BAADA ya kufanikiwa kuendeleza soka la vijana , wanawake na timu kubwa kuwa sehemu ya klabu kubwa Barani Afrika, uongozi wa Klabu ya Simba umezindua programu maalumu ya kuibua vipaji vya watoto mashuleni.
Hatua hiyo ni baada ya uongozi wa klabu hiyo kuja na Programu maalumu kutoka kwenye jopo la benchi la ufundi wa timu za vijana kutembelea shule zote Tanzania kwa kuipa jina la (Back to School).
Mtendaji Mkuu wa Simba, Iman Kajula alisema wameamua kurudi mashuleni kwa makocha wa timu za vijana kutembelea katika shule siku za michezo ili kuwaweka karibu watoto na Simba.
Alisema wanatambua katika shule kuna vipaji na wanaenda huko kuibua wachezaji wapya lakini pia kuwaandaa mashabiki wa Simba wa baadae kupitia programu hiyo.
“Programu hiyo itakuwa endelevu kutembelea shule zote hapa nchini , huku makocha wetu wa vijana kufanya programu zao, lakini pia siku za mechi watoto katika shule mbalimbali watapewa nafasi ya kuja uwanjani kusapoti timu yao,” alisema Kajula.
Alisema Simba walizungumza na wabia wao (taasisi za mabank) kuhakikisha wanakuwa na Akaunti za watoto ili wanapofungua wanakuwa sehemu ya mashabiki.
“Wabia wetu wamekubali hilo na sasa mzazi anapokwenda kumfungulia Akaunti anakuwa sehemu ya uanachama wa Simba, tumeenda mashuleni kwa sababu elimu na michezo inawafanya watoto wetu kuwa na utimamu wa mwili (Afya ya akili) na kujenga ushirikiano wenyewe kwa wenyewe na nidhamu,” alisema Kajula.
Naye Meneja wa programu za vijana wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema baada ya kufanikiwa kupata timu ya vijana kuanzia U-17, 18, 19 na 20 sasa wanaenda katika shule za msingi na kindagate kwa ajili ya kuibua vipaji vya watoto.
Alisema miaka ya sasa watoto wamepoteza hamu ya kucheza mpira wa miguu kwa sababu ya changamoto za viwanja kuwa duni, sasa Simba wameamua kurudisha mapenzi ya kupenda kucheza na kuibua vipaji.
“Hii haitakuwa faida kwa Simba pekee bali ni kwa Taifa letu, tunapotengeneza programu hii inasaidia kuibua vipaji kuanzia chini na baadae itakuwa rahisi kupata wachezaji wazuri na kuleta manufaa kwa timu zetu za taifa za kike na kiume,” alisema Rweyemamu.
SOMA NA HII YANGA WASHINDWE WENYEWE TU LEO...KUMBE KIPA WA MAZEMBE KAGOMA KUJA TZ...ISHU IKO HIVI...