Home Habari za michezo VITA YA UFUNGAJI HUKO LIGI YA MABINGWA AFRIKA SIO POA

VITA YA UFUNGAJI HUKO LIGI YA MABINGWA AFRIKA SIO POA

CAF

Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi inaanza leo kwa mechi mechi mbili za kibabe, Yanga ikiwa ugenini Algeria dhidi ya CR Belouizdad, huku kule Misri chama la Fiston Mayele, Pyramids FC likiwaalika mabingwa mara tano wa Afrika, TP Mazembe ya DR Congo.

Wekundu wa Msimbazi, Simba watatupa karata ya kwanza kesho katika mechi yao ya Kundi D dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kupitia makala haya, Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mastaa wanaoweza kuibuka na kiatu cha ufungaji bora kutokea timu kadhaa zinazoshiriki kutokana na viwango vyao walivyovionyesha msimu uliopita ingawa haina maana lazima wajitokeze tena.

Mahmoud Kahraba (Al Ahly SC)

Nyota huyo ambaye hucheza kama winga wa kulia ni mmoja wa mastaa wanaotegemewa zaidi ndani ya kikosi cha mabingwa mara 11 wa Afrika Ahly, kutokana na kiwango kizuri alichonacho huku akibeba matumaini ya timu hiyo ya kutetea tena taji hilo walilolibeba msimu uliopita.

Msimu uliopita alikuwa nguzo imara na kuifikisha fainali timu hiyo na kuchukua Ligi ya Mabingwa Afrika huku akifunga pia mabao sita.

Peter Shalulile (Mamelodi Sundowns FC)

Raia huyo wa Namibia amekuwa na kiwango bora na Mamelodi na msimu huu tayari ameipa ubingwa wa michuano mipya ya African Football League kwa kufunga bao moja katika ushindi wa 2-0, kwenye mchezo wa marudiano na Wydad Casablanca ya Morocco.

Shalulile anategemewa tena kuendeleza makali yake huku ikikumbukwa msimu uliopita alikuwa mfungaji bora wa michuano hiyo baada ya kufunga jumla ya mabao sita kama ilivyotokea pia kwa nyota wa Al Ahly, Mahmoud Kahraba waliolingana mabao.

Percy Tau (Al Ahly SC)

Katika michuano ya African Football League msimu huu, Tau ni moja ya nyota wa Al Ahly ambao walishindwa kuonyesha makali kwenye michezo yote miwili ya robo fainali dhidi ya Simba ingawa huwezi kumuhukumu sana kutokana na uwezo alionao.

Kuonyesha sio mchezaji wa kiwango kidogo, msimu uliopita Tau alihusika katika mabao mengi (10) kwenye Ligi ya Mabingwa akikichezea kikosi hicho cha mabingwa watetezi ambapo aliifungia matano na kuasisti mengine matano.

Kennedy Musonda (Yanga)

Musonda hajaanza vizuri ndani ya timu hiyo chini ya kocha, Miguel Gamondi ila ubora wake kwenye kufunga kama ataendelea kupewa nafasi inaweza kuleta faida kubwa kwa Yanga licha ya mastaa, Stephane Aziz Ki na Maxi Mpia Nzengeli kung’ara.

Mbali na Musonda ila Aziz Ki na Maxi wamekuwa ni wachezaji ambao wanatarajiwa kuwa na mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho katika michuano ya msimu huu kutokana na kiwango kizuri wanachoonyesha kwani wamefunga mabao saba ya Ligi Kuu Bara kila mmoja.

Kwa msimu uliopita Musonda alishika nafasi ya pili kwa wachezaji waliohusika na mabao mengi (6) kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo alifunga matatu na kuasisti mengine matatu akipitwa na Mayele aliyehusika katika 10.

Hata hivyo, Musonda na wachezaji wenzake watapaswa kukaza msuli zaidi katika kundi lao la ‘D’ ambalo limezungukwa na timu kubwa kali kama mabingwa watetezi wa michuano Al Ahly (Misri), CR Belouizdad (Algeria) na Medeama kutokea nchini Ghana.

Fiston Mayele (Pyramids FC)

Mayele anakumbukwa zaidi msimu uliopita akiwa na Yanga ambapo alionyesha kiwango kizuri na kuisaidia timu hiyo kufika hadi fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza kanuni ya mabao ya ugenini dhidi ya USM Alger ya nchini Algeria.

Msimu uliopita akiichezea Yanga aliibuka mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufunga mabao saba huku pia kwenye Ligi Kuu Bara akiibuka kinara kufuatia kufunga 17 sawa na nyota wa Simba Mrundi, Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’.

Hata hivyo, Mayele atakuwa na kibarua cha kuendelea kuonyesha ubora wake kutokana na kundi gumu la ‘A’ iliyopo Pyramids linaloundwa na timu mbalimbali za Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), TP Mazembe (DR Congo) na Nouadhibou ya Mauritania.

Clatous Chama (Simba SC)

Msimu huu nyota huyu hajaanza vizuri ndani ya kikosi cha Simba ingawa amekuwa msaada mkubwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kama alivyofanya msimu uliopita ambapo alifunga jumla ya mabao manne na kuchangia pia moja la asisti.

Licha ya kiwango chake kudorora msimu huu, Chama huwezi kumtoa moja kwa moja katika vita ya ufungaji kwani ana uwezo mkubwa wa kupika mabao na kufunga akishika nafasi ya nane katika chati ya wafungaji bora wa muda wote wa Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na mabao 20.

Nyota mwingine anayeweza kuisaidia timu hiyo ni mshambuliaji, Jean Baleke aliyefunga mabao saba ya Ligi Kuu Bara hadi sasa.

Hussein El Shahat (Al Ahly SC)

Nyota mwingine atakayeangaliwa zaidi ni El Shahat ambaye uwezo wake ni mkubwa jambo ambalo linaifanya Al Ahly kufanya vizuri kutokana na mastaa bora iliyonayo huku akiwa amefunga mabao manne msimu uliopita na kuchangia matatu ‘Assisti’.

SOMA NA HII  BAADA YA KUANZA KUICHEZEA YANGA..'SURE BOY' AAMUA KUANIKA YOTE YA AZAM..AGUSI ALIVYOTENDWA...