Home Habari za michezo ACHANA NA KIPIGO CHA YANGA…HUU HAPA UBAYA WA SIKU YA J/NNE KWA...

ACHANA NA KIPIGO CHA YANGA…HUU HAPA UBAYA WA SIKU YA J/NNE KWA MAKOCHA WA SIMBA….

Novemba 7, 2023, ilikuwa Jumanne ya wiki iliyopta, Klabu ya Simba ilitoa taarifa ya kuvunja mkataba wa Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, ikiwa ni baada ya kutoka kufungwa 5-1 na Yanga.

Kipigo hicho Simba walikipata Novemba 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, siku mbili mbele, ndipo uamuzi huo mgumu ukafanyika.

Kuondoka kwa Robertinho, kunatukumbusha namna watangulizi wake watatu walivyoondolewa kikosini hapo ambapo wote ilikuwa siku ya Jumanne, lakini tarehe tofauti.

ZORAN MAKI

Alijiunga na Simba Juni 28, 2022, na kupewa mkataba wa mwaka mmoja ukiwa na masharti ya kurudisha makombe yote ambayo Simba iliyapoteza msimu wa 2021/22 ambayo ni Kombe la Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam Sports (FA), taji la Ngao ya Jamii na kuifikisha Simba nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Jumamosi ya Agosti 13, 2022, alianza vibaya safari yake Simba baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii.

Kisha baada ya ushindi katika michezo miwili ya Ligi Kuu, Jumanne ya Agosti 15, 2022, aliondolewa rasmi. Kumbuka Maki Alitangazwa Jumanne na ameondoka Jumanne.

Kocha huyo aliondoka Simba baada ya kuhudumu kwa muda wa takribani siku 57.

DIDIER GOMES

Alitangazwa rasmi kuwa kocha wa Simba Januari 24, 2021, akichukua nafasi ya Mbelgiji, Sven Vandenbroeck ambaye alijiunga na FAR Rabat ya Morocco.

Gomes aliipokea Simba ambayo ilikuwa imefanikiwa kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kufanya kazi kubwa ya kuifikisha robo fainali ya mashindano hayo, kutetea ubingwa wa Kombe la Ligi Kuu Bara na lile la Shirikisho la Azam Sports bila kusahau ubingwa wa mashindano maalum ya Simba Super Cup.

Baada ya mafanikio makubwa ya msimu wa 2020/21 msimu wa 2021/22 aliuanza vibaya kwa kupoteza Ngao ya Jamii baada ya kufungwa na Yanga bao 1-0 na kuondolewa hatua ya pili Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana. Jumanne ya Oktoba 26, 2021 ilikuwa mwisho wake ndani ya Simba.

PABLO FRANCO

Uongozi wa Simba Jumanne ya Mei 31, 2022, kupitia mitandao yao rasmi ya kijamii uliweka wazi kuwa umefikia makubaliano ya pande mbili na aliyekuwa kocha wao mkuu, Pablo pamoja na aliyekuwa kocha wao wa viungo, Daniel De Castro Reyes ya kuvunja mikataba ya utumishi wao klabuni hapo.

Pamoja na kuvunja mikataba hiyo, uongozi wa Simba uliwashukuru makocha hao kwa mchango wao mkubwa wa kuwasaidia kushinda Kombe la Mapinduzi na kuifikisha timu hiyo hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku pia ukiwatakia kila la kheri katika majukumu yao mapya

Pablo alihudumu ndani ya Simba kwa kipindi cha miezi mitano tu, ambapo aliiongoza timu hiyo kwenye michezo 40 ya mashindano yote, mafanikio yake makubwa yalikuwa kushinda Kombe la Mapinduzi na kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

YANGA WANAHUSIKA PIA

Ukiacha sababu nyingine za kiutawala ambazo zimepelekea makocha hao watatu wa Simba kufukuzwa, tathimini ya karibu inaonesha kuwa Yanga kwa kiasi fulani wamechangia kufukuzwa kwa makocha hao kwani wote kwa nyakati tofauti walianza kupitia katika nyakati ngumu baada ya kupoteza michezo yao mbele ya Yanga.

Gomes alipoteza mbele ya Yanga kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii Septemba 25, 2021 na kufukuzwa Oktoba 26, 2021. Pablo yeye alijikuta akipoteza kibarua chake ndani ya Simba mara baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Yanga kwenye mchezo wa nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam, Mei 28, 2022.

Zoran naye akionja joto ya kupoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Yanga katika Ngao ya Jamii, huku Robertinho akipoteza kwa mabao 5-1 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga.

SOMA NA HII  UJIO WA ATEBA SIMBA...WAWILI ROHO JUU...FREDY NAE MMMH