Home Habari za michezo KUMBE UJANJA WANAOTAMBA NAO YANGA UKO HAPA

KUMBE UJANJA WANAOTAMBA NAO YANGA UKO HAPA

Geita vs Yanga

Yanga inavuma kila sehemu ikiwa ya moto uwanjani ikiendeleza kasi ya kulitaka taji la tatu mfululizo la Ligi Kuu Bara, lakini kuna mambo matatu mazito yanawapa mabingwa hao jeuri mbele ya wapinzani wao.

Ikiwa imevuka wiki ngumu kwa kushinda mechi nne za ligi dhidi ya Azam FC (3-2), kuifumua Singida Biga Stars (2-0), Simba (5-1 ) na Coastal Union (1-0) matokeo yaliyothibitisha bado ipo kwenye ubora uleule wa msimu uliopita.

Hata hivyo, imebainika janja yote ya wababe hao ipo kwa kocha wa viungo wa viwango, Taibi Lagrouni anayetajwa kama mtu wa kwanza anyechomoza mbele ya ubabe wa Yanga kwenye maandalizi ya awali ya msimu huu timu hiyo imeonekana kuwa fiti pengine kuliko timu yoyote.

Yanga haonekani kukata pumzi kama timu nyingine ikiwa na uwezo wa kucheza kwa ubora bila kuchoka muda wote wa dakika 90.

Lagrouni ni kocha mkongwe wa mazoezi ya viungo akiwa amewahi kuhudumu RS Berkane ya Morocco ilipochukua kombe la Shirikisho Afrika chini ya Kocha Florent Ibenge.

Master Gamondi yumo

Kando ya Lagrouni kuna bosi wake, Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ambaye mbinu zake uwanjani zimeiongezea Yanga ubora mkubwa.

Kwenye mechi nane za ligi ambazo Yanga imeshacheza mpaka sasa licha ya kupoteza mchezo mmoja lakini imekuwa ikikaba kwa nguvu na kushambulia kwa idadi kubwa ya watu kwenye eneo la mwisho la wapinzani.

Nidhamu hii ikitumia mfumo sawa na ule wa aliyekuwa akiutumia kocha aliyetangulia Nasreddine Nabi wa 4-2-3-1 Yanga imekuwa ikitengeneza nafasi za kutosha za kufunga ikiwa ndio timu iliyofunga mabao mengi 26 ikiwa ndio vinara wa mabao mengi ikifautiwa na Azam yenye 19 huku Simba ikiwa na mabao 18.

Ubora wa Gamondi na Lagrouni umewafanya makocha wa timu pinzani kutawaliwa na changamoto na tayari Simba imeshawatimua makocha wake, Roberto Oliveira ‘Robertinho na wasaidizi wake Ounane Selami na kocha wa viungo, Mrundi Corneille Hategekimana.

Janja nyingine ni hii

Kwenye kambi ya mazoezi ya Yanga kuna kazi kubwa ya mazoezi makali yanayofanywa na wachezaji, lakini siri kubwa ni uongozi wa timu hiyo chini ya Rais wa klabu hiyo, Injinia Hersi Said na mfadhili, Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ aliyemwaga vifaa vya kisasa vinavyokaribia Sh 1.4 bilioni ambavyo vimekuwa ni mtaji mkubwa wa makocha wao kuwafanya wachezaji wao kuwa fiti. Vifaa hivyo vinaelezwa ndivyo vinavyowarahisishia kazi makocha pamoja na wachezaji kuibeba timu hiyo ndani na anga za kimataifa.

Msikie Gamondi

Kocha Gamondi alisema: “Tunafanya mazoezi makali sana, kwenye mazoezi yetu hutashangai kuona mafanikio ambayo tunayapata, nafurahi kuona tuna wachezaji ambao wametambua umuhimu wa kujituma.”

SOMA NA HII  BAADA YA YANGA KUPOTEANA ZNZ...SENZO AIBUKA HADHARANI NA KUIMWAGIA 'HEKO' SIMBA..