Home Habari za michezo KIRAKA MPYA WA YANGA APEWA MITIHANI MITATU CHAP

KIRAKA MPYA WA YANGA APEWA MITIHANI MITATU CHAP

Yanga tayari ina uhakika wa kupata huduma ya kiraka kutoka Zanzibar, Shekhan Ibrahim Khamis, lakini fundi huyo mpya ana mitihani mitatu ndani ya kikosi hicho kutokana na mastaa anaokutana nao, huku mwenyewe akifunguka kuwa hana presha yoyote.

Shekhan aliyepewa mkataba wa miaka mitatu anamudu kucheza nafasi nne tofauti za kiungo, winga na ushambuliaji ambako tayari ndani ya Yanga zina mastaa wenye majina makubwa ambao wanaweza kumpa changamoto katika kuwania namba chini ya Kocha Miguel Gamondi.

Nyota huyo chipukizi aliyesajiliwa na Yanga akitokea vinara wa Ligi Kuu ya Zanzibar, JKU ametua akitoka kung’ara kwenye michuano ya Vijana U18 kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati ambapo Zanzibar ilitolewa kutokana na kuwa na kadi nyingi za njano licha ya kulingana na ndugu zao wa Tanzania Bara.

Kwenye eneo la kiungo ikijumuisha ukabaji na ushambuliaji lina mastaa kama Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki na Maxi Nzengeli ambao wote wanacheza eneo la mbele na wameonyesha uwezo mzuri ni mtihani kwake kutusua, wakati kwenye kiungo mkabaji kuna Khalid Aucho, Mudathir Yahya, Zawadi Mauya, Salum Abubakar na Jonas Mkude huku ni mastaa wawili tu wenye uhakika wa namba – Mudathir na Aucho.

Hivyo kama anataka kupenya ni lazima apambane kwelikweli kuwachomoa waliojitengenezea ufalme kikosini na huo ni mtihani wa pili kwake.

Iwapo Shekhan mwenye mabao mawili ZPL akitaka kutumika kama winga iwe kulia au kushoto pia ni lazima awe na maajabu zaidi ya nyota anaowakutaa Jesus Moloko, Denis Nkane, Mahlatsi Makudubela na Farid Mussa ambao chini ya Gamondi wamepoteza namba kikosi cha kwanza kutokana na mfumo anaoutumia.

Hata hivyo eneo hilo licha ya kuwa ni mtihani wake wa tatu, lakini ndiko kwenye nafuu zaidi kutoboa kulinganisha na kiungo kutokana na wachezaji wanaocheza kuonekana ndio roho ya timu kwenye michuano ya ndani na ile ya kimataifa.

Kitu anachotakiwa kinda huyo anayetajwa kuwa na miaka 18 ni kujaribu kucheza nafasi hiyo ili kuongeza ushindani wa namba kwa mawinga hao ambao wana kazi kubwa ya kufanya ili kupata nafasi.

Mwanaspoti lilimtafuta Shekhan ili kufafanua juu ya dili hilo lililokuja ghafla ikielezwa pia alikuwa akizivizwa na Simba, lakini hakutaka kuweka wazi kuhusiana na usajili wake ndani ya Yanga japo alisema ana imani kubwa na kipaji chake anaweza kucheza timu yoyote. “Suala la mimi kusajiliwa Yanga, sio wakati wangu sahihi kulizungumzia kwa vile bado ni mchezaji halali wa JKU hadi hapo nitakapoondolewa kikosini,” alisema.

“Kuhusiana na kupata nafasi endapo nitatua Yanga, hilo ni jukumu la kocha kunitumia, ila naamini kipaji changu kinaniruhusu kucheza timu yoyote Zanzibar na Bara kwani namudu kutumika katika nafasi nyingi na zote nacheza kwa usahihi.”

Shekhan aliongeza hakuna mchezaji ambaye hatamani kuzichezea timu kubwa za Bara suala lililopo ni kupata nafasi ya kuonekana na kusajiliwa.

Alisema anatamani kuendeleza kipaji alicho nacho na kuwa mchezaji atakayezungumzwa zaidi kama ilivyokuwa kwa kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ anayemtaja kuwa kioo chake kwa namna alivyokuwa akimfuatilia na kuiga mambo mengi kiuchezaji tangu zamani. Fei aliyeitumikia Yanga akitokea pia JKU kwa sasa anakipiga Azam FC.

SOMA NA HII  RASMI...MSUVA AFUNGUKA SAKATA LAKE NA KLABU YA MOROCCO...AGUSIA MKWANJA WA PESA..TFF YATAJWA..