Home Habari za michezo HALI MBAYA YA MAHUJAA FC YAMBAGIHA MANYANGA BARESI

HALI MBAYA YA MAHUJAA FC YAMBAGIHA MANYANGA BARESI

Mashujaa imecheza mechi nane mfululizo bila kupata ushindi katika Ligi Kuu Bara, kitu kimemfanya Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ kuamua kubwaga manyanga kwa kuandika barua ya kujiuzulu kukinoa kikosi hicho ikiwa ni saa chache baada ya kufumuliwa nyumbani mabao 2-0 na Tanzania Prisons.

Kocha Abdallah Mohammed ‘Baresi (wa kwanza kushoto) akiwa na baadhi ya wasaidizi wake katika timu ya Mashujaa kwenye moja ya mechi ya Ligi Kuu Bara ya hivi karibuni.

Mara ya mwisho kwa Mashujaa kushinda mechi ya ligi ilikuwa Septemba 16 ilipoifumua Ihefu kwa mabao 2-0 mjini Kigoma, lakini baada ya hapo ni mechi mbili tu ilizovuna pointi kwa kutoka sare, huku sita nyingine ikipoteza na kuifanya timu hiyo iteme jumla ya 22 katika mechi nane zilizopita na kumtisha hadi Baresi.

Baresi alitua Mashujaa akitokea Tanzania Prisons akimpokea Meja Mstaafu Abdul Mingange aliyeipandisha daraja kutoka Ligi ya Championship kabla ya kocha huyo kuachana na timu hiyo na tangu atue aliiongoza mechi tatu za awali ikishinda mbili na kutoka sare moja kabla ya mambo kumharibikia.

Awali tetesi za Baresi kutaka kuachana na timu hiyo zilikuwepo tangu wiki iliyopita ikidaiwa kuwapa viongozi taarifa ya kuachana nao mara atakapomaliza mechi mbili zilizokuwa mbele yake ikiwamo ile ya Tabora United iliyoisha kwa sare ya 1-1 kisha jana kulala 2-0 mechi zote zikiwa za nyumbani na mara baada ya mechi ya jana aliwasilisha barua ya kuachia ngazi akiwajibika kwa matokeo hayo mabovu.

Mwanaspoti limemtafuta Baresi ili kujua ukweli ya taarifa hizo za kuachia ngazi na amekiri kwa kusema; “Ni kweli mwenendo wa timu sio mzuri, nimepeleka barua kwa uongozi, lakini bado mabosi wangu hawajajibu hivyo kila kitu kikijibiwa basi kitawekwa wazi.”

Mwenyekiti wa Mashujaa, Meja Yahya Ismail Mgaya alipoulizwa na Mwanaspoti kama klabu imepokea barua ya Baresi, alisema kwa kifupi; “Sijui lolote kwa vile nipo Dar es Salaam kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa Bodi ya Ligi, ila narejea leo kurudi mjini Kigoma, kama kutakuwa na chochote nitawafahamisha.”

Baresi anaachana na timu hiyo ikiwa imecheza mechi 11, ikishinda mbili, sare tatu na kupoteza sita na kuvuna jumla ya pointi tisa tu, ikifunga mabao manane na kufungwa 15, ikiwa kwenye nafasi ya 15 kati ya timu 16 za ligi hiyo inayoongozwa kwa sasa na Azam yenye pointi 25 ikicheza mechi 11, ikizidi Yanga na Simba zinazofuata nyuma ya timu hiyo katika msimamo huo.

SOMA NA HII  MAYELE ALISTAHILI TUZO MBELE YA HUYU MWAMBA