Home Habari za michezo RAIS WA YANGA AANZA MIKAKATI, BAADA YA GAMONDI KUMPA LIST HII

RAIS WA YANGA AANZA MIKAKATI, BAADA YA GAMONDI KUMPA LIST HII

Habari za Yanga

Wakati mashabiki na wapenzi wa Yanga wakiendelea kutamba mtaani kutokana na kiwango bora kilichoonyeshwa na timu hiyo iliyoshinda mechi nane kati ya tisa za Ligi Kuu na kuwa vinara wa kutupia mipira kambani, kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi kumbe mawazo yake yapo tofauti kabisa.

Kocha huyo amekiangalia kikosi kilicho kwa sasa na nyota waliopo kisha akaandika ripoti na kuikabidhi kwa viongozi akitaka aletewe winga teleza mmoja na straika anayejua kufunga mabao kupitia dirisha dogo litakalofunguliwa mwezi ujao ili amalize kazi mapema.

Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 24 na mabao 26, kwa sasa inajiandaa kwa ajili ya mechi sita za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikitarajiwa kuanza ugenini dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria, Novemba 24 kabla ya kuikaribisha Al Ahly ya Misri moja baadae jijini Dar es Salaam.

Lakini pamoja na kuwa kwenye maandalizi kwa ajili ya mechi hizo dhidi ya klabu kutoka Afrika Kaskazini, kocha Gamondi tayari ameshawasilisha ripoti ya benchi la ufundi kwa mabosi wa klabu hiyo, ambayo inaelezwa imeanza kufanyiwa kabla hata kabla dirisha la usajili halijafunguliwa Desemba 16.

Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni ripoti ya Gamondi ambayo imeshaanza kufanyiwa kazi na mabosi wawili wa juu wa klabu hiyo, inataka mashine mbili zenye ubora kuzidi wachezaji waliopo sasa kikosini

Ripoti hiyo imeonyesha mchezajui wa kwanza anayetakiwa ni mshambuliaji mwenye ubora mkubwa wa kufunga atakayekuja kuongeza makali ya eneo la ushambuliaji la mabingwa hao, kwani kwa sasa hajaridishwa na kazi, licha ya timu hiyo kuongoza kwa kufunga mabao mengi katika Ligi Kuu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kuna uwezekano mkubwa straika wa sasa Hafiz Konkoni kupewa mkono wa kwaheri endapo Yanga itapata nyota wanayemfukuzia kwa sasa ambaye hata hivyo jina lake limefanywa siri.

Yanga inataka kuachana na Hafiz kutokana na mshambuliaji huyo Mghana kushindwa kukata kiu ya benchi la ufundi la timu hiyo.

Gamondi ametaja pia kuhitaji winga mwenye kasi na kujua kupangua ukuta ambaye naye akitakiwa kuwazidi mawinga wote waliopo kikosini akiwamo Mahlatse Makudubela ‘Skudu’, Maxi Nzengeli, Jesus Moloko na Denis Nkane.

Baada ya kupokea ripoti hiyo, Mwanaspoti linafahamu kwamba tayari Rais wa Yanga Injinia Hersi Said yuko msituni kusaka watu wao wawili ambao klabu hiyo inataka kuwaingiza kwenye dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Desemba mwaka huu. Inaelezwa kuna majina ya nyota wapya kama watatu, lakini mchujo unfanywa kabla ya jina moja kupelekwa kwa Gamondi ili kuamua.

MSIKIE KOCHA

Akizungumzia mahitaji hayo Gamondi alisema tayari ameshawakabidhi anachohitaji mabosi na sasa akili yake inaanza kufikiria mechi za makundi watakapoanzia ugenini dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.

“Viongozi wangu wanajua tayari kipi kinahitajika kwa ajili ya timu nimewapa nafasi ya kuifanyia kazi lakini tunahitaji watu wa kuja kutuongezea ubora kwenye mechi hizi ngumu,”alisema Gamondi ambaye ndani ya muda mfupi tu falsafa zake zimeanza kutema cheche akiwa na Yanga.

“Unapoingia kwenye maboresho Kuna mambo mengi ya kutakiwa kuzingatia kwanza ni suala la bajeti ya klabu lakini lingine kubwa ni wapi mtapata mtu au watu mnaowahitaji.”

SOMA NA HII  YANGA YAGONGANA NA AZAM FC ZAKUTANA KWA KIPA WA KAGERA SUGAR KUSAKA SAINI YAKE