Home Habari za michezo UFUPI CHANZO CHA DICKSON JOB KUTOPANGWA AFCON…..ISHU NZIMA ILIKUWA HIVI…

UFUPI CHANZO CHA DICKSON JOB KUTOPANGWA AFCON…..ISHU NZIMA ILIKUWA HIVI…

Habari za Michezo leo

NI ngumu kuamini, lakini ndivyo ukweli ulivyo, beki Dickson Job, ameenda katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 bila kucheza hata dakika moja.

Ndio, beki huyo wa kuaminika wa Yanga ni kati ya wachezaji 23 waliokuwa wakiunda kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars iliyoaga fainali hizo usiku wa kuamkia leo kwa kumaliza mkiani mwa Kundi F.

Hata hivyo, licha ya kuwa ni beki wa kuamini na anayetumika kwa muda mrefu ndani ya Yanga katika fainali hizo zilizokuwa za tatu kwa Tanzania kushiriki baada ya zile za mwaka 1980 ziliofanyika Nigeria na za 2019 pale Misri, Job hakuwa chaguo la kocha Adel Amrouche na hata wasaidizi wake, Hemed Suleiman ‘Morocco’ na Juma Mgunda waliokaimishwa Stars baada ya kocha mkuu kusimamishwa mechi nane na CAF.

Katika dakika 270 ambazo Stars ilikuwa kwenye fainali hizo za Ivory Coast, Job alikuwa amesugua benchi mwanzo mwisho kutokana na Adel kuwatumia na kuwaamini zaidi, Bakari Mwamnyeto ‘Nondo’ na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ aliyeacha gumzo kwenye fainali hiyo kutokana na umaridadi wake katika eneo la beki ya kati.

Wakati anaenda kwenye fainali hizo za Afrika, Job alikuwa ametumika ndani ya Yanga kwa dakika 720 kupitia mechi nane kati ya 11 ilizocheza katika Ligi Kuu Bara akitumika zote kwa dakika 90 kila mchezo.

Ndani ya Yanga, Job anacheza sambamba na Nondo na Bacca na ni michezo mitatu tu ndio hakutumika, kwani wenzake hao wamemzidi ujanja kwenye kikosi cha Stars na timu imeaga akiwa benchini kwa kukosa nafasi.

TATIZO HILI HAPA

Hata hivyo imebainika staa huyo licha ya ubora wake kinachomnyima nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza ni umbile lake.

Kwa kimo Job ana urefu wa futi 5’6, akiwa ndiye mchezaji mfupi katika safu ya beki ya kati ya Taifa Stars na hata Yanga, kwani Nondo urefu wa futi 6’1″ wakati Bacca yeye ni futi 5’10”.

Beki mwingine wa kati aliyepo Stars ambaye pia hakutumika ni Abdulmalik Zakaria kutokea klabu ya Namungo mwenye urefu wa mita 1.87 (sawa na Sentimita 187 au futi 6′ 2″ akiwa ndiye mrefu zaidi kikosini, huku Abdi Banda anayecheza Richards Bay ya Afrika Kusini naye analingana urefu na Nondo, wakati Gift Fred anayecheza pamoja na Job, Bacca na Nondo ndani ya Yanga ana urefu wa mita 1.83 (sawa na sentimita 183 au futi 6) akiwa ni wa pili kwa urefu nyuma ya Nondo.

Inaelezwa, ishu ya kuwa mfupi kwenye eneo la beki ya kati hata Job mwenyewe anajua na mara kaadhaa amekuwa akiambiwa na makocha kubadilisha nafasi ili acheze beki wa pembeni, kama alivyowahi kutumika mara kadhaa Yanga ilipokuwa chini ya Nasreddine Nabi na hata Miguel Gamondi.

MAKOCHA WAMSHAURI

Inadaiwa kocha Gamondi alishamwambia kimo chake hakimpi uhuru wa kucheza kwa ubora zaidi eneo la beki wa kati.

Gamondi alimtaka mchezaji huyo kumhamishia kucheza eneo la beki wa pembeni kutokana na kimo chake lakini mwenye ameomba kuendelea kuaminiwa eneo la beki ya kati kwani ndio sehemu anayoimudu zaidi kucheza.

Wakati hilo likibainika hivyo Yanga, laklini hata kwa Stars imesemekana pia kocha Adel Amrouche alibaini upungufu huyo kwenye eneo la kimo chake licha ya ubora alionao hali ya kutompa nafasi katika michezo yote iliyopita ya Afcon, ukiwamo ule wa Morocco ambao aliusimamia mwenyewe na Stars kulala 3-0.

Hata kwenye michezo miwili iliyopita dhidi ya Zambia ulioisha kwa sare ya 1-1 na ule ya juzi usiku uliisha kwa suluhu dhidi ya DR Congo na kuitupa nje Stars kwa kuambulia pointi mbili tu kama Zambia pia hakupewa nafasi na kaimu kocha mkuu, Hemed Morocco na badala yake Nondo na Bacca waliliamsha.

Mbali na kushindwa kupata nafasi ya beki wa kati, mwenyewe hupenda kucheza katika kikosi cha Stars, ila hata kwenye beki ya kulia nako imekuwa ngumu kupata nafasi kutokana na uwepo wa Haji Mnoga na Lusajo Mwaikenda umemzuia kuingia kikosini kutokana na ubora wa wachezaji hao ambao hucheza kiasili eneo hilo.

Aliyekuwa kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi alishawahi kunukuliwa akisema; ”Job ni mfupi lakini ana umakini kwenye mipira ya juu na ni mchezaji mzuri wa kuanzisha mashambulizi kuanzia nyuma.”

“Kutokana na kimo chake nimekuwa nikimtumia kulingana na mpinzani husika na ndio maana muda mwingine nimekuwa nikimtumia kati na wakati mwingine beki wa pembeni kwani ni mchezaji mzuri na mtulivu awapo na mpira anasambaza mashambulizi,” alinukuliwa Nabi.

WASIKIE WAKONGWE

Kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Amri Kiemba ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa soka akizungumzia juu ya kimo cha Job, alisema licha ya kimo hicho bado beki huyo ni miongoni mwa mabeki bora katika Ligi ya Tanzania.

“Job anapaswa kupewa heshima kulingana na anayoyafanya ndani ya Yanga na Taifa stars bila ya kuangalia zaidi kimo chake kwani kila mmoja anakifahamu lakini akipewa nafasi ni mchezaji mzuri,” alisema Kiemba na kuongeza;

“Anajijua ni mfupi, hivyo mara nyingi anakuwa makini kucheza mipira ya juu anayohisi akichelewa itakuwa na madhara, pia ni bora kwenye kuanzisha mashambulizi na kumiliki mpira hizo ndio sifa zake kuu.”

Stars eneo la beki wa kati lina machaguo manne ambayo ni Job, Mwamnyeto, Bacca na Abdi Banda ambaye anacheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Beki za zamani wa kimataifa aliyewahi kutamba na timu za Pamba, Simba, Kajumulo na Taifa Stars, George Masatu aliwahi kukikiri kila anapomuona Job akicheza hujihisi ni yeye enzi akiupiga kwani naye alikuwa mfupi na alisimama pia beki wa kati.

“Job ni kama mimi tu, kuna vitu akiviongeza atakuwa mkali kama ilivyokuwa enzi zangu, ni kweli ni beki wa kimo kifupi, lakini anajua kuruka kuwahi mipira, anakaba kwa akili na mwepesi kufanya maamuzi, kama nilivyokuwa nikicheza, kwa kweli namkubali sana huyo dogo,” alinukuliwa Masatu aliyewahi kucheza soka kulipwa Oman na Indonesia.

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  BAADA YA KUIMUMUNYA YANGA KAMA PIPI LEO....AHMED ALLY ATAJA UELEKEO MPYA WA SIMBA...