Home Habari za michezo MASTAA SIMBA WAMTEGA ROBERTINHO

MASTAA SIMBA WAMTEGA ROBERTINHO

Habari za Simba

Takwimu za ufungaji za Moses Phiri na Jean Baleke katika Ligi Kuu msimu huu wa 2023/24, zinaweza kumuweka mtegoni kocha wa Simba Roberto Oliveira katika mchezo dhidi ya Young Africans, utakaounguruma Jumapili (Novemba 05) katika kuamua nani aanze kikosini ikiwa atatumia mfumo wa kuanza na mshambuliaji mmoja wa kati kama ambavyo amekuwa akifanya mara kwa mara.

Katika mechi sita zilizopita za Ligi Kuu ambazo Simba imecheza dhidi ya Mtibwa Sugar, Dodoma Jiji, Coastal Union, Tanzania Prisons, Singida Big Stars na Ihefu, nyota hao wawili wameifungia mabao tisa ambayo ni sawa na 56.25% ya mabao yote l8 ambayo timu hiyo imefunga hadi sasa.

Wakati wakijiandaa kuikabili Young Africans, Baleke anabebwa na takwimu za kuwa mchezaji aliyefunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika kikosi cha Simba msimu huu ambapo hadi sasa amefumania nyavu mara sita kwenye ligi, sawa na Stephane Aziz Ki wa Young Africans na hivyo kuwa vinara wa ufungaji kwenye ligi.

Lakini nyota huyo kutoka DR Congo anaangushwa na takwimu za kutumia wastani wa muda mrefu zaidi kufunga bao kulingana na nafasi anayopewa kikosini.

Baleke ameichezea Simba SC kwa dakika 415 kwenye ligi na kwa makadirio amekuwa akifunga bao moja kila baada ya dakika 69 za mchezo. Phiri, yeye anabebwa na takwimu za kuhitaji dakika chache zaidi uwanjani ili afunge bao.

Phiri ameichezea Simba SC kwa dakika 157 tu ambapo amefunga mabao matatu jambo linalomfanya awe na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 52.3. Namba ya mabao aliyofunga ndani ya muda huo mfupi aliocheza ndio kitu kinachomuwekea kauzibe Phiri mbele ya Baleke.

Mshambuliaji mwingine wa kati wa Simba SC ni nahodha John Bocco ambaye amecheza dakika 129 tu, akifunga bao moja na amekuwa na makadirio ya kufunga bao katika kila dakika 129.

Kocha Aldof Rishard alisema; “Kocha anaangalia mchezaji anampa nini na kwa wakati gani, Phiri, Baleke na John Bocco wako vizuri kutokana na matumizi ya kocha.

“Kwa mfano Bocco ukimpanga basi lazima uangalie mpinzani wako yukoje, kama pale Young Africans akipangwa Bakari Mwamnyeto kocha anaweza kumtumia Bocco kwa vile anaiweza mipira ya juu, anakaa na mpira, ni mmaliziaji mzuri, wengine ni watalaamu wa mipira ya chini na mipira mgawanyo,” amesema na kuongeza;

“Phiri na Baleke huenda kocha anajua hawa ndiyo wachezaji wangu wa akiba wanaojua kuusoma mchezo na kubalidilisha mchezo na matokeo, lakini kwa wachezaji hao pia wanapokaa benchi wanapaswa kuambiwa sababu za kuwaweka benchi.”

Naye mshambuliaji wa zamani wa Simba SC na Taifa Stars, Emannuel Galbriel alisema: “Kama Simba SC wanataka matokeo mazuri basi ni vyema kocha akawaanzisha Phiri na Baleke, ni wachezaji wanaompa matokeo mazuri na ukiangalia wamefanya vizuri kwenye mechi walizocheza.

“Kibu Denis anampa majukumu ambayo hayawezi kwa kumchezesha namba tisa, anamnyima uhuru wa kutembea, Bocco amwache kwanza benchi aingie timu ikipata matokeo mazuri na hawana cha kupoteza.

“Mechi mbili za mwisho za Simba zimeleta mwanga kuelekea dabi ingawa watani zao wapo vizuri, lakini kama kocha ataamua kutumia mshambuliajia mmoja basi tumwachie kazi yake na uamuzi wake huenda ukawa sahihi, ila kuimaliza Young Africans ni kuwatumia Baleke na Phiri kwa pamoja.

SOMA NA HII  MTIBWA SUGAR YAPATA PAKUTOKEA LEO