Home Azam FC BANGALA AMKINGIA KIFUA FEI TOTO

BANGALA AMKINGIA KIFUA FEI TOTO

Kiungo wa Azam Yannick Bangala amefurahishwa na kiwango cha Feisal Salum ‘Fei Toto’ akisema jamaa ameanza kuwa mtamu huku akimpa ushauri juu ya mashabiki wanaomzomea kwenye mechi zao.

Fei alionyesha kiwango cha juu juzi wakati timu yake ya Azam ilipopoteza kwa kuchapwa mabao 3-2 na Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya NBC.

Akizungumza na Mwanaspoti Bangala ambaye alikuwa akicheza pamoja na Fei Toto wakati wakiwa Yanga na sasa wapo wote Azam alisema kiungo huyo ameanza kurudi kwenye kiwango chake lakini anatakiwa kuwapuuza mashabiki wanaomzomea.

Bangala raia wa Jamhuri ya Congo alisema Fei Toto anatakiwa kuendelea kupambana uwanjani bila kuyaingiza kichwani makelele ya mashabiki hao kama ambavyo alifanya mchezo uliopita walipokutana na Yanga.

Alisema endapo Fei Toto ataendeleza kiwango hiki alichonacho sasa atawanyamazisha wote ambao wamekuwa wanaomzomea.

“Ukiangalia alivyofika hapa Azam na alivyo sasa hasa alipocheza mechi dhidi ya Yanga utaona jinsi anavyoimarika, alicheza kwa kiwango kikubwa ni kwa kuwa tulipoteza mechi ile lakini ujumbe umefika,”alisema Bangala.

“Najua anakutana na ugumu kwa watu wanaomzomea mimi namshauri awapuuze asiweke makelele yao kichwani kwake akiendelea na kiwango hiki atawafanya wanyamaze,”

Fei Toto tangu ahame Yanga mashabiki wa timu hiyo wamekuwa wakimuandama kwa kumzomea kila mchezo, lakini ameonekana kuwa makini na kazi yake zaidi.

Kiungo huyo ni mmoja kati ya wale wenye mabao mengi kwenye Ligi Kuu Bara akiwa ameshapachika mabao manne hadi sasa.

SOMA NA HII  RAIS AL-NASSIR AJUTA KUMSAJILI RONALDO..."NIMEUZIWA MBUZI KWENYE GUNIA