Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI NA MAMELOD….KWA HILI YANGA ‘MMEPUYANGA’ SANA …

KUELEKEA MECHI NA MAMELOD….KWA HILI YANGA ‘MMEPUYANGA’ SANA …

Habari za Yanga leo

Upende usipende. Yanga ndiyo timu bora nchini kwa msimu wa tatu mfululizo. Hakuna ubishi. Huo ndiyo ukweli. Wako kwenye dunia yao kwa sasa. Kila mchezaji anaitaka mechi. Kila mechi kwao ni fainali. Wakipoteza mechi moja, wanakupa uhakika wa kushinda mechi 10 mfululizo.

Nimesikitika kuona eneo la mzunguko ambalo kimsingi ndilo hubeba watu wengi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa watu wataingia bure.

Kuna uwezekano mkubwa mechi kubwa wikendi hii kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ikawa hii ya Yanga dhidi ya Mamelodi Sundowns na kama kwa ukubwa wa Wanajangwani bado hawawezi kujaza uwanjani kwa kulipia, kuna mahali bado tunakwama.

Timu yenye mastaa kama Pacome Zouzoua, Stephano Aziz KI, Dickson Job, Djigui Diarra, Mudathir Yahya, Yao Athohoula, watu wanaingia bure? Hili linafikirisha Kidogo. Kwa ukubwa wa Yanga, hata mazoezi yao ambayo sio ya Kimkakati ilibidi watu walipie.

Yanga wana timu bora na wameenea. Wamekuwa na matokeo bora sana na wachezaji bora katika misimu hii. Hii sio Yanga ya kwenda kuiona bure kwa Mkapa. Ni Yanga inayoshawishi kila mtu kwenda kuwatazama.

Mechi dhidi ya Mamelodi ndiyo gumzo Afrika kwa sasa maana inakutanisha timu mbili zenye ushawishi. Mamelodi ni kubwa kuliko Yanga, lakini Yanga ni timu inayopanda kila kukicha.

Dar es Salaam ni jiji lenye wakazi zaidi ya milioni sita. Uwanja wa Mkapa una uwezo wa kubeba watazamaji karibu 60,000. Kimahesabu, unahitaji asilimia moja tu ya wakazi wa Dar es Salaam kujaza Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Mechi ya Yanga na Mamelodi ina uwezo wa kuwaleta watu kutoka Zanzibar, Mkoa wa Pwani na Morogoro. Kushindwa kuujaza uwanja kwa kulipia kuna mahali soka letu bado linakwama. Kila watu 100 wa Mkoa wa Dar es Salaam, ukipata mtu mmoja tu wa kwenda uwanjani kwa Mkapa kunajaa.

Bado soka la Tanzania lina kazi kwenye suala la watu kulipia kwenda uwanjani. Haiwezekani kwa ukubwa na ushawishi wa Yanga wa sasa washindwe kujaza watu uwanjani kwa kulipia.

Mamelodi ni miongoni mwa timu bora kwa sasa Afrika. Watu ilibidi muda kama huu wawe wanagombania tiketi za kwenda uwanjani. Soka la bure limeshapitwa na wakati.

Kuna watu tangu Yanga itangaze mzunguko watu wataingia bure, hawataki hata kwenda uwanjani. Watu wengi wanaamini soka la bure limetawaliwa na vurugu. Hakuna starehe ya bure. Tunahitaji kufanya tafiti kujua sababu za watu kusuasua kwenda uwanjani kutazama timu zao.

Tanzania mechi pekee yenye uhakika wa kujaza uwanja ni Simba na Yanga. Hapa hauhitaji hata kupiga kelele. Watu kutoka kila kona ya nchi utawaona. Tofauti na hapo, hata mechi ya timu yetu ya Taifa huwezi kujaza Kwa Mkapa kirahisi.

Timu bora nchini haiwezekani ishindwe kujaza uwanja. Huu ni muda wa Yanga kuitetemesha Afrika. Wametengeneza timu kwa muda na sasa taratibu wamejipata. Mechi kama hizi ndizo zinatakiwa kuwapa ukubwa wa Afrika.

Ili uwe timu kubwa ni lazima uweze kushindana na wakubwa. Mamelodi wamefanya uwekezaji mkubwa sana lakini bado na wao sio wakubwa sana Afrika.

Wamefanikiwa sana kutawala soka la Afrika Kusini lakini bado wana kazi kubwa kwenye kutawala Afrika. Ni Mabingwa mara moja tu wa Ligi ya Mabingwa Afrika. Pale kwa Madiba wameua ufalme wa Kaizer Chiefs na Orlando Pirates, lakini bado sio wababe wa soka la Afrika. TP Mazembe, Zamalek, Al Ahly ndio wafalme wa Afrika. Bado Mamelodi haijafika daraja hili ingawa haiondoi ukweli ina timu bora.

Ni wakati wa kuzichangia timu zetu na kwenda kupata burudani. Soka ni starehe kama zilivyo starehe nyingine. Kama tukienda bar au klabu za usiku tunalipa, kuwaona Yanga na Mamelodi, ilibidi tulipe pia.

Yanga imewekeza pesa nyingi sana kwa wachezaji wa daraja lao. Mechi ya Yanga na Mamelodi ilipaswa kuwa mtoko wa Pasaka na mashabiki hasa walioko Dar es Salaam waipokee kitofauti.

Simba imeweka viingilio mechi yake dhidi ya Al Ahly ingawa haikupi uhakika kama watu watajaa. Huku inabidi tutoke haraka sana. Ukubwa wa Simba kujaza Kwa Mkapa inabidi liwe jambo la kawaida. Inabidi watu waanze kuzoea kulipa.

Shirikisho la Soka nchini, Bodi ya Ligi Kuu Bara na wadau wengine ni lazima kulitafakari hili.

Kwa ukubwa wa mechi na kwa kuzingatia ubora wa Yanga wa sasa, Uwanja wa Mkapa ulipaswa kujazwa na mashabiki wa kulipia.

Kuna hili pia!

Mamelodi inacheza soka la kisasa. Wale ni wazungu watupu. Hawana mambo ya nje ya uwanja. Yanga na kocha wao Gamondi inabidi kuiandaa timu sawa sawa. Kwenye mechi hizi za mtoano ni vizuri kuepuka kwa gharama yoyote bao la ugenini. Presha ya tamko la Serikali na mashabiki kuna namna yamewashtua Mamelodi. Moja ya changamoto za kocha Gamondi ni pale yanapohitajika mabadiliko ya haraka wakati mchezo unaendelea.

Amekuwa mzuri sana kwenye kuwasoma wapinzani na kuanzisha kikosi bora lakini kwenye mabadiliko, amekuwa mzito kidogo. Hizi ni aina za mechi ambazo kila kitu kinapaswa kufanywa kwa usahihi. Moja kati ya maeneo ambayo mtangulizi wa Gamondi, Kocha Nasreddine Nabi alikuwa bora sana ni suala la mabadiliko ya wachezaji sahihi kwa nyakati sahihi.

Gamondi amekuwa na wachezaji wale wale anaowatumia sana. Anawachezaji wengi wazuri lakini hana kikosi kipana.

Hakuna uwiano wa wachezaji wa kwanza na wachezaji wa akiba. Ana kikosi tu cha kwanza bora lakini wanaotoka benchi wengi hajawapa muda wa kutosha uwanjani.

Akimkosa Khalid Aucho, Sure Boy na Jonas Mkude kuna muda wanapata tabu kwa sababu ya kukosa dakika za kutosha uwanjani. Mechi ya nyumbani kwa soka la Afrika hakuna unachohotaji zaidi ya ushindi.

Yanga inatakiwa kumfunga kwanza Mamelodi nyumbani kabla ya kuwaza jambo lolote.

Mamelodi ina timu nzuri sana lakini inafungika pia. Ili uwe timu kubwa, unahitaji kucheza mechi kubwa na kushinda. Kila la heri Wananchi.

SOMA NA HII  ROBERTINHO ATAMBA AWAPA NENO HILI MASHABIKI

2 COMMENTS

  1. Tuachie Yanga yetu, umeambiwa wananchi hawana pesa ya kulipia, Yanga imeona itupe burdani ya bure twende kufurahia mchezo

  2. Basi, Sumba izichukue hizo zilizoachwa na Yanga ili wanunue wachezaji wenye kuitaka kila mechi, ama vipi mwandishi wetu?