Home Uncategorized SASA WAKATI WA KUONA TOFAUTI YA AJIBU GIRLFRIEND NA AJIBU HUSBAND

SASA WAKATI WA KUONA TOFAUTI YA AJIBU GIRLFRIEND NA AJIBU HUSBAND

NA SALEH ALLY
BAADA ya picha za video kusambaa mtandaoni zikimuonyesha Ibrahim Ajibu Migomba akiwa katika mazoezi ya gym, mjadala ukazuka kama ataweza kuvumilia kutokana na kuwa na sifa ya uvivu.


Ajibu yuko Afrika Kusini ambako timu yake ya zamani na sasa mpya ya Simba, imeweka kambi Simba kujiandaa na msimu mpya wa 2019/20.


Kiungo huyo mshambuliaji, ni kati ya wachezaji walio nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kambi hiyo na hali inaonyesha kuwa ni kambi bora kabisa, inastahili kwa timu yenye malengo.


Mjadala wa Ajibu umeendana na maneno mawili anayopewa kila mara, moja ni kuwa ana uwezo sana katika kucheza soka. Pili, kwamba ana tatizo hasa kuhusiana na uvivu au kutokuwa msikivu au kijana asiyejituma.


Wakati anaondoka Simba kwenda Yanga, kilichoelezwa ni hichohicho kwamba ni mchezaji asiyejituma na badala ya kutumia kipaji chake kuwa msaada, akageuka mvuto kurudi nyuma. Hivyo akaonekana hana msaada na huku Yanga wakionekana wana mashamsham, Simba wakamuachia akaondoka kwa ulaini kabisa.


Kipindi ambacho Ajibu alikuwa anaondoka kwenda kujiunga na Yanga, Simba ambao walimkuza katika timu yao ya vijana, wala hawakuonekana kutikisika. Mwisho yakatokea mambo mawili, Simba kufanya vizuri zaidi bila ya Ajibu, lakini Ajibu akafanya vizuri kwa muda kabla ya mwisho kuonekana kama alijua anaondoka Yanga, akapunguza kasi na ubora ukaporomoka.


Kumbuka Kocha Mwinyi Zahera alilazimika kumteua kuwa nahodha, akimvua mkongwe Kelvin Yondani. Hali ilionyesha hivi, Zahera ni mwerevu, alijua uwezo wa Ajibu na akajua mhusika hakuwa akiutumia wote, akipewa jukumu la nahodha, ataingia hofu ya kuwaangusha wenzake na kujituma zaidi.


Zahera alifanikiwa nusu, lakini baadaye baada ya Ajibu kuonekana amejua anakwenda Simba, akawa tena hana hofu wala sababu ya kutumia nguvu badala yake kusubiri kwa hamu siku yake ya kutambulishwa rasmi kwamba anarejea “nyumbani.”


Simba ndio waliokuwa wamechukua uamuzi wa kumuacha Ajibu, akaondoka kwenda Yanga. Safari hii Yanga, nao wakasema maneno yanayofanana na Simba kabisa. Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Frederick Mwakalebeba alisema wanamsubiri Ajibu kwa kuwa wanao mkataba wake, akiona inafaa wanamkaribisha mezani, akiona haiwezekani na anataka kwenda, wanamtakia kila la kheri.


Kuna jambo kubwa la kujifunza hapa, kwamba Ajibu mwenye kipaji kikubwa na mifano ipo lakini wakati wake wa kuondoka, hakuna anayeshituka, hakuna anayempigania abaki. Jiulize, huwa anachosha mwishoni au anachoka mwishoni!


Kwamba si mchezaji ambaye anaweza kumaliza na kasi aliyoanza nayo au si mtengeneza mwendo mnyooko? Alivyoanza Simba, akamaliza taratibu mwisho wakaona aende. Yanga hali kadhalika akafanya hivyohivyo, sasa amerudi tena Simba.


Msimu uliopita aliifungia Yanga mabao sita, lakini akatoa asisti zilizozaa mabao 17. Hili si jambo dogo na huenda hata wachezaji hao wageni wanaosajiliwa nchini ni vigumu kufanya jambo hilo.


Asisti 17 au kupika idadi hiyo ya mabao, ni mtaji mkubwa. Ajabu kabisa, neno “angekuwa anajitambua”, linaendelea kumzunguka. Kwa maana hiyo Ajibu alikuwa na uwezo wa kufunga mabao zaidi na asisti zaidi.


Sasa tujiulize, karudi Simba, ni kweli amebadilika? Au ataanza kwa mbwembwe mwanzoni kwa kuwa tayari amekuwa “mgeni” tena, halafu akizoea kama kawaida atamaliza taratibu tena na mwisho Simba wataona hata akienda Yanga tena poa tu, naye ataondoka zake?
Majibu ya mengi ambayo nimeyauliza anayo Ajibu mwenyewe, safari hii ana nafasi ya kutuonyesha kwa kuwa yule aliyeondoka Simba kwenda Yanga anatofautiana mambo mengi sana na huyu.


Mfano, umri tayari ni tofauti, wakati huo anaondoka Simba alikuwa boyfriend (mpenzi) wa mtu, leo ni husband (mume) wa mtu. Unajua kuna tofauti anavyofikiria mume wa mtu na mpenzi wa mtu na ikitokea mume akafikiria kama mpenzi tu, basi ujue kuna tatizo.


Lazima Ajibu atakuwa anaangalia mbali zaidi kwa maana wakati akiondoka Simba pia alikuwa mvulana, sasa ni mwanaume baba kwa kuwa tayari ana mtoto (Mungu amkuzie). Hivyo unaelewa kuwa majukumu yameongezeka na siku zinavyosonga yanazidi kuwa mengi zaidi maana mtoto anakua na huenda familia ikakua zaidi.


Kile ambacho kimekuwa kinasubiriwa na watu wengi, mfano Ajibu kujitambua na kujituma. Ajibu kusimama na kuutumia uwezo wake ambao watathmini wamekuwa wakiona hafanyi hivyo na hili lina ukweli, basi ndio umefika.


Uthibitisho wa kwamba alikuwa na upungufu, Simba na Yanga ndio waliothibitisha na hasa wakati wa kuondoka. Simba wameamua kumuamini tena na yeye kama binadamu yoyote, ana kila sababu ya kulionyesha hili ingawa wakati wa kujirekebisha huwa kuna mawili, kuamka au kuanguka milele.


Ajibu atachagua, ajirekebishe na kusimama na ikiwezekana baadaye kuwa gumzo hasa. Au aanguke milele kwa kuwa wako wengi wenye kipaji kama chake, leo wanaishi kwa tabu sana, wakilalamika kuonewa au kutotendewa haki lakini uhalisia, wao ndio walikuwa chanzo na leo maumivu yanaendelea kuwaandama.
SOMA NA HII  PAPY TSHISHIMBI ABAKIZA SIKU MBILI NDANI YA YANGA, VIONGOZI WASIMULIA NAMNA WANAVYOPAMBANA