Home Habari za michezo YANGA vs MAMELOD NI JIWE KWA JIWE….VITA IPO KWA MASTAA HAWA….PACOME NI...

YANGA vs MAMELOD NI JIWE KWA JIWE….VITA IPO KWA MASTAA HAWA….PACOME NI ZAIDI YA WOTE…

Habari za Michezo leo

HESABU za kila mdau wa soka nchini kwa sasa ni namna Yanga itatoboa kwenye mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wapinzani wake Mamelodi Sundowns kutoa Afrika Kusini ambao wanatisha kinoma, lakini kuna mwamba huyo kutokea Jangwani ambaye amefunika wakali wa timu zote hizi mbili kwa takwimu za kibabe.

Kiungo fundi wa mpira, Pacome Zouzoua wa Yanga, ana takwimu ambazo hakika zitawapasua vichwa Mamelodi ambao watatafuta namna ya kumdhibiti.

Pacome, ambaye alifunga mabao mawili makali ya ‘kusepa na kijiji’ yanayofanana katika mechi dhidi ya Al Ahly na dhidi ya Medeama, ndiye anayeshika nafasi ya pili ya ufungaji wa mabao wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu akiwa na mabao matatu na ametoa asisti moja. Amezidiwa na mtu mmoja tu, Sankara Karamoko wa Asec Mimosas, ambaye ana mabao manne na asisti moja, lakini mshambuliaji huyo hayupo tena barani Afrika baada ya kuhamia Ulaya, hivyo utawala umebaki kwa Pacome.

Kiungo huyo fundi wa timu ya Wananchi pia ndiye anayeongoza michuano yote kwa kupata alama nyingi zaidi (rating) kwa kiwango anachoonyesha katika kila mechi akipata alama 7.99 akifuatiwa na Mustafa Ahmed wa Al Ahly mwenye alama 7.93 na Karamoko ana alama 7.74.

Pacome pia anashika nafasi ya pili katika chati ya wachezaji waliotengeneza nafasi nyingi kwenye michuano ya mwaka huu akitengeneza nafasi 17 nyuma ya Mohammed Chid wa Pyramids aliyetengeneza nafasi 19.

Staa huyu wa Ivory Coast pia yumo ndani ya 10-Bora ya wachezaji wakali wa kupiga chenga zilizofanikiwa akiwa na asilimia 53, ambazo hakuna mchezaji wa Mamelodi anayemfikia, huku anayemkaribia zaidi kutoka kwa mabingwa hao wa Afrika Kusini ni Mbrazil, Ribeiro mwenye asilimia 42.

Moja ya matukio ya kutisha ya uwezo wa chenga za Pacome, aliuonyesha wakati alipowalambisha nyasi kipa na beki wa CR Belouizdad na kutoa asisti ya bao la pili alilofunga Kennedy Musonda wakati Yanga ilipowachakaza mabingwa hao wa Algeria kwa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Timu hizo zitakutana kwa mara ya pili baada ya awali kuwahi kukutana kwenye mechi za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2001 na Yanga kupasuka kwa jumla ya mabao 6-5, kwani ilianza kwa kufungwa ugenini 3-2 kisha kulazimishwa sare ya mabao 3-3 nyumbani na kutolewa na Wasauzi.

Pia zinakutana huku Mamelodi ikitoka kutwaa ubingwa wa michuano mipya ya Afrika (African Football League), huku Yanga ikitinga hatua ya robo kwa mara ya kwanza tangu ilipocheza makundi mara ya kwanza 1998, baada ya michuano hiyo kubadilishwa jina na mfumo kutoka Klabu Bingwa Afrika mwaka 1997.

Yanga pia inakutana na Mamelodi ikiwa inatambia kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na kulikosa taji kiduchu kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini iliyowabeba USM Alger ya Algeria kwani matokeo ya jumla yalikuwa sare ya 2-2, Yanga ikichapwa nyumbani 2-1 na kushinda ugenini 1-0 kwa bao la penalti ya Djuma Shaban.

Ukitazama makaratasi, Mamelodi ipo juu sana kulingana na Yanga lakini uhalisia wa soka bado unatoa imani kwa Yanga kutoboa mbele ya Wasauzi hao.

Kuanzia uwekezaji, bajeti ya timu, gharama za wachezaji, ukubwa wa benchi la ufundi na rekodi kwenye michuano ya CAF, Mamelodi imeitupa mbali Yanga lakini bado Wananchi wana jeuri kwenye dakika 180 za uwanjani katika mechi ya nyumbani na ile ya ugenini kutokana na ubora walioonyesha kwenye michezo ya michuano hiyo msimu huu.

Jeuri ya Yanga ipo kwenye ubora wa kikosi chake kwa sasa na namna timu hiyo inavyocheza kwa umoja, ushirikiano, kasi kujitoa na ufundi kiasi. Hapa ndipo Yanga inapovimba.

Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea uhalisia wa soka na jeuri ya Yanga ilipo kwenye mtu na mtu (1v1) katika vikosi vyote viwili na namna mechi inavyoweza kuamuliwa kulingana na mchezaji mmoja mmoja katika nafasi wanazocheza na hasa watakapokuwa kwenye ubora wao. Hapa mabilioni ya Mamelodi hayahusiki, kinachotembea ni boli tu na vita nzima itakavyotokea kwenye mechi mbili za timu hizo kuanzia ile ya kwanza ya nyumbani itakayopigwa Machi 29-30 kisha marudiano Aprili 5-6.

DIARRA vs WILLIAMS

Hapa ndio mipira mingi itafika kwenye mechi hizo. Kwa makipa Djigui Diarra wa Yanga na Ronwen Williams wa Mamelodi wote ni bora katika maeneo yao.

Wawili hao wote walifanya makubwa katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023, zilizopita wakiwa makipa namba moja wa timu zao ambapo Diarra aliifikisha Mali robo fainali huku Williams akiifikisha Afrika Kusini nusu fainali.

Viwango vyao kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu, vinatofautiana, Williams anashika nafasi ya pili kwa ujumla wa mashindano kama kipa ambaye amecheza mechi nyingi za makundi bila kuruhusu bao (5), huku Diarra akishika nafasi ya 12 baada ya kumaliza michezo miwili tu bila kuruhusu bao.

YAO VS ALLENDE

Upande wa kulia wa Yanga ni kati ya maeneo bora kwenye kulinda na kushambulia. Huku anacheza Muivory Coast, Kouassi Attohoula Yao ambaye hadi sasa ana asisti saba kwenye ligi na amefunga bao moja katika Ligi Kuu.

Kutokana na mifumo ilivyo, Yanga na Mamelodi wanaelekea kufanana namna ya timu zinavyocheza kwa kutumia viungo wengi na kwa Mamelodi upande huo mara nyingi hucheza Mchile Marcelo Allende.

Hapo wanakutana vijana wawili wenye ubora mkubwa wa soka hivyo bato yao uwanjani haitakuwa kinyonge kama wakipangwa wote. Allende ana asisti mbili hadi sasa kwenye michuano hii.

LOMALISA vs ZWANE

Upande wa kulia pia wa Mamelodi wanatumia zaidi viungo na eneo hili anayecheza mara kwa mara ni, Msauzi, Themba Zwane.

Ni moja ya wachezaji wazoefu na mwenye ubora mkubwa kikosini hapo lakini kwa upande wa Yanga anaweza kukutana na Mkongomani Joyce Lomalisa ambaye ni mzoefu na bora pia.

Huku kutakuwa ni shoo ya wakongwe wa hizi kazi kwani Zwane ana miaka 34 huku Lomalisa akiwa na 30.

JOB vs RIBEIRO

Eneo la ulinzi la Yanga wakisimama wazawa Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’, huwa linakuwa imara zaidi.

Hata hivyo, eneo hili Mamelodi pia ni noma kwani huongozwa na Mbrazil Lucas Ribeiro ambaye atakutana na Job ambaye anasimamia safu ya ulinzi ya Yanga. Hapa itakuwa bato ya akili na ujanja tu. Ribeiro anaongoza orodha ya ufungaji ligi ya Afrika Kusini akiwa na mabao 10.

BACCA vs SHALULILE

Kitasa Bacca hii ni nafasi yake ya kuendelea kujizolea ujiko kama ataweza kumdhibiti mshambuliaji hatari wa Mamelodi, Mnamibia Peter Shalulile.

Shalulile ndiye roho ya Mamelodi kwenye kutengeneza mabao lakini pia Bacca ndiye nguzo ya eneo la ulinzi la Yanga.

Bato ya wawili hawa kama watapangwa pamoja itakuwa ya akili, ufundi, undava, kasi na ubabe. Kwa sasa Shalulile ana mabao manne kwenye ligi, lakini kwa Bacca atatakiwa kuwa makini kwa kuwa anashika nafasi ya pili kwa kadi nyingi za njano kwenye michuano hii msimu huu akiwa nazo tatu, moja nyuma ya Sadio Kanoute wa Simba.

AUCHO/SURE BOY vs LORCH

Dimba la kati la Yanga kuna wataalamu Mganda, Khalid Aucho na Mbongo Salumu Abubakar ‘Sure Boy’. Wote hawa wanacheza kwa ubora na itategemea kocha Miguel Gamondi atampanga nani kwenye mechi hii kwani Aucho kwa sasa ana majeraha.

Kivyovyote vile, yeyote atakayeanza huenda akakutana na fundi Msauzi, Thembinkosi Lorch, wenyewe wanamuita Nyosso.

Wachezaji wote hawa ni wazoefu na bora kila mmoja kwenye eneo lake hivyo tutajarie bato la kitalaamu zaidi.

NZENGELI vs MASHEGO

Kama Mkongomani Maxi Nzengeli mwenye mabao tisa kwenye ligi atapata nafasi ya kucheza mechi hizo basi huenda akakutana na beki kisiki, Msauzi, Terrence Mashego anayecheza eneo la kushoto la Masandawana.

Wawili hawa wote wana kasi lakini pia ni wabunifu. Nzengeli anaweza kukaba na kushambulia, hivyo hivyo kwa Mashego ambaye ni beki wa kupanda na kushuka. Itakuwa mwendo wa kasi tu huku.

MUDATHIR vs MOKOENA

Eneo ambalo linaweza kuamua mechi hizi ni hili la viungo wa kati wa Mamelodi, Teboho Mokoena na Mudathir Yahya wa Yanga.

Hapa ndipo injini za timu zote mbili zipo kwa sasa na wawili hao ni wachezaji tegemeo kwenye vikosi hivyo.

Mudathir na Mokoena wote wako kwenye viwango bora kwa sasa, Mudathir akiwa na mabao manane kwenye ligi lakini Mokoena akiwa mkali wa kutengeneza nafasi, kuzuia na kupiga pasi. Huku Muda tayari ana mabao mawili CAF, Teboho Mokoena akiwa anaongoza kwa pasi zenye kuwafikia walengwa kwa asilimia 78.9.

 MUSONDA vs LEBISA

Musonda amekuwa akiaminiwa na kupewa nafasi ya kuanza kwenye mechi za kimataifa kama namba tisa mbele ya Clement Mzize na Joseph Guede.

Kama Mzambia huyo mwenye asisti mbili kwenye Ligi ya Mabingwa atapata nafasi kwenye mechi hii basi ataenda kukutana na beki mtulivu Mosa Lebusa anayeiongoza safu ya ulinzi ya Mamelodi.

Lebusa ni mzoefu na moja ya mabeki hodari zaidi nchini Afrika Kusini akiwa Mamelodi tangu mwaka 2018. Akili itaamua hapa.

AZIZ KI vs KEKANA

Yanga kwa sasa inamtegemea Stephane Aziz Ki akiwa kinara wa mabao (12) lakini pia ametoa asisti sita katika Ligi Kuu Bara. Mechi kubwa kama hizi ndio maeneo yake lakini duru hii atakutana na beki kisiki, Grant Kekana.

Huyu ni mtaalamu sana wa kukaba na kunusa hatari akiwa na uzoefu kwenye kikosi cha Masandawana alichojiunga nacho mwaka 2021, akitokea SuperSport United.

Aziz Ki ana namba nzuri kwenye Ligi ya Mabingwa akiwa ameshatengeneza nafasi nne za hatari zaidi na amehusika kwenye mabao matatu ukijumlisha mabao na asisti.

PACOME vs MUDAU

Utaalamu mwingine kwenye mechi hii utakuwa unapatikana eneo hili. Ni kwa staa wa Yanga, Muivory Coast, Pacome na beki wa Mamelodi Khuliso Mudau.

Wawili hawa wote mali ipo mguuni, kasi ya kutosha lakini pia ni injini za timu zao.

Pacome hadi sasa ameifungia Yanga mabao saba kwenye ligi na kutoa asisti nne lakini kwa upande wa Mudau amekuwa kinara wa kuanzisha mashambulizi kupitia upande wa kulia. Kwenye Ligi ya Mabingwa Pacome anaonekana kwenye maeneo mengi, tayari ana mabao matatu nyuma ya Sankara Karamoko anayeongoza akiwa na manne, lakini pia akiwa na asisti moja.

GAMONDI vs MOKWENA

Vichwa vya makocha Miguel Gamondi wa Yanga na Rhulani Mokwena wa Mamelodi navyo vitakuwa na kazi kubwa ya kuamua mbinu za mechi hii. Hapa kiufupi atakayepanga silaha zake vyema ndiye ataivusha timu yake hatua ya robo kwenda nusu fainali. Wote ni wakali na wanalijua boli hivyo vichwa vitakunwa kinoma. Mokwena ameipa Mamelodi taji la AFL wakati Gamondi ameifikisha Yanga robo fainali na kuifanya kuwa timu kutoa dozi za 5G. Moto utawaka!

SOMA NA HII  KWA SIMBA HII YA KOCHA MHISPANIA...LITAKUFA JITU WALAH...AURUDISHA MFUMO WA MASOUD DJUMA..