Home Azam FC KWA HILI LA FEI TOTO LIPO LA KUJIFUNZA

KWA HILI LA FEI TOTO LIPO LA KUJIFUNZA

Habari za Michezo

Feisal Salum ‘Fei Toto’ ameendelea pale pale alipoishia. Si ajabu amezidi kuwa wa moto zaidi akiwa na jezi ya Azam FC. Kama alivyomtungua Aishi Manula katika pambano la Nusu Fainali ya ASFC la Simba na Yanga pale Mwanza ndicho anachoendelea kufanya akiwa na timu yake Azam.

Anafunga mabao ya kuvutia akiwa na Azam, lakini katika chati ya ufungaji anamfukuzia kwa karibu Stephane Aziz Ki wa Yanga. Wakati Aziz Ki ana mabao 10 yeye ana mabao manane. Nadhani amefunga mabao mengi katika kipindi kifupi tofauti na alivyokuwa Yanga. Wachambuzi wa takwimu hawana muda wa kuweka rekodi hizi kwa sababu hazipokelewi vizuri uswahilini.

Hata hivyo, Fei haimbwi. Hakuna anayepiga kelele. Kwanini aimbwe wakati anacheza Azam? Kuna wachezaji wanafunga mabao mazuri lakini kwa sababu hawapo Simba na Yanga basi hatuwapigii sana kelele na wala mabao yao hatuyaposti mitandaoni kwa mbwembwe kama mabao ya kina Pacome Zouzoua.

Kama Feisal angekwenda Simba basi kiwango hiki hiki ambacho kinatumika na Wanayanga kumsifu Pacome ndicho kiwango kile kile ambacho watu wa Simba wangekuwa wanamsifu Fei. Tatizo kubwa Fei amekwenda katika klabu ambayo haina mashabiki wengi kama wa Simba na Yanga. Amekwenda katika klabu ambayo nadhani hata wachezaji wa kigeni hawapewi sifa wanazostahili.

Naamini hata kina Kipre Tchetche hawakupewa sifa wanazostahili kwa sababu walikuwa Azam. Vipi kuhusu James Akaminko? Unadhani anaweza kusifiwa kama ambavyo Mudathir Yahya anasifiwa pale Jangwani au Fabrice Ngoma anavyosifiwa pale Msimbazi? Hapana. Mpira wetu una utamaduni wake.

Kipimo kikubwa cha mchezaji wa Tanzania ni pale anapokuwa katika mazingira ya Fei sasa hivi. Zaidi ni kama umewahi kucheza hizi timu ukasifiwa kisha ukaondoka. Ni tofauti kidogo na yule ambaye hajawahi kuchezea licha ya kuwa staa sehemu nyingine. Hii ni hasa kwa wachezaji wa ndani. Wachezaji wa nje hawana mapenzi ya dhati na timu hizi. Wamezijulia ukubwani. Ndio maana siku ile mnyama alipochapwa 5-1 na Yanga wakati kina Jean Baleke wakicheka na Wacongo wenzao, Shomari Kapombe na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ walikuwa wanalia katika benchi.

Fei Toto anapitia katika kipindi bora kabisa kwa sasa. Akifunga hasifiwi sana. Azam ikiwasili mkoani hakuna msafara wa bodaboda wa kuwapokea. Hata ndani ya uwanja ameona namna ambavyo waamuzi wapo tayari kuinyonga Azam kwa urahisi tu tofauti na kule alikotoka. Kama Fei ni mwanadamu mwenye hisia basi kuna vitu atakuwa anawaza sasa hivi.

Anapata pesa nyingi na maslahi makubwa kuliko Yanga, lakini yupo katika kipimo cha kuonyesha kama kweli yeye ni mchezaji wa kulipwa ambaye anataka kuishi kwa ajili ya mpira na sio mambo mengine-yo. Kwamba lengo lake la kwanza ni pesa na kuitumikia timu yake kwa namna inavyowezekana bila ya kujali sifa.

Kuna wachezaji walishindwa mitihani hii. Anko wangu Mrisho Ngassa alishindwa. Alinunuliwa kwa pesa nyingi na Azam akalipwa mshahara mkubwa, lakini aliichezea Azam huku mawazo yake yakiwa Yanga. Timu yake kipenzi. Ujinga wa mwisho zaidi aliowahi kuufanya ni pale alipovaa na kuibusu jezi ya Yanga katika pambano moja la Azam. Tabia ya utoto iliyopitiliza ambayo ilisababisha Azam waachane naye.

Lakini kuna mastaa wengi wazawa ambao waliamua kuzitosa dili nzuri za klabu mbalimbali za ndani na nje ya Afrika. Hii yote ni kwa sababu ya kupenda kucheza mpira wa sifa wa Uwanja wa Taifa. Shukrani kwa wachezaji kama Mbwana Samatta na Simon Msuva ambao kwa nyakati tofauti waliamua kwenda kucheza nje huku wakiwa wanaimbwa na mashabiki wa Kitanzania.

Usiseme kwamba waliondoka kwa sababu klabu zao zililipwa pesa nzuri na klabu zilizowataka. Hapana. Uamuzi wa mwisho unabakia kuwa wa mchezaji. Na kama mchezaji mwenye-we akisema kwamba hataki kuondoka basi viongozi wa Simba na Yanga huwa wanafurahi kwa sababu mara zote wamekuwa wakiuza wachezaji kwa roho upande.

Tusubiri kumtazama Fei mpaka mwisho wa safari yake. Ukisikia anataka kwenda Simba au kurudi Yanga basi ujue atakuwa ‘amemiss’ maisha yake ya zamani. Maisha ya ufalme mitaani na mitandaoni. Sidhani kama timu hizi zina ubavu wa kushindana kipesa na Azam kama Azam wakiamua jambo lao. Labda kama atakuwa ameisha kimpira.

Kama ataendelea kuichezea Azam kwa misimu minne na zaidi au akaamua kwenda kucheza soka la kulipwa nje basi huenda akawa ametufundisha kitu. Kwamba yeye ni mchezaji halisi wa kulipwa ambaye anajali maslahi yake bila ya kujali sifa kama alivyokuwa anajinasibu wakati akisisitiza kuondoka Yanga kuhamia Azam.

Akiweka mfano huo huenda akawafumbua macho baadhi ya wachezaji vijana ambao mara zote wamekuwa wakitamani zaidi kuchezea timu hizi kimapenzi kuliko maslahi. Wapo waliofanya hivi mara nyingi na leo wameishia katika majuto makubwa. Maisha yao yamekuwa duni huku wakiwa na majuto ya kukataa ofa nyingi kubwa za zamani kwa ajili ya sifa za Uwanja wa Taifa.

Kwa wenzetu kitu cha kwanza ni maslahi. Bukayo Saka alilelewa na Arsenal tangu akiwa na miaka sita, lakini leo amekuwa staa katika timu na bado mazungumzo yake ya mkataba huwa yanachukua hadi miezi sita kwa ajili ya kupigania maslahi yake. Mifano ya wachezaji wa namna hii ni mingi. Wachezaji wanaotofautisha kazi na mapenzi.

Hongera pia ziende kwa baadhi ya wachezaji wetu walioenda nje na kung’ara bila ya kupitia Simba na Yanga. Wapo kina Nizar Khalfan, Novatus Dismas, Thomas Ulimwengu na wengineo. Hawa walivunja ule mwiko kwamba unapokuwa kijana mdogo Mtanzania basi ndoto yako kubwa ni kucheza Simba au Yanga.

Lakini hongera pia itakwenda kwa Fei kama atacheza Azam kwa nidhamu baada ya kukatiza boda kutoka katika mapenzi na kutua katika maslahi zaidi, huku akiwa hapa hapa nchini. Inanikumbusha mastaa wawili wa zamani wa Yanga, Edibily Jonas Lunyamila na Nico Bambaga ambao waliwahi kuikimbia Yanga na kutua Malindi ya Zanzibar kufuata pesa za tajiri wa Kihindi Noushad Mohammed.

SOMA NA HII  DJUMA WA SIMBA KUIBUKIA KMC