Home Habari za michezo KISA SARE NA AZAM FC JUZI…MASTAA SIMBA WAPEWA ‘MAKAVU LIVE’…KIBADENI ‘ATAPIKA NYONGO’…

KISA SARE NA AZAM FC JUZI…MASTAA SIMBA WAPEWA ‘MAKAVU LIVE’…KIBADENI ‘ATAPIKA NYONGO’…

Habari ya Simba leo

ALIYEKUWA mchezaji na Kocha wa Zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni amewataka wachezaji wa Simba kujituma na kujitolea kwa ajili ya klabu, vinginevyo wataukosa ubingwa kwa mara nyingine tena msimu huu.

Amesema wachezaji wa timu hiyo wanaonekana kama wamekuwa wakiridhika mapema hasa wanapokuwa wakipata ushindi katika mechi mbili mfululizo na kutoitolea macho mechi inayofuata.

Kibadeni amesema wanatakiwa kujitoa na kupambana kwa ajili ya klabu kama ilivyo kwa Yanga, anaimani wakifanya hivyo watafikia malengo yanayotarajiwa ikiwemo kutwaa taji la ubingwa wa Ligi hiyo na kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Amesema hana shida na uwezo wa benchi la ufundi la Simba linaloongozwa na Abdelhak Benchikha, amebadilisha timu yao kutoka kule kucheza kwa presha hadi sasa jambo ambalo linaangushwa na wachezaji kutojitoa na kupambana.

“Kuifunga Tabora United mabao 4-0 tuliona ni kipimo cha kuweza kupambana na timu kubwa, baada ya ushindi huo tukaona Azam FC ni sawa nao na kucheza kipindi cha kwanza kwa kuridhika na kuruhusu bao licha ya kusawazisha dakika za mwisho.

Kuna kazi kubwa kwa kocha amekuwa akifanya majukumu yake vizuri ukiangalia Simba imekuwa na mabadiliko siyo kama ilivyokuwa awali, tatizo kubwa bado lipo kwa wachezaji kujitoa na kupambania timu.

Kama wasipokuwa makini wanaweza kupoteza ubingwa, maana unapoteza pointi mbili mbele ya Azam FC, unakuja kupoteza zingine kwa mwingine huku unayekimbizana naye anavuna alama tatu kila mechi,” amesema Kibadeni.

Kuhusu wachezaji wapya, Ameongeza kuwa wanahitaji muda wa kuzoea mazingira ya ligi na kutengeneza muunganiko na nyota waliopo katika kikosi cha timu hiyo tangu mwanzoni mwa msimu.

“Mapema sana kuanza kutoa maoni juu ya viwango vyoa hasa ukizingatia hawana muda mrefu kujiunga na timu na hawajapata muda wa kutengeneza muunganiko lakini kwa mechi tatu walizocheza wanaonyesha wanaweza kusaidia timu,” amesema Kibadeni.

Ameongeza kuwa Simba isipobadilika katika mechi za marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wanakazi kubwa kwa sababu wanaenda kukutana na wachezaji wanaopambana na kujitoka kwa ajili ya timu.

Simba wanakibarua kigumu leo ugenini dhidi ya Geita Gold FC, uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na Februari 15 na 23, dhidi ya JKT Tanzania na atacheza mchezo wa marudiano dhidi ya Asec Mimosas, Ivory Coast .

SOMA NA HII  CAF YAWAOKOA YANGA SAKATA LA USAJILI WA MORRISON...ATUMIWA RATIBA YOTE KWAO GHANA...MSUVA AWEKWA KANDO...