Home Habari za michezo SOKA LA BONGO LIMEENDELEA KUPASUA ANGA HUKO CAF UNAAMBIWA NAMBA HAZIDANGANYI

SOKA LA BONGO LIMEENDELEA KUPASUA ANGA HUKO CAF UNAAMBIWA NAMBA HAZIDANGANYI

Klabu za Tanzania zimeonekana kujitutumua katika mashindano ya klabu Afrika katika kipindi cha miaka 10 iliyopita kuanzia 2013 hadi 2023 kulinganisha na hapo nyuma ambapo zilikuwa wasindikizaji.

Hapana shaka mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwekezaji ambao klabu hizo zimekuwa nao ambao umezifanya ziwe na wachezaji wazuri na ziweze kumudu gharama za ushiriki wa mashindano hayo.

Ni katika kipindi cha miaka hiyo 10, tumeshuhudia klabu tatu tofauti za Tanzania zikitinga hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika ambazo ni Simba, Yanga na Namungo.

Namungo ilikomea hapo, Simba katika nyakati tofauti ikifika hadi robo fainali huku Yanga ikifanikiwa kuingia hadi hatua ya fainali ambayo ni ya juu zaidi kwenye mashindano ya Klabu Afrika.

Makala hii inatoa tathmini ya namna namba zinavyoweza kutoa majibu juu ya ushiriki wa klabu za Tanzania kwenye mashindano ya klabu Afrika.

Ubabe wa namba 6 Simba

Tangu Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) lianzishe hatua ya makundi kwenye mashindano yake ya klabu mwaka 1998, Simba ndio timu ya Tanzania iliyoshiriki mara nyingi zaidi hatua ya makundi kwenye mashindano ya Afrika ikifanya hivyo katika awamu sita ambazo ni 2003, 2018/2019, 2020/2021, 2021/2022, 2022/2023 na msimu huu wa 2023/2024.

Mara nne kati ya tano ilizoshiriki ilifika hatua ya robo fainali na mara moja ambayo ilikuwa ni mwaka 2003, ilimaliza katika nafasi ya tatu kwenye kundi lake.

Namba moja inavyoipa jeuri Yanga

Yanga ndio klabu ya kwanza ya Tanzania kushiriki hatua ya makundi ya Klabu Afrika ambapo ilifanya hivyo mwaka 1998 ilipotinga hatua hiyo katika Ligi ya Mabingwa Afrika na kipindi hicho hatua hiyo ilikuwa inachezwa kwa mara ya kwanza.

Mabingwa hao watetezi wa taji la Ligi Kuu, ndio klabu ya kwanza ya Tanzania kutinga katika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo ilifanya hivyo mwaka 2016 ilipomaliza katika nafasi ya mwisho katika kundi lake.

Kuashiria kwamba Yanga ina bahati ya namba moja, msimu uliomalizika, Yanga ilikuwa timu ya kwanza ya Tanzania kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, tangu mashindano hayo yalipoanzishwa mwaka 2003.

Noti juu ya noti

Kitendo cha Yanga na Simba kucheza katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, kinaihakikishia kila timu kiasi kikubwa cha fedha ambacho ni zaidi ya Sh 1.7 bilioni kutoka CAF, kiasi ambacho kinaweza kuongezeka zaidi iwapo timu inafanya vizuri na kusogea hatua za juu za mashindano hayo.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, timu inayoishia hatua ya makundi kwa kushika nafasi ya tatu au ya nne kwenye kundi lake, inapata kiasi cha Dola 700,000 huku ile inayoingia hatua ya robo fainali inavuna Dola 900,000.

Timu inayoishia hatua ya nusu fainali inapata kiasi cha Dola 1.2 milioni, ile inayoshika nafasi ya pili inapata kitita cha Dola 2 milioni na bingwa wa mashindano hayo anapata Dola 4 milioni.

Chama kiboko

Clatous Chama ndiye mchezaji pekee aliyepo katika vikosi vya Simba na Yanga hivi sasa ambaye yupo katika chati ya wachezaji 10 wanaoongoza kwa kufumania nyavu katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na mabao 20 sawa na Dioko Kaluyituka na Mouhcine Lajour.

Mabao hayo ya Chama yanamfanya awe katika nafasi ya nane kwenye chati hiyo ya wafungaji bora wa muda wote wa Ligi ya Mabingwa Afrika huku akiachwa kwa mabao 19 na mchezaji anayeshikilia rekodi ya mfungaji bora wa muda wote kwenye mashindano hayo ambaye ni nyota wa zamani wa TP Mazembe, Tresor Mputu.

Samatta, Ngassa hawana mpinzani

Wachezaji wawili wa Tanzania, Mbwana Samatta na Mrisho Ngassa wanaendelea kutamba na historia yao ya kuwa wachezaji pekee kutoka Tanzania ambao wamewahi kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa mashindano ya klabu Afrika ambapo wote kwa nyakati tofauti walifanya hivyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Aliyeanza kufungua milango ya neema ni Mrisho Ngassa ambaye aliibuka mfungaji bora wa mashindano hayo mwaka 2014 alipomaliza akiwa amepachika mabao sita sawa na El Hedi Belameiri (ES Setif), Haythem Jouini (Esperance) na Ndombe Mubele wa AS Vita.

Msimu uliofuata wa 2015, Mbwana Samatta akafuata nyayo za Ngassa kwa kuibuka mfungaji bora wa mashindano hayo akipachika mabao saba sawa na Bakri Al-Madina aliyekuwa akichezea Al Merrikh ya Sudan.

Hapa hatumjumuishi aliyekuwa straika wa Yanga, Fiston Mayele aliyeshinda tuzo ya mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, sababu si raia wa Tanzania.

Neema ya pointi 56.5

Katika msimu wa 2023/2024, Tanzania Bara ilipata fursa ya kuwakilishwa na klabu nne kwenye mashindano ya klabu Afrika kutokana na kukusanya pointi 56.5 katika mfumo wa ukokotoaji alama za ushiriki wa mashindano hayo katika kipindi cha miaka mitano kwa klabu za nchi husika.

Timu hizo nne ni Yanga, Simba, Azam FC na Singida Fountain Gate ambapo Azam na Singida Fountain Gate zilijikuta zikitolewa katika hatua ya awali ya mashindano hayo.

Ukiondoa kupata fursa ya kuwakilishwa na klabu hizo nne, Tanzania imenufaika na pointi hizo 56.5 ilizokusanya katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kwa kupanda hadi nafasi ya sita katika chati ya ubora wa nchi katika mfumo huo wa ukokotoaji alama.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI NA AZAM FC LEO....MBRZAILI SIMBA APANIA 'KUUA MMBU KWA RUNGU'...