Home Habari za michezo HUU HAPA UKWELI ISHU YA ‘SURE BOY’ KUONGEZA MKATABA YANGA…ATALIPWA KAMA ZAMANI….

HUU HAPA UKWELI ISHU YA ‘SURE BOY’ KUONGEZA MKATABA YANGA…ATALIPWA KAMA ZAMANI….

Habari za Yanga

Kikosi cha Yanga tayari kimeshatua jijini Cairo, Misri kwa ajili ya maandalizi ya mechi ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji Al Ahly itakayopigwa keshokutwa Ijumaa (Machi Mosi), lakini taarifa njema kwa wanayanga ni kwamba mabosi wa timu hiyo wamzuia kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ kwa kumpa mkataba mpya.

Kiungo huyo aliyesajiliwa misimu miwili kutoka Azam FC ameongezwa mkataba mwingine wa miaka miwili wa kuendelea kuitumikia timu hiyo iliyotinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu huu ikiwa na mchezo mmoja mkononi utakaopigwa keshokutwa ili kuamua nani awe kinara wa Kundi D linaloongozwa na Al Ahly kwa sasa.

Al Ahly ambao ndio watetezi wa taji la michuano hiyo, inaongoza msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi tisa, huku Yanga ikiwa na nane kila mmoja ikiwa imecheza mechi tano na mshindi wa mechi ya Ijumaa ataongoza kundi hilo lenye CR Belouizdad ya Algeria iliyopo ya tatu na pointi tano na Medeama ya Ghana iliyopo mkiani na pointi nne tu.

Wakati Yanga ikijiandaa na mchezo huo huku ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya 1-1 na Al Ahly katika mechi ya mkondo wa kwanza jijini Dar es Salaam, mabosi wa klabu waliamua kumpa mkataba mpya Sure Boy ili aendelee kusalia kikosini, hivyo kama kuna klabu zilikuwa zikimmezea mate, sijui mapema kwamba jamaa bado yupo sana Jangwani.

Kiungo huyo anayefahamika pia kwa jina la utani la Babu Kaju, alijiunga na Yanga katika dirisha dogo la msimu wa 2021/22 kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kuachana na Azam aliyokuwa ameichezea tangu 2007, inaelezwa amepewa mkataba huyo baada ya ule wa awali kuwa ukingoni na benchi la ufundi bado linahitaji huduma yake.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, kimesema kuwa, kiungo huyo ameongezwa mkataba wa miaka miwili ili aendelee kuitumikia timu hiyo inayotetea taji la Ligi Kuu Bara na Kombe la ASFC.

“Ni kweli ameongezwa mkataba na viongozi hivyo mtaendelea kumuona sana kwenye viunga vya timu hii kuhusiana na makubaliano ni baina ya muajiri na mwajiriwa,” kimesema chanzo hicho.

Chanzo hicho kimesema mkataba aliopewa kiungo huyo hauna maboresho yoyote ataendelea kulipwa kama ilivyokuwa awali ambapo inasemekana alikuwa akilipwa Mil 3.5 ,walivyofanya makubaliano alipokuwa anajiunga na timu hiyo.

Alipotafutwa Sure Boy ili aweze kuzungumzia suala hilo na amekiri ameongeza mkataba na timu hiyo.

“Ni kweli nimeongeza mkataba, lakini suala la kuzungumzia ni mkataba wa muda gani nauachia uongozi maana wao ndio wenye jukumu hilo,” amesema Sure Boy na kuongeza;

“Kazi yangu ni kupambana uwanjani nitazungumza kwa vitendo kulingana na namna nitakavyoipa timu matokeo mazuri uwanjani.”

Kiungo huyo msimu huu amecheza mechi sita akitumika kwa dakika 331 hana bao wala asisti katika mashindano yote wanayoshiriki Yanga, tofauti na msimu uliopita timu ikiwa chini ya Nasreddine Nabi alifunga bao moja la Ligi Kuu na kushiriki kwa sehemu kubwa ya mafanikio ya Yanga kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kulikosa taji kwa kanuni za bao la ugenini mbele ya USM Alger ya Algeria.

SOMA NA HII  HII HAPA MASHINE YA MAGOLI YA MARUMO ILIYOWAINGIZA VITANI MABOSI WA SIMBA NA YANGA...