonyooka kwamba ‘he wastes his time’. Kwamba anapoteza muda wake kucheza Congo na Afrika.

Haijanishangaza sana kuona Novatus anakwenda kucheza katika klabu inayoshiriki Ligi ya Mabingwa kwa sababu Novatus ni ‘jeuri’ halafu ni ‘kiburi’. Kwa wachezaji wetu wengi Watanzania vinahitajika vitu hivi viwili ambavyo baadaye vinakwenda kutengeneza uthubutu. Watu wa Afrika Magharibi wana vitu hivi viwili ambavyo vinakwenda kuwatengenezea uthubutu.

Wachezaji wetu wengi wana vipaji sawa na hawa wachezaji wa Afrika ambao wanatamba Ulaya. Tofauti pekee baina yao na sisi ni ujeuri chanya ambao unakwenda kutengeneza uthubutu. Basi. Hakuna maajabu mengine makubwa ambayo wanayo halafu sisi hatuna.

Nimemtazama sana Nova. Ni msela. Ni msela ambaye ana sura nzuri ya kiume inayovutia, lakini anacheza soka la shoka, ana kipaji, mshindani kutoka moyoni. Sisi tunatengeneza wachezaji wengi ambao wana vipaji lakini sio washindani kutoka moyoni. Tunatengeneza vipaji vipi legelege ndani na nje ya uwanja.

Nova, kama ilivyo kwa Samatta au Simon Msuva sio kwamba wao ni vipaji vya ajabu ambavyo taifa letu limewahi kuvitoa. Hapana. Ila ni wachezaji washindani ambao tumewahi kuwa nao. Ushindani sio ndani ya uwanja tu bali pia nje ya uwanja. Kuna mambo mengi ambayo yanaweza kufanikisha mchezaji kufika juu.

Kwa mfano, huyu Novatus akiwa na Biashara United alionyesha kipaji kikubwa kiasi cha kuchaguliwa kuwa mwanasoka bora chipukizi wa msimu wa ligi yetu. Kule Biashara alikwenda kwa mkopo akitokea Azam. Kwa wakati ule alikuwa bidhaa nzuri kwa Azam wenyewe au kama angeamua kwenda Simba na Yanga. Matokeo yake akakubali kwenda Israel.

Ni wachezaji wachache Tanzania ambao wamekubali kuuepuka ustaa wa Simba na Yanga kwa ajili ya kwenda nje halafu nchi yenyewe ikawa Israel. Nova ni mmojawapo. Huu ni mwanzo wa uthubutu ambao wachezaji wetu huwa wanakosa. Wanapenda kuimbwa majina yao wakipita Kariakoo.

Ndani ya uwanja Nova ni mchezaji wa shoka. Sio kwa sababu ya kipaji, hapana, anapiga kazi na ni mgumu. Mara nyingi nimekuwa nikiandika hapa kwamba tatizo kubwa la wachezaji wetu ni kutegemea zaidi vipaji zaidi kuliko kuwa wagumu na kufanya kazi nzito uwanjani. Wachezaji wetu wengi ni legelege.

Mtazame beki wa kulia wa Yanga. Yao Yao. Anajua mpira, sawa, lakini ni mtu wa shoka hasa. Anatumia nguvu, ana stamina, ana pumzi. Soka sio mchezo rahisi kama ambavyo tumekuwa tunaaminishwa na wachezaji wetu wenye vipaji. Ndio maana tumeendelea kuwaamini kina Mzamiru Yassin katika timu zetu huku wachezaji wenye vipaji wakiangukia timu za kawaida kila siku.

Sijamshangaa Novatus kuendelea kupata timu kubwa huko Ulaya kwa sababu anasimama katikati yao. Ana kipaji na anapiga soka la shoka. Mzungu lazima akupende. Wachezaji wengi wa Afrika Magharibi wanajaa Ulaya kwa sababu hiyo. Na wapo wachezaji wa kawaida kabisa wa Afrika wanaotamba Ulaya kwa sababu tu ni wachezaji wa shoka.

Nawafahamu maelfu ya wachezaji wa Kitanzania ambao wangeweza kutamba Ulaya kama wangekuwa tu na uthubutu wa kupambana ndani na nje ya uwanja. Ni kama tu wangeweza kucheza soka la shoka uwanjani ambalo lingeambatana na vipaji vyao kisha nje ya uwanja wakakubali kuishi mazingira ya ugenini na kusahau maisha ya nyumbani.

Kitu kingine ambacho inawezekana hatuna lakini ubora wetu unaweza kutusaidia ni msaada kutoka kwa mawakala wa nje. Hawa kina Samatta na Novatus wanaendelea zaidi kutokana na kuanza kuwa na ushirikiano na mawakala wa nje. Hili lipo ndani ya uwezo wetu kama tutaendeleleza ubora wetu wa kuhimili maisha ndani na nje ya uwanja.

Kikubwa kinachotakiwa ni uthubutu. Kichwani nina orodha ndefu ya mastaa wa Tanzania wa kizazi hiki ambao wangeweza kucheza nje kwa mafanikio kama ilivyo kwa Novatus au Samatta. Tofauti pekee iliyopo ni uthubutu tu. Wengine wameamua kutimiza ndoto zao kwa Simba na Yanga.

Hakuna ambacho Novatus amenishangaza. Anachofanya ni kitu cha kawaida tu kwa watu wa Afrika Magharibi. Huku tunaona kitu cha ajabu kwa sababu amezaliwa katika taifa lenye watu wazembe ambao wanaamini mafanikio makubwa ni kucheza Simba na Yanga.

Makala haya yaliandikwa kwanza na mwandishi kwenye wavuti la MwanaSpoti
SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA PILI ORLANDO vs SIMBA....CAF YAPANGA WAAMUZI KUTOKA NCHI KARIBU NA AFRIKA KUSINI..