Home Habari za michezo MASTAA YANGA WAIPIGA MKWARA MZITO ALAHLY

MASTAA YANGA WAIPIGA MKWARA MZITO ALAHLY

Beki wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Dickson Job amesema kupoteza kwao dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria haina maana kwamba wametoka kwenye mashindano.

Young Africans ilikubali kichapo cha 3-0 ugenini nchini Algeria katika mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza wa Kundi D, uliopigwa Ijumaa (Novemba 24).

Job ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Young Africans katika mchezo huo, amesema wanajipanga kucheza dhidi ya Al Ahly ambayo ni timu bora Afrika na wanawaheshimu, lakini hawawezi kuwaogopa kwani mchezo ni dakika 90 na wachezaji wa pande zote wana uwezo mkubwa wa kucheza.

“Tutaongeza umakini wa kupata matokeo lakini pia kuhakikisha sisi kama mabeki hatųwapi nafasi wapinzani kufunga,” amesema Job.

Ameongeza kuwa haitakuwa rahisi kwao kupoteza mara mbili hasa uwanja wa nyumbani.

Naye Beki wa kushoto wa Young Africans Joyce Lomalisa Mutambala, amesema kwenye kundi lao kila aliyecheza nyumbani kwake ameshinda na wao wanarudi nyumbani kutengeneza ushindi wao kwanza.

Ameongeza kuwa ana uzoefu mkubwa kwenye mechi kama hizi amecheza dhidi ya Al Ahly mara nyingi anajua wanahesabu gani wakiwa wanacheza ugenini atawashauri wenzake kwenye maandalizi yao na hata kwenye mechi.

Lomalisa amesema kwenye maandalizi yao yaliyoanza jana Jumatatu (Novemba 27) watasikiliza kwanza makocha wao wanakuja na mipango gani dhidi ya Al Ahly lakini mashabiki wao wasivunjike moyo waje uwanjani

“Hata msimu uliopita wapo waliosema tutapoteza mbele ya TP Mazembe lakini tulishinda mechi zote hivyo tutawashangaza,” amesema

Baada ya michezo ya Mzunguuko wa kwanza, Msimamo wa Kundi D unaonesha Al Ahly wanaongoza msimamo wakiwa na alama tatu sawa na CR Belouizdad, huku Young Africans na Medeama SC wakiburuza mkia.

SOMA NA HII  YANGA WAJA NA JAMBO HILI JIPYA KWENYE MARUDIANO NA AL MAREKH