Home Habari za michezo HIKI HAPA NDIO KINACHOENDA KUTOKEA KWA YANGA NA GAMONDI WAKE

HIKI HAPA NDIO KINACHOENDA KUTOKEA KWA YANGA NA GAMONDI WAKE

SHUGHULI iliingia mvua katika dakika za mwisho mwisho za pambano la Yanga dhidi ya Al Ahly. Masheikh wakasimama na kuanza kula wima. Pale Percy Tau, staa wa timu ya taifa ya Afrika Kusini alipokumbana na mpira wa kichwa wa Bakari Mwamnyeto huku Djigui Diarra akiwa ametoka langoni.

Mvua ilikatika baada ya Pacome Zouzoua kufanya maajabu yake katika dakika za mwisho za pambano kwa kufunga moja kati ya mabao bora yaliyowahi kufungwa kwenye Uwanja wa Mkapa katika mechi za kimataifa. Pacome alikuwa anahitimisha siku yake nyingine bora katika jezi ya Yanga. Jamaa ni bonge la mchezaji.

Shughuli ni kama iliingia mvua kwa namna ambavyo Yanga waliiandaa mechi hii. ilikuwa ni Bacca Day. Yaani siku maalum kwa kwajili ya mlinzi wao wa kimataifa wa Tanzania na Zanzibar, Ibrahim Bacca. Yanga huwa ina siku maalum kwa ajili ya wachezaji wake.

ALSO READ
Simba, Yanga SC freshi zikijipanga zinatoboa
Kolamu 20 hours ago

Sijaelewa kwanini. Iliwahi kutokea kwa Maxi Nzingeli halafu ikaenda kwa Aziz Ki. Jumamosi usiku ikatua kwa Ibrahim Bacca. Labda ni siku maalumu ya kukubali mchango wa mchezaji klabuni. Ingeweza kufanyika tofauti kidogo.

Kuelekea mechi hii nilikuwa naona kama Yanga wameichukulia mechi kitofauti kidogo. Walijawa na kiburi. Katika midomo walikuwa wanaongea kama vile Al Ahly ilikuwa timu ya kawaida. Ungeshangaa kuona kwamba walikuwa wanaongea haya baada ya kufungwa pale Algeria na Belouzidad.

Yanga wana jeuri sana na timu yao. Ukweli wana timu nzuri ambayo inaweza kukupa kiburi. Hata hivyo, nilihofia kiburi hiki dhidi ya Al Ahly. Moja kati ya timu iliyotwaa vikombe vingi duniani. Hata hivyo, nilithibitisha jeuri hii ya Yanga mpira ulipoanza.

Walicheza vema. Walitawala mechi vema. Waliishikilia vizuri. Al Ahly walikuwa wajanja kwa kufanya mashambulizi mazuri ya kushtukiza na nusura wapate bao ndani ya dakika 10 tu za kwanza. Wakapoteza nafasi ya wazi wakati Yanga wakiwa wamepoteana.

Baada ya hapo mechi ikaenda vema uwanjani kwa kila mchezaji wa Yanga kasoro Aziz Ki tu. Hapa karibuni Aziz Ki alikuwa amechangamka sana lakini Jumamosi usiku alirudi kuwa Aziz Ki yule yule tu. Anapoteza mipira ovyo halafu hakabi. Hana madhara.

Unaweza kuelewa kwamba Maxi Nzengeli hakuwa na siku nzuri uwanjani lakini alikuwa anajitahidi. Aziz alikuwa hajitahidi. Mechi kama hizi unahitaji wachezaji wako bora wawe katika viwango bora. Muda si mrefu Pacome atakuwa mchezaji kipenzi zaidi kwa Yanga kwa sababu mara zote amekuwa na siku nzuri.

Nini kinafuata kwa Yanga? Majibu anayo Miguel Gamondi. Kila kocha ana fungate yake na mashabiki. Nadhani fungate yake inaweza kufika mwisho na mashabiki wa Yanga licha ya kutembeza vichapo vizuri kwa wapinzani wa Ligi Kuu na pia kuifikisha Yanga katika hatua hii.

Yanga wanatamani kwenda robo fainali. Wanataka wawafunge Simba mdomo. Msimu uliopita Yanga walifika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini Simba bado wakapiga mdomo kwamba ni michuano midogo kwa sababu wao wanafika robo fainali mara nyingi.

Miaka 25 tangu wafike hatua hii, Yanga wanataka wavuke. Kama hawatavuka baadhi yao wataamini kwamba Mzee Nasreddine Nabi angewafikisha. Ni kwa sababu Nabi alifanya vizuri katika msimu uliopita kiasi cha kukosa kuchukua kombe lenyewe kwa uzi mwembamba.

Sijui Gamondi atafanya nini zaidi lakini Yanga wanakabiliwa na kazi ngumu katika kundi lao. Kwa sasa wanahitaji kwanza pointi sita kutoka kwa Medeama ya Ghana. Kama ilivyo kwa Jwaneng Galaxy katika kundi la watani wao Simba hii, hawa watu wa Ghana nao walionekana kama vile wangekuwa wepesi katika kundi lao. Haijakuwa hivyo.

Medeama wamewachana wababe wa Yanga Belouzidad katika pambano la pili la kundi hili. Katika pambano la kwanza ilichukua dakika 67 kwa Al Ahly kupata bao lao la kwanza wakiwa nyumbani pale Cairo. Sio timu rahisi sana kama inavyoonekana katika makaratasi. Binafsi nilidhani hivyo na hata watu waliopanga makundi walidhani hiyo wakati walipokuwa katika nafasi ya mwisho.

Yanga watahitaji walau pointi sita kutoka kwa Medeama ili waweze kufikisha pointi saba za haraka haraka kabla ya kuwasubiri Belouzidad nyumbani. Wakati huo huo wanaweza tu kutamani Al Ahly ashinde mechi zake dhidi ya Belouzidad walau awe mbabe wa kundi na yeye ajiweke katika nafasi nzuri ya kushika nafasi ya pili.

Hesabu hizi za vidole haziwezi kufanya kazi kama Gamondi hafanyi kazi yake vema. Hatuhitaji kumfundisha kazi lakini bado Yanga wanahitaji kuimarika zaidi katika michuano hii. Inabidi pia aongeze mzunguko wa wachezaji (rotation) kwa sababu umepungua tangu Nabi aondoke.

Kabla ya kufika dirisha la usajili wanahitaji kuendelea kuimarika katika kikosi. Wachezaji kama kina Aziz Ki wanapozingua basi wachezaji wengine wachukue nafasi zao kama kina Jesus Moloko wachukue nafasi zao. Nabi alikuwa na ubora katika hili na ndio maana tulimuona kama mchawi wa kipindi cha pili cha mchezo.

Jambo jingine, licha ya ubora mkubwa wa kikosi na ubunifu mkubwa wa watu wa masoko wa Yanga lakini kuna umuhimu kidogo wa Yanga kupunguza shughuli nyingi kabla ya mechi hizi. Yanga wana shughuli nyingi siyo kidogo. Mpaka kuna wakati unajiuliza kama wanazingatia kweli mechi au?

Kinachotuziba mdomo ni ukweli kwamba wanakuwa katika kiwango bora lakini shughuli nyingi zisingekuwepo kabla ya mechi kubwa kama hii. Vinginevyo ni jukumu la viongozi na benchi la ufundi kuiona Yanga wakitinga robo fainali kwa mara ya kwanza. Waanze kwanza na mechi mbili dhidi ya Medeama.

SOMA NA HII  ORODHA YA KIKOSI CHA NAMUNGO FC KITAKACHOIBUKIA ANGOLA