Home Habari za michezo GAMONDI AWEKA WAZI SIRI HII YA YANGA

GAMONDI AWEKA WAZI SIRI HII YA YANGA

Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Miguel Angel Gamondi amesema siri ya wao kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ni ushirikiano mzuri Kati ya uongozi, Benchi Ufundi na Wachezaji.

Young Africans juzi Jumamosi (Septemba 30) iliibuka na ushindi wa bao 1-0, dhidi ya Al Merreikh ya Sudan na kuifanya itinge hatua hiyo kwa matokeo ya jumla ya mabao 3-0.

Kocha huyo kutoka nchini Argentina ambaye ameweka Rekodi ya kuiridisha Young Africans hatua ya Makundi baada ya miaka 25, amesema, amekuwa akipata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wa timu hiyo wakiongozwa na Rais Hersi Said lakini pia wasaidizi wake na wachezaji wa timu hiyo.

“Niseme tu tangu nimefika hapa nimekuwa na ushirikiano kutoka kwa viongozi, wasaidizi wangu na wachezaji wote. Bila ya kuwa na umoja hauwezi kupata mafanikio kwenye mchezo wa soka,” amesema Gamondi.

Aidha, akizungumzia mchezo ulivyokuwa amesema walicheza vizuri kwa kumiliki mpira na kutengeneza nafasi za kutosha za kufunga lakini pia kubadili mifumo ya uchezaji na kila kitu kilikuwa upande wao.

“Baada ya kuwafunga mabao 2-0 ugenini wapinzani wetu ni kama hawakuwa na cha kupoteza kwenye mchezo wa juzi Jumamosi na kucheza na timu ya namna hii sio kitu rahisi, tuliamua kuwashambulia hata kama tulikuwa na mtaji wa ushindi kwenye mchezo wa kwanza,” amesema Gamondi.

Amesema anajua hatua inayofuata ni ngumu lakini wamejipanga kwenda kushindana na siyo kushiriki lengo ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Al Merreikh, Osama Nabih amekiri timu yake kuzidiwa huku akiwapongeza Young Africans kwa ubora waliouonesha katika mechi zote mbili.

SOMA NA HII  KAKOLANYA ALAMBA SHAVU SIMBA