Home Habari za michezo HII ROBO FAINALI SIMBA, YANGA BADO KITENDAWILI

HII ROBO FAINALI SIMBA, YANGA BADO KITENDAWILI

Yanga SC na Simba SC

Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ya makundi inaendelea kwa kuingia raundi ya tatu wikiendi hii, leo kukiwa na mechi tatu ikiwamo ya Yanga itakayokuwa ugenini kuvaana na Medeama ya Ghana.

Mechi nyingine za leo ni ile ya Al Ahly dhidi ya CR Belouizdad pamoja na ile ya Etoile du Sahel na Al Hilal, kabla ya kesho Jumamosi kupigwa michezo mingine minne ukiwa ule wa Wydad itakayoialika Simba jijini Marrakech, Morocco.

Hadi sasa ni kwamba hakujapambazuka kwa timu zote juu ya kupata mwanga wa nani ataingia robo fainali au nani atakwamia makundi, kwani hadi raundi ya pili inakamilika hakuna klabu iliyokuwa imejihakikishia kuingia robo fainali kama ambavyo hakuna klabu iliyokatiwa tamaa kuingia hatua inayofuata ya robo fainali.

Mashabiki wa soka wameshuhudia matukio yasiyotarajiwa kama vigogo kuangushwa lakini nyingi kati ya timu zilizokuwa nyumbani ziliitumia faida hiyo kupata pointi muhimu.

Hapa nyumbani macho, masikio na mioyo ya wapenzi na mashabiki ni katika kundi B na D zilizopo Simba na Yanga mtawalia, kwani hadi tunapoandika makala hii, hakuna mmoja kati ya hao wawili aliyeandikisha ushindi, si nyumbani si ugenini.

Katika kundi la B, Simba inashika nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa juu ya timu yenye matokeo hasi na yasiyotarajiwa yaani mabingwa wa zamani na wanafainali wa msimu uliopita Wydad Athletic Club ya jijini Casablanca, Morocco.

Wydad imepoteza michezo yote dhidi ya timu zinazoongoza kundi hilo, Asec Mimosas na Jwaneng Galaxy. Simba ililazimishwa sare ya 1-1 na Asec ya Ivory Coast katika mchezo wao wa kwanza uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Simba ilishindwa kuulinda utangulizi wao wa bao moja lililopatikana kwa penalti iliyokwamishwa wavuni na kiungo mshambuliaji kutoka Burundi, Saido Ntibazonkiza.

Kipindi cha pili Asec ilisawazisha bao hilo na kuwafanya Simba waridhike na pointi moja ya nyumbani.

Baada ya mtanange dhidi ya Asec, Simba ilisafiri kwenda Francistown, Botswana kupambana na timu iliyowatoa hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa miaka miwili iliyopita yaani Galaxy.

Mchezo huo uliomilikiwa kwa kiasi kikubwa na Simba, ulishuhudiwa timu hizo zikitoshana suluhu. Asec na Galaxy zinaongoza kundi hilo, huku zote zikiwa zimejikusanyia pointi nne yaani moja kutoka kwa Simba na tatu kutoka kwa Wydad AC.

Pamoja na matokeo hayo, Simba na Wydad wanaotifuana kesho Jumamosi huko Morocco, wote wana nafasi ya kupindua matokeo na kupenya kwenye tundu la robo fainali japo shughuli yao ni mlima mrefu.

Wanafainali wa Kombe la Shirikisho msimu uliopita, Yanga, wanaburuza mkia katika Kundi la D wakiwa na pointi moja waliyoipata kwa kulazimisha sare ya 1-1 dhidi ya Mabingwa Watetezi ambao pia ni Mabingwa wa Misri, Al-Ahly ya Cairo.

Ilibidi Yanga wasubiri dakika za jioni sana kuweza kusawazisha bao la kichwa lililofungwa na Percy Tau katika dakika ya 87. Kiungo mshambuliaji Pacome Zouzoua aliwainua mashabiki kwenye Uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa, huku wengi wakiwa wameanza safari ya kurejea nyumbani wakijua wamepoteza mchezo huo.Yanga walianza mchezo wa kwanza kwa kufungwa ugenini nchini Algeria na timu ya CR Belouizdad ambapo pamoja na kutawala umiliki na takwimu nyingi za mchezo walijikuta wakiambulia kipigo cha magoli 3-0. Katika kundi hili pia imo klabu ya Medeama ya Ghana ambayo inaikaribisha Yanga jioni ya leo. Medeama, kama ilivyokuwa kwa Yanga ilianza kwa kupigwa magoli matatu mbele ya Mabingwa wa kihistoria Al Ahly ya Cairo. Hata hivyo, Medeama ilijitutumua nyumbani katika mchezo wa pili na kuwalaza wababe wa Yanga, CR Belouizdad kwa bao 2-1.

Belouizdad inakwenda kutupa karata yao dhidi ya Ahly katika mchezo ambao utaonyesha kama mabingwa hao wa Algeria wanaweza kwenda ugenini kuendeleza ubabe waliowafanyia Yanga au ilikuwa ni nguvu ya soda.

Je, Yanga wataendelea kusalia mkiani mwa kundi hili na kufifisha matumaini ya kuingia robo fainali? Mchezo wa leo dhidi ya Medeama kwenye Uwanja wa Baba Yara, jijini Kumasi utajibu sehemu ya swali hili.

Kundi A la michuano hili laweza kuwa pengine kundi lenye matokeo yasiyotarajiwa hadi sasa kwani mabingwa wa zamani Mamelodi Sundowns ya Afrika ya Kusini na TP Mazembe ya Congo DRC, Pyramids ya Misri na Nouadhibou ya Mauritania kila moja imeshinda mchezo mmoja mmoja.

Mamelodi na Pyramids ya Misri ndizo zilikuwa zinapewa nafasi ya kushinda kundi hili, hata hivyo Mamelodi iliyoshinda mchezo wa kwanza dhidi ya FC Nouadhibou kwa mabao 3-0, iliangukia pua jijini Lubumbashi mbele ya Mabingwa wa zamani TP Mazembe ambao wanaonekana kukitafuta kiwango chao cha zamani kilichowapa ubingwa wa Afrika mara tano.

Timu ya FC Nouadhibou pengine ilikuwa miongoni mwa fungu la kushangaza pale ilipowapiga Pyramids kwa mabao 2-0. Katika kundi hili yawezekana hata michezo ya mwishoni mwa juma isitoe picha halisi ya nani atakwenda robo fainali.

Mabingwa wa kwanza wa Ligi ya Afrika (African Football League), Mamelodi pengine watakuta kina cha maji ni tofauti na walivyotarajia japo wanaongoza kundi hilo kwa faida ya mabao ya kufunga. Michezo yao miwili ijayo dhidi ya Pyramids ni muhimu sana ili kujihakikishia robo fainali.

Kundi C linaongozwa na Petro du Luanda ya Angola ambayo ndiyo timu pekee iliyovuna pointi 6 katika mechi mbili za kwanza ikizifunga Al Hilal ya Sudan bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa 11 de Novembro, jijini Luanda. Matajiri hao wa mafuta walienda kushinda ugenini nchini Tunisia kwa kuifunga Etoile du Sahel kwa 2-0. Al Hilal ya Sudan inayotumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kama wa nyumbani Dar es Salaam, iko kwenye nafasi ya pili ikiwa inajivunia pointi 3 ilizozivuna kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Esperance ya Tunisia pale ilipoandikisha ushindi wa 3-1.

Michezo ya makundi ya mwishoni mwa juma hili inaweza isitoe mustakabali wa ni timu zipi zitafuzu robo fainali lakini inaweza kutoa mwanga wa nani ataenda nani atabaki.

Mwandishi wa Makala hii ni katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania. Unaweza kumtumia maoni yako kupitia namba yake ya simu iliyoko hapo juu.

SOMA NA HII  YANGA YAZIDI KUNOGA NA VIFAA VIPYA,SIMBA NAO WAMO, KESHO NDANI YA CHAMPIONI JUMAMOSI